WAFANYAKAZI wa Kiwanda cha Nguo cha Urafiki cha Dar es Salaam jana waligoma wakishinikiza kulipwa mshahara wa sh 150,000 badala ya ya sh 80,000.
Mgomo huo umekuja baada ya wiki iliyopita kupewa mshahara wa sh 80,000 wanazosema katika marekebisho ya mishahara yaliyotangazwa hivi karibuni na Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, John Chiligati, kiwanda hicho si moja ya viwanda vilivyoruhusiwa kulipa kiwango hicho.
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa masharti ya kutotajwa majina, wafanyakazi hao walisema siku moja kabla ya kupewa mishahara hiyo, kila mfanyakazi alipatiwa barua iliyosainiwa na Meneja Utawala, Mosses Swai, ya kumjulisha kuwa wameruhusiwa na wizara kuwalipa kima cha chini cha sh 80,000 badala ya sh 150,000 kama ilivyotangazwa hapo mwanzo.
Barua hiyo yenye kumb. Namba PF/2702762 ambayo Tanzania Daima iliona nakala yake, ilieleza kutokana na ruhusa hiyo, marekebisho ya mishahara yao itakuwa ni sh 82,000 kwa mwezi badala ya sh 70,000 kama walivyokuwa wanalipwa mwanzo na marekebisho hayo yataanza rasmi Januari mosi mwaka huu.
Wafanyakazi hao walisema baada ya kupata barua, waliwasiliana na tawi la wafanyakazi la Urafiki (TUICO) na kuwaeleza kutoridhishwa na maamuzi hayo. Na TUICO walikwenda kuonana na uongozi na walipouliza walipewa majibu ya kutoridhisha.
Mbali na kugomea mshahara huo, pia wanamtaka Waziri Chiligati au mwakilishi wake kwenda kuzungumza nao na kuwachambulia sababu ya wao (wizara) kuruhusu kiwanda hicho kuwalipa wafanyakazi wake mshahara huo bila ya wao kushirikishwa.
“Tutaendelea hivi hivi na mgomo wetu hadi hapo waziri atakapokuja, kwani barua tuliyopewa na uongozi hatuiamini kama kweli wameruhusiwa.
“Isitoshe mshahara wanaotupa haulingani na kazi tunazozifanya kutokana na wao mwaka jana kufukuza vibarua wote kwa madai kwamba wasingeweza kuwalipa kiwango kilichotakiwa na serikali, hivyo kwa sasa badala ya mfanyakazi kuendesha mashine nane, anaendesha mashine 16, kwa nini wasituongeze huo mshahara?” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Huang Li-lan, alisema mgomo huo si halali kutokana na kile alichoeleza kwamba haukufuata taratibu na sheria za kazi. Alisema kutokana na hali hiyo hata tawi lao la wafanyakazi halina taarifa ya mgomo huo.
Huang aliwasihi wafanyakazi wenye nia ya kufanya kazi waendelee na kazi na kama kuna malalamiko yoyote kuhusiana na utendaji kazi, basi wayapitishe kwenye tawi la TUICO kama taratibu zinavyosema.