HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
jumanne, 4 novemba 2008
Pekua Tovuti
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari


Serikali yakiri kutumia fedha nyingi kuajiri wageni
JIBU LA SWALI LA MBUNGE Kalambo

Mhe. Ludovick Mwananzila (CCM)
 

na Rahel Chizoza na Lucy Ngowi, Dodoma


SERIKALI imekiri kwamba inaajiri wataalamu wa nje kwa gharama kubwa baada ya kupoteza wataalamu wazalendo wanaotafuta kazi nje ya nchi, ambao ni nguvu kazi ya taifa, wenye uwezo na ujuzi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, alisema bungeni jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kalambo, Ludovick Mwananzila (CCM), aliyetaka kujua hasara inayopata serikali kutokana na wataalamu wazalendo kutafuta kazi nje ya nchi kama Botswana, Namibia, Swaziland na Afrika Kusini.

Mbali na hilo, Ghasia alisema baadhi ya wazalendo hao, wanaoondoka nchini kinyemela, mara nyingine huleta matatizo yanayoiaibisha nchi na pia nchi kukosa pato la taifa.

Alisema, serikali imechukua hatua zenye lengo la kuhakikisha kuwa unakuwepo utaratibu endelevu wa kuratibu wataalamu hao ili waweze kukidhi matarajio ya serikali.

Alitaja hatua hizo kuwa ni kuanzisha mchakato wa maandalizi ya sera ya menejimenti ya uhamaji wa nguvukazi, itakayotoa mwongozo wa jumla kuhusu masuala ya utumiaji wa wataalamu wa Kitanzania waishio na kufanya kazi nje ya nchi na kuandaa mazingira yatakayoruhusu Watanzania hawa kuwekeza nchini.

“Sera hii, vile vile itaweka mfumo mzuri wa Watanzania waishio na kufanya kazi nje kusafirisha fedha zao kuja hapa nchini kwa ajili ya kuiendeleza nchi pamoja na kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwao pale serikali itakapohitaji,” alisema Ghasia.

Aliongeza kuwa, kupitia kitengo cha Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, kitaanzishwa kitengo chenye lengo la kuratibu utoaji huduma za ajira za wataalamu wazalendo ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kuandaa mikakati ya kuwavutia Watanzania walio nje ya nchi kurudi nchini na kuwapa kazi zinazohitaji ujuzi wa kipekee.



juu

Warning: mysql_connect() [function.mysql-connect]: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2) in /hermes/bosweb/web098/b983/glo.freemanm2/include/comment.php on line 9
I cannot connect to the database because: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2)