na Tamali Vullu
TIMU iliyoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, baada ya taarifa ya ukaguzi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kuhusu upotevu wa fedha za Akaunti ya Malipo ya Kigeni (EPA), juzi ilitangaza kuanza kazi rasmi.
Mwenyekiti wa timu hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, alikaririwa akisema wameshapata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi ambao wamejitokeza kwa ridhaa yao wenyewe kutoa maelezo kuhusiana na suala hilo.
Pamoja na hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewaomba wananchi wengine zaidi kujitokeza ili kusaidia kukamilisha kazi ambayo imepewa muda wa miezi sita.
Mwenyekiti huyo wamewahakikishia wananchi kuwa kila chembe ya habari itakayopatikana itafuatiliwa kwa makini, kwa nia ya kuhakikisha kuwa ukweli unajulikana na kuwekwa hadharani, ili kulinda heshima ya taifa.
Awali, napenda kumpokeza Rais Kikwete kwa kufikia uamuzi wa kumfukuza kazi gavana wa BoT, Daudi Ballali kutokana na ubadhirifu huo.
Ubadhirifu huo wa zaidi ya sh bilioni 133, ulibainishwa na kampuni ya nje iliyofanya uchunguzi, Ernst & Young, ambao ulibainisha fedha hizo zililipwa katika kampuni 22 zisizokuwa na nyaraka, ama zenye nyaraka batili na nyingine usajili wake haupo kwa Msajili wa Makampuni (BRELA.
Pongezi hizi kwa Rais Kikwete zitakuwa na maana zaidi na kuonekana amefanya jambo la maana katika utawala wake, iwapo wananachi watakuwa tayari kutoa ushirikiano kwa timu hiyo, ili iweze kukamilisha kazi yake.
Wananchi wenye ufahamu kuhusu suala hili wanapaswa kupeleka taarifa muhimu kwa timu hiyo, kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tunamuunga mkono rais katika maamuzi yake.
Rais Kikwete ametimiza wajibu wake, kwanza kwa kumfukuza kazi Ballali na kisha kuunda tume hiyo ambayo inamjumuisha Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), ili kuweza kuwabaini watu wengine waliohusika katika ubadhirifu huo.
Wananchi hatupaswi kuukumbatia ufisadi, tunapswa kupambana nao kwa kila hali, na hilo tutaweza na kupiga hatua mbele zaidi kwa kutoa ushirikiano kwa timu hii, kwani ufisadi gharama yake halisi ni kuzorotesha maendeleo ya nchi na kuwaneemesha wachache.
Hivyo ni wakati muafaka kwa kila mmoja kuonyesha uzalendo kwa kujitokeza na kutoa ushirikiano kwa timu hiyo, ili iweze kufanikisha jukumu lake hilo.
Kutokana na ukweli huo, ombi la timu hiyo la kuwataka wananchi kutoa ushirikiano, ili kuharakisha uwekaji sawa wa suala hili kwa hatua zaidi za kisheria, linafaa kuchangamkiwa na wananchi.
Kulingana na utaratibu walioweka, kila mwananchi si lazima awaone kama timu kwa pamoja, bali anaweza kutoa taarifa ama kwa timu au kwa mjumbe mmoja mmoja.
Dk. Willbrod Slaa, Mbunge wa Karatu (CHADEMA), ndiye aliyekuwa wa kwanza kuibua kashfa hiyo hadharani Septemba 15 mwaka jana katika viwanja vya Mwembeyanga, Dar es Salaam. Hakuna anayeweza kubisha katika hili, Dk. Slaa ameonyesha uzalendo kwa nchi yake.
Hivyo, wananchi wengi wazalendo na wanaopenda maendeleo ya nchi yetu ni vema kutumia nafasi hii, ili wote waliohusika na wizi wa fedha hizo za umma wachukuliwe hatua, kwa kupeleka taarifa na vielelezo zaidi.
Katika sakata hili, hadi sasa mtu anayetajwa zaidi kuhusika ni Balali, lakini ni dhahiri kwamba nyuma yake kuna watu wengi waliohusika katika suala hilo ambalo limesababisha hasara kubwa kwa Watanzania.
Timu hii itaweza kufanikisha majukumu yake iwapo wananchi wataendelea kuisaidia kwa kuwapa taarifa ambazo wataona ni muhimu na zinazoweza kufanikisha kazi iliyopo ya kuwanasa wahusika na kurejesha fedha hizo za umma.
Jamani tuwe na uzalendo kwa nchi yetu, watu wenye ushahidi wajitokeze mbele ya timu hiyo kuuwasilisha, kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaendeleza kazi ambayo ameianza Rais Kikwete ya kukomesha vitendo vya ufisadi nchini.