RAIS Jakaya Kikwete, amewataka watumishi wa umma kuacha umangimeza na kujiona ni mabwana mkubwa, bali wanapaswa kutambua kuwa wapo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
Rais Kikwete alisema hayo jana kwenye hafla ya uzinduzi wa awamu ya pili ya programu ya kuboresha utumishi wa umma itakayotekelezwa kuanzia mwaka huu hadi 2012 ambayo itagharimu dola milioni 103.8 za Marekani.
“Tuache umangimeza na kujiona kuwa sisi ni mabwana mkubwa na wananchi si lolote. Tutambue kuwa tupo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na siyo vingenevyo, hivyo kazi ya kuwaelimisha watumishi ili kutambua wajibu wao huo iwe ni ya kudumu…..nawaomba msichoke kuifanya,” alisema.
Alisema hiyo inatokana na ukweli kwamba sehemu kubwa ya maboresho ya utumishi wa umma yanalenga katika kubadilisha taratibu, tabia na utamaduni wa kazi uliozoeleka kwa muda mrefu, hivyo kubadilika kifikra na kimtizamo ni jambo la lazima.
Alisema wananchi wana haki ya kupata huduma nzuri kutoka kwa watumishi wa umma na si fadhila na kusema kuwa utumishi wa umma upo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
Aidha, rais alisisitiza nidhamu na utumishi wa umma unaozingatia maadili na kuwataka mambo hayo kuyapa umuhimu mkubwa, ili kujenga mafanikio na ufanisi katika kazi, jambo hilo pia limeainisha katika mpango wa pili wa maboresho.
Akizungumza kuhusu masilahi ya wafanyakazi, Rais Kikwete alisema pamoja na kuwepo na mikakati ya kuboresha masilahi ya wafanyakazi kwa nyakati mbalimbali, serikali itaendelea kuboresha masilahi.
Hata hivyo, alisema masilahi bora yanategemea kukua kwa uchumi wa nchi yetu sambamba na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya serikali.
“Uchumi unaokua kwa kasi na umakini katika ukusanyaji wa kodi ndivyo pekee vitakavyoiwezesha serikali kuwalipa watumishi wake vizuri. Lazima tufanye hayo.
“Hivyo, nawasihi ndugu zangu wote tuliomo kwenye utumishi wa umma tujitume zaidi, tufanye kazi kwa bidii na maarifa zaidi, ili kuimarisha uchumi wa nchi yetu. Kila mmoja wetu atimize wajibu wake ipasavyo, tena kwa wakati,” alisema rais.
Aidha, alisema licha ya kuwapo kwa mafanikio katika kuboresha huduma kwenye mpango wa kwanza wa maboresho ya utumishi wa umma, lakini bado kuna upungufu katika baadhi ya maeneo ambayo hawana budi kuendelea kuutafutia ufumbuzi.
Aliyataja maeneo hayo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wananchi wengi kuwa ni huduma zisizoridhisha kwa baadhi ya idara za Serikali, malalamiko yahusuyo ubabaishaji na vitendo vingi vya rushwa vikiwa vimeelekezwa kwenye sekta za elimu, afya, usalama wa raia, utoaji haki, mambo ya ndani na ardhi.
Awali, akimkaribisha rais, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, alisema mpango wa pili wa maboresho wa utumishi wa umma umekuja baada ya kumalizika kwa mpango wa kwanza mwaka 2007.
Alisema lengo ni kuimarisha utendaji na hivyo kusaidia kukuza uchumi na kuwapatia wananchi wake huduma bora.
Waziri Ghasia alisema mpango wa kwanza ulijikita katika kuweka mifumo mipya ya utendaji wa kimenejimenti katika utumishi wa umma, kuboresha matumizi ya rasilimali watu na ajira, kuboresha uongozi, menejimenti na kuboresha matumizi ya teknolojia ya kompyuta pia mifumo ya mawasiliano na utunzaji wa kumbukumbu.
Alisema mfumo huo hasa unaotumia kompyuta, na kuratibu watumishi na kutoa taarifa za kiutumishi na mishahara unatumika na umeweza kupunguza asilimia kubwa ya tatizo la watumishi hewa.
Aidha, alisema programu ya pili ni mwendelezo wa maboresho wa utumishi wa umma hasa katika mifumo ya utoaji wa huduma, kuongeza uwajibikaji, kuboresha masilahi, mifumo ya usimamizi wa watumishi na kuimarisha uongozi wa utumishi wa umma.