MCHAKATO wa kurudisha fomu za shindano la Maisha Plus umesogezwa mbele hadi Novemba 8 mwaka huu.
Awali fomu hizo zilianza kutolewa Oktoba 15 hadi 30 mwaka huu.
Mratibu wa shindano hilo Masoud Ally ‘Kipanya’ alisema lengo la hatua hiyo ni kuwapa muda washiriki kuchukua fomu hizo kutokana na zile za awali kuwa chache kulinganisha na watu waliojitokeza kuchukua fomu hizo.
“Katika awamu ya kwanza kila kituo kilikuwa na fomu 56 ambazo zimeisha haraka tofauti na mategemeo yetu, hivyo tumeongeza nyingine na kusogeza muda wa kurudisha hadi Novemba 8, ili kuwapa nafasi waliochukua katika awamu hii ya pili kujiandaa na mchujo.” Alisema Kipanya.
Alisema mchujo wa kwanza utafanyika Novemba 11 jijini Arusha katika hoteli ya Triple A na wa pili utakuwa ni Novemba 16, Stone Club, Mwanza Hotel jijini Mwanza.
Fomu hizo zinapatikana Millenium Towers, kwenye duka la KP Wear, jijini Dar es Salaam na kwa jiji la Mbeya ni katika duka la vinywaji la Isarth Associates Co. Meta, Tanga katika ukumbi wa La Casa Chica, Dodoma Brian’s Boutique barabara ya 12, Zanzibar Ofisi za Bomba FM na Oasis Hotel, Morogoro.
Maisha Plus ni shindano lenye mtazamo wa uhalisia wa maisha ya kila siku ambapo washiriki watakuwa wakipewa kazi mbali mbali na mafunzo kutoka kwa wataalam na mshiriki anayeshindwa kufanya kazi atakuwa akitolewa kila wiki katika kipindi kitakachorushwa na televisheni ya TBC1 na mshindi atapata zawadi ya sh. Milioni 10 na washiriki wengine watapata mikataba ya kufanya matangazo na kuigiza filamu.