HIVI karibuni wastaafu wa Serikali Kuu wa idara na wizara mbalimbali walitoa siku saba kwa serikali ili wafanye mazungumzo kuhusu malipo ya pensheni zao. Ikishindikana, watachukua hatua stahili.
Madai ya wastaafu hao kwa serikali ni kupuuzwa mawazo yao wakati walishiriki kikamilifu kujenga taifa na kulinda amani ya nchi miaka iliyopita.
Waliitaka serikali kuacha matumizi ya nguvu za dola na kupuuza madai ya haki zao. Wastaafu hao wanadai kutolipwa pensheni zao na kwamba wameacha milango wazi kwa wizara itakapowahitaji kwa ajili ya majadiliano ya malipo hayo.
Kutokana na jambo hilo, nafikiri ni busara kwa serikali kusikiliza kilio cha wastaafu hawa kabla ya kutokea kwa hatua yoyote ambayo hatujui itakuwa na athari kiasi gani kwa taifa.
Ni aibu kwa taifa ambalo kila kukicha kuna matatizo ya serikali na watumishi wake ambao hudiriki kugoma na kuacha kufanya kazi kwa siku kadhaa, yote hiyo ni baada ya kulilia haki zao kwa muda mrefu bila mafanikio.
Mara nyingi serikali imekuwa haitaki kuonana na wahusika wanaodai haki zao mpaka wanapoamua kuandamana au kugomea kazi ndipo serikali hujitokeza.
Kuna usemi kwamba ‘kinga ni bora kuliko tiba’ kwa hiyo ni bora serikali ikafuata tamko la hawa wastaafu ili wawasikilize kilio chao kwa sababu mtu hakatai wito, hukataa maneno, siku zilizotolewa na wastaafu hao zinakaribia ukingoni.
Wastaafu hao wanapinga na kukanusha hoja ya Wizara ya Fedha na Uchumi kwamba huwa inawapa malipo ya pensheni mwanzoni mwa kipindi cha miezi sita.
Badala yake wahusika hao wanadai kuwa kumekuwa na ujanja wa unaofanywa na watendaji wa serikali kwa kutumia nyaraka zinazoonyesha hundi za pensheni hupelekwa katika Benki ya makabwela (NMB) mwanzoni mwa kila kipindi na marejesho ya wasiolipwa hutolewa ndani ya miezi mitatu.
Kutokana na hatua ya watumishi hao wa serikali waliostaafu, naamini kwamba upo ukweli unaopuuzwa, hivyo ni bora wakakutana na serikali ili kubaini lilipo tatizo.
Sababu ya yote hayo ni kwamba wastaafu wa serikali kuu wamekuwa wakidai kulipwa hundi husika inapofikisha miezi saba tangu ilipoandikwa na kupelekwa NMB wakati serikali inadai huwalipa kipindi cha mwanzo cha miezi sita. Hilo ni tatizo.
Pamoja na hayo, wanadai kuwa Wizara ya Fedha na Uchumi kwa makusudi iliondoa nyaraka stahili za serikali na wakati huo huo NMB nao wakaondoa nyaraka za kutolea fedha na kuanzisha mpango wa kadi ambao hata siku moja hauwaonyeshi ni yapi malipo stahili ya wastaafu.
Kwa mtazamo wangu nadhani serikali ionane na hawa wastaafu ili iwaeleweshe juu ya mlolongo mzima wa malipo yao yanavyokwenda, kwa sababu huenda serikali ikawa sahihi lakini kwa kuwa haitaki kuonana na wahusika, ambao wanalalamika, basi kila mtu atajua serikali ndiyo yenye makosa.
Kwa sababu wastaafu wenyewe wanadai kuwa wengi wao hawajawahi kujiunga na mfuko wa pensheni ya jamii na mashirika ya uuma, hivyo inawezekanaje Wizara ya Fedha na Uchumi, kufanya jambo hilo kwa ghafla tena bila kuwaelimisha wahusika, hali iliyosababisha usumbufu?
Ni wakati wa serikali kuwaelewesha wastaafu hao kwa sababu kama mtu haujui ukweli ulivyo, siku zote atalalamika, matokeo yake mlalamikiwa humpuuza kama wanavyodai kufanyiwa wastaafu hao.
Wanadai wao hawapingi malipo yao kupitia NMB, isipokuwa kinachowasumbua ni kulipwa fedha bila nyaraka stahiki za serikali na kumbukumbu muhimu.
Sababu hiyo inawezekana ikawa tatizo, kwani siku zote biashara bila daftari haiendi, ndiyo maana wanapiga kelele, wanalipwa lakini hawajui kimetoka kiasi gani na kimebaki kiasi gani.
Kwa mtazamo wangu, nadhani serikali ingetafakari mara mbili kabla ya wastaafu hao kuchukua hatua ambazo naamini kabisa zitakuwa mbaya, kwani jamii imechoka kuona kila kukicha watu wanaandama na kugoma, wakati kikwazo ni serikali.
Tumeshuhudia wazee wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, walivyoamua kufanya baada ya kutosikilizwa, hatimaye serikali imewapeleka mahakamani.
Uzee ni dawa, lakini pale unapothaminiwa. Wastaafu wote ni wazee, hivyo serikali inatakiwa kuwathamini.
0784 846 907
amananyembo@yahoo.com