EDWIN Mukenya, nyota wa kimataifa timu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, alirejea nchini juzi akitokea kwao Kenya alikokuwa amekwama kwa muda mrefu kutokana na vurugu za kisiasa zinazoendelea nchini humo.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali, alisema jana kuwa Mukenya aliwasili juzi na leo anatarajiwa kujiunga na wenzake kwenye mazoezi katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Mukenya na mwenzake, George Owino, Desemba mwaka jana walikwenda kwao kwa mapumziko ya Krismasi na uchaguzi mkuu wa Desemba 27, lakini vurugu zilizotokana na matokeo ya uchaguzi huo, zikawa kikwazo.
Chanzo cha vurugu hizo ni wafuasi wa Chama cha ODM, wakiongozwa na aliyekuwa mgombea urais kupitia chama hicho, Laila Odinga, kupinga ushindi wa mgombea wa Chama cha PNU, Mwai Kibaki.
Baada ya Desemba 27, mwaka jana hali ya hofu imetanda nchini humo hata kutatiza huduma ya usafiri na shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii, hivyo wachezaji hao kushindwa kurejea kwa wakati.
Hata hivyo, Owino alifanikiwa kurejea wiki kadhaa zilizopita huku Mukenya akikwama kwao hadi juzi alipopata nafasi ya kuja nchini kwa ajili ya kuitumikia timu yake ya Simba.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Mukenya alisema amerejea baada ya kupata walau nafasi kuondoka kwani hali bado inatisha.
Mukenya alisema, vurugu hizo zimesababisha kukosekana kwa huduma ya usafiri, lakini akasema anamshukuru Mungu kwamba yu salama na akaahidi kuifanyia makubwa Simba.
Mukenya alijisajili na Simba msimu huu akitokea Yanga alikocheza kwa misimu kadhaa, amerejea huku hatua ya pili ya Ligi Kuu ya Bara ikiwa inaingia katika raundi ya pili.