KAMPUNI ya Sigara Tanzania TCC, imetoa msaada wa sh milioni 120, kwa Jeshi la Polisi, zitakazotumika kugharimia safari ya maofisa watano wa jeshi hilo kwenda nchini Marekani kuhudhuria mafunzo ya ngazi ya juu maofisa wa polisi duniani.
Akikabidhi msaada huo kwa maofisa hao, Meneja Mkuu wa TCC, Simon Matta, alisema kampuni yake imetoa ufadhili huo sawasawa na ushirikiano uliopo kati ya serikali na idara zake na sekta binafsi ambapo kwa Jeshi la Polisi ulianzishwa na jeshi hilo mapema mwaka 2006.
Mafunzo hayo ya wiki mbili yanatarajiwa kufanyika San Diego, California, nchini Marekani kuanzia Novemba 8 mwaka huu.
Matta alisema mwaka jana TCC ilifadhili safari kama hiyo ya mafunzo kwa gharama ya sh milioni 90. Aidha TCC imekuwa ikifadhili safari za maofisa hao wa polisi tangu mwaka 2001.
“Taarifa tulizozipata kutoka kwa wale waliohudhuria mafunzo hayo miaka ya nyuma zinatufurahisha sana, kwani yale waliyojifunza yamelinufaisha sana Jeshi la Polisi. Kwa sababu hiyo tumeona ni vyema tuendelee kukufadhilini tena mwaka huu,” alisema.
Matta alisema yeye na viongozi wenzake, wana imani kwamba mafunzo, uzoefu na uhusiano wa kimataifa wanaoupata katika mafunzo hayo ya kila mwaka, yatasaidia kukuza hali ya usalama nchini.
Akitoa shukrani zake, Mkurugenzi wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi hilo, Kamishna wa Polisi, Paul Chagonja, alisema jeshi lake limefaidika sana na maafisa wake kuhudhuria mafunzo ya maofisa wake nchini Marekani.
CP Chagonja alisema mafunzo hayo yanayojulikana kama IACP, husaidia kubadilishana uzoefu na kupeana mbinu mbalimbali za kijinai zinazoendeshwa na wahalifu kitaifa na kimataifa.
“Sote tunafahamu kwamba wahalifu wa nyakati hizi hawafungwi na mipaka ya kijiografia, ndiyo maana wanafanya uhalifu katika nchi moja na kukimbilia nchi nyingine kama wapemdavyo. Na kwakuwa hakuna nchi moja inayoweza kupambana na uhalifu wa namna hii peke yake, juhudi za kimataifa kama mafunzo haya ya IACP ndizo zinaonekana kuwa na mwelekeo wa kuimarisha uzoefu na mbinu zetu sisi polisi katika sura ya kimataifa,” alisema.
Katika hafla hiyo, Matta alikabidhi msaada huo kwa maofisa hao watano wanaotarajiwa kuondoka leo.
Msafara huo unaoongozwa na Kamishna Paul Chagonja, umewajumuisha Kamishna Msaidizi Ernest Mangu (Utawala), Kamishna Msaidizi, Sillas Beatus (Fedha), Kamishna Msaidizi, Anyisile Kyoso (Kompyuta na Mawasiliano) na Mrakibu wa Polisi, Susan Kaganda (Bohari Kuu ya Polisi).