JUMLA ya sh bilioni 4.2 zimetolewa kama ruzuku kwa Asasi 23 kutoka katika mikoa 13 nchini na mradi wa Rapid Funding Envelope (RFE) ili kusaidia mapambano dhidi ya mambukizi ya virusi vya ugonjwa wa ukimwi na kazi za jamii.
Akizungumza baada ya kukabidhi vyeti vya ushiriki wa mafunzo na awamu ya kwanza ya ruzuku hiyo kwa washiriki wa asasi hizo, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Mariam, Mwaffisi, alizitaka Asasi hizo kuhakikisha wanatumia fedha hizo kwa ufasaha na malengo yaliyokusudiwa.
Alisema asasi hizo zimeaminiwa kwa kuwa wako karibu na jamii, hivyo wana jukumu la kutoa elimu ya ukimwi kwa watu wanowazunguka na mambo mengine ya kijamii.
“Hakikisheni fedha hizo zinasaidia kuwafikia wananchi wengi zaidi, kwani serikali pekee haitaweza kuifikia jamii kubwa bila kushirikiana nanyi, ninyi ndio mko nao karibu, hivyo shirikianeni katika kuutokomeza ugonjwa huu hatari kwa niaba ya serikal,” alisema.
Naye mratibu wa mradi huo, Fadhili Matumbwi alisema mradi huo unaofadhiliwa na mashirika sita ya kimataifa ambayo ni kutoka kwa watu wa Marekani USAID, Irish Aid, DANIDA, CIDA, SDC, na DFID jana imefikia awamu ya sita ambapo mashirika hayo kwa pamoja wamechangia ruzuku hiyo kwa asasi mbali mbali zilizochaguliwa nchini.
“Utaratibu uliotumika ni kwamba kabla ya kupatiwa ruzuku hii kunakuwa na asasi ambazo zinatuma maombi, mwaka huu zilikuwa asasi 475 ambazo zilichujwa na kubaki 23 ambazo kamati ya uendeshaji wa mfuko iliamua kuwachagua kutokana na kuridhika na utendaji wao na ndio hizi leo zimepokea awamu ya kwanza ya ruzuku na nyingine watapatiwa baadaye kwani kuna awamu nne kwa hiyo bado awamu tatu,” alisema Matumbwi.
Mikoa iliyonufaika na mradi huo ni Ruvuma, Shinyanga, Morogoro, Zanzibar, Mara, Arusha, Dar es Salaam, Mbeya, Kilimanjaro, Pemba, Tabora, Pwani na Tanga.