jumanne, 29 Januari 2008

Lowassa kuwekwa ‘kitimoto’ bungeni

na Mwandishi Wetu, Dodoma


WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, huenda sasa akalazimika kujibu maswali ya papo hapo kutoka kwa wabunge, kutokana na kuanza kutumika rasmi kwa kanuni mpya za Bunge zilizofanyiwa marekebisho makubwa.

Wakati hayo yakitokea, wabunge kadhaa wameonya kuwa wakati umefika sasa kwa Bunge kuacha kukwepa wajibu wake wa kuisimamia serikali, kwani kwa kufanya hivyo Bunge linajipotezea hadhi yake.

Wakizungumza na gazeti hili jana kabla ya kikao chao cha kupatiwa maelezo kuhusu mkutano wa 10 wa Bunge unaoanza leo, wabunge hao walisema ‘urafiki’ unaojengeka baina ya Bunge na serikali hauwezi kulisaidia taifa.

Wengi wa wabunge hao waliokuwa wa upinzani walibainisha kuwa hoja zinazotolewa na kambi hiyo bungeni hazilengi katika kufanya siasa, kwani siasa zikiingizwa bungeni nchi haitasonga mbele.

Kutokana na hali hiyo, walitaka kutokuwapo kwa ubabaishaji wakati kanuni ya Waziri Mkuu kujibu maswali itakapoanza kutumika, na kusema kuwa hiyo itumike kama fursa ya kutoa maelezo kuhusu matatizo ya wananchi yatakayoulizwa na wabunge kwa niaba yao.

Hata hivyo, ingawa hiyo ni moja ya kanuni mpya zilizoingizwa kwenye toleo jipya la Kanuni za Bunge, jana haikuelezwa kinagaubaga iwapo itaanza kutumika mara moja sambamba na kanuni nyingine.

Kanuni hiyo ya Waziri Mkuu kujibu maswali ya moja kwa moja, imenukuliwa kutoka Bunge la Uingereza kulikotengwa muda maalumu kwa wabunge kumuuliza Waziri Mkuu maswali kuhusu mambo mbalimbali.

Kwa kawaida, maswali yanayoulizwa bungeni huwa yamewasilishwa muda mrefu uliopita katika wizara husika na watendaji kuyatafutia majibu yanayosomwa bungeni.

Ofisa Habari Mkuu wa Bunge, Ernest Zullu, jana alithibitisha kuanza kutumika kwa kanuni mpya na kusema kuwa kanuni iliyothibitishwa kuanza kutumika ni ile ya wabunge kuimba wimbo wa taifa katika mkutano wa kwanza.

“Kanuni zimeshakamilika ingawa hazijachapishwa, baadhi yake zitaanza kutumika mara moja na itakayoonekana mapema ni ile ya wabunge wote kuimba wimbo wa taifa...wabunge wataimba wote kwa maneno wimbo huo mara baada ya maandamano ya Spika,” alisema Zullu.

Hata hivyo, Zullu alisema kuwa katika masuala yaliyozungumzwa katika kikao cha faragha cha wabunge wote jana mchana, haikuelezwa iwapo kanuni hiyo ya Waziri Mkuu kujibu maswali nayo itaanza kutumika.

Alisema kwamba kilichojadiliwa na kukubalika katika kikao hicho cha wabunge ni kuanza kutumika kwa kanuni ya kuimba wimbo wa taifa pamoja na ile ya mavazi.

Aidha, Zullu alithibitisha kuwa ripoti ya Kamati Teule ya Bunge, iliyoundwa na Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kupitia mchakato wa mkataba wa kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond Development (RDC) ya Marekani, itawasilishwa bungeni.

“Ripoti imeshakamilika na kama mnavyofahamu ilishawasilishwa kwa Spika. Imethibitishwa kuwa ripoti hiyo itawasilishwa bungeni katika mkutano huu na ikiwasilishwa document (nyaraka) hiyo itakuwa ni ya wazi...iwapo wabunge wataamua kuijadili watafanya hivyo,” alisema Zullu.

Pamoja na ripoti ya Richmond, pia Bunge litapokea taarifa za kamati zikiwasilisha kazi zake kwa kipindi cha mwaka 2007. Ripoti hizo zinaweza kujadiliwa na wabunge iwapo wataona umuhimu wa kufanya hivyo.

Kwa upande mwingine, mjadala kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) unatarajiwa kuwa mkali hasa kutokana na kawaida ya ripoti hizo kuonyesha upotevu mkubwa wa fedha za serikali.

Mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete aliagiza kuwa ripoti hiyo iwe inajadiliwa kwa kina katika ngazi mbalimbali ili kupata dawa ya upotevu wa fedha za serikali. Inatarajiwa kuwa wabunge watakitumia kikao hiki kutekeleza agizo hilo kwa lengo la kuisaidia serikali.

Majibu ya maswali 210 yameshaandaliwa na yanatarajiwa kutolewa katika mkutano huo wa 10 utakaodumu kwa wiki tatu. Sambamba na kujibiwa kwa maswali hayo, pia miswada kadhaa ya sheria itawasilishwa na kujadiliwa.

Wakati huo huo, Mchungaji Getrude Rwakatare anatarajiwa kuapishwa leo. Rwakatare anaingia bungeni kwa mara ya kwanza leo kupitia Viti Maalumu, kuziba nafasi iliyoachwa wazi na marehemu Salome Mbatia, aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.