WANANCHI wa Kijiji cha Ngarananyuk, wilayani Arumeru, wamepanga kufanya maandamano kumuona Rais Jakaya Kikwete kutokana na mgogoro wa kugombea ardhi ulioibuka kati yao na Mamlaka ya Hifadhi ya Arusha (ANAPA).
Mkutano mkuu wa kijiji hicho uliofanyika jana, umeazimia kwenda kumuona Rais Kikwete, ili kupata haki yao ambayo wanadai kuwa hifadhi inataka kumega eneo lao kwa mabavu.
Mkutano huo mkuu wa serikali ya kijiji ulioshirikisha wazee wa mila wa kabila la Wameru, ulikuwa na lengo la kupata ufumbuzi kutokana na kutokuwepo kwa mahusiano mazuri kati yao na mamlaka hiyo.
Kiongozi Mkuu wa mila ya kabila la Wameru, IShimael Saanya, alisema wamefikia hatua hiyo kutokana na kukosekana kwa ufumbuzi wa mgogoro huo.
Saanya, alisema chanzo cha mgogoro huo ni Mhifadhi Mkuu wa ANAPA, Erastus Rufungilo, waliyemtuhumu kuwatuma mara kwa mara askari wa wanyamapori kwenda kuvamia maeneo yao na kukamatwa wananchi na kuwafungulia mashitaka ya kuwabambikia.
Alisema hivi karibuni kumetokea mtafaruku uliosababisha mwananchi mmoja kuuliwa kwa kipigo na askari wa hifadhi wakati mwananchi huyo alipokuwa akitetea wanakijiji wenzake 31 waliokuwa wanashikiliwa na askari hao kwa kosa la kuokota kuni kando kando ya hifadhi.
Mwenyekiti wa kijiji, Joseph Nnko, alisema mahusiano kati yao na mamlaka hiyo ni mabaya na mamlaka haina msaada wowote na hivyo kusababisha mapigano ya mara kwa mara ingawa jambo hilo wameshalifikisha kwa uongozi wa serikali ya mkoa lakini hadi leo mkoa umelifumbia macho.
Mhifadhi Mkuu wa ANAPA, Erastus Rufungilo, alipoulizwa chanzo cha mgogoro alisema ni kweli kuna mgogoro wa kugombea mashamba kati ya hifadhi na wanakijiji na akakiri kuwa yeye haitambui vizuri mipaka ya hifadhi hiyo.