HATIMAYE baada ya kampeni za muda mrefu, leo wananchi wa Marekani wanamchagua rais wao wa 44 kwa ajili ya kipindi cha miaka minne ijayo.
Tunachukua nafasi hii kulitakia kila la kheri taifa hilo katika uchaguzi huo na yeyote atakayeshinda ajue ana nafasi kubwa ya kuwaunganisha Wamarekani kuwa kitu kimoja.
Ni uchaguzi wa aina yake katika historia ya dunia na ndio sababu ya ulimwengu kuelekeza macho na masikio katika taifa hili kubwa.
Ni uchaguzi unaomshirikisha kwa mara kwanza mweusi mwenye asili ya Afrika, Barack Obama, kupitia tiketi ya Chama cha Democratic. Vilevile kwa mara ya kwanza nchini humo, John McCain, kupitia Chama cha Republican anaweka historia ya kuwa mtu mwenye umri mkubwa zaidi kugombea nafasi hiyo.
Yote kwa yote, Marekani lazima impate mrithi wa Rais George Bush kati ya Obama au MacCain.
Kutokana na nafasi ya Marekani duniani, tunaamini kuwa uchaguzi huo si wa Wamarekani pekee, bali ni wa dunia na Afrika kwa ujumla.
Hii inatokana na athari za kisera zinazotungwa n nchi hiyo kutoiathiri nchi hiyo pekee bali dunia yote, huku nchi zinazoendelea na zinazotegemea misaada zikiathirika kwa kiwango kikubwa.
Ukiangalia matatizo ya kifedha yanayoisukasuka dunia kwa sasa, yalianzia Marekani, kabla ya kusambaa Ulaya na Asia. Kwa hili, kiwango cha ukuaji wa sekta za kiuchumi na kitalii unatarajiwa kudumaa.
Vilevile ni sera za nje za Marekani ndizo zinazoelekeza vipaumbele vya dunia. Hivi sasa dunia yote imeelekeza macho kupambana na ugaidi, huku nyingine, ikiwamo Tanzania, ikikiuka baadhi ya vipengele vya katiba na maazimio kadhaa ya kimataifa juu ya kufuata haki za binadamu.
Sera ya ugaidi ndiyo iliyoishawishi Tanzania kutunga Sheria ya Ugaidi ya mwaka 2002, ambayo inalalamikiwa kila kona na watetezi kwa kuwa inawakandamiza raia.
Vile vile, dunia imeshuhudia masharti ya kupewa misaada ikiongezeka hasa kwa kigezo cha kupambana na ugaidi duniani. Hata hivyo wafuatiliaji wa mambo wanabainisha kuwa kiwango cha misaada kinachotolewa kukuza uchumi ama kupambana na magonjwa kama ukimwi na Malaria, kinaishia kuimarisha nchi husika katika juhudi za kupambana na ugaidi.
Hii ni mifano michache tu inayothibitisha kuwa Tanzania na Afrika kwa ujumla inaguswa kwa namna moja ama nyingine na uchaguzi huu wa leo.
Kwa hali hiyo basi, tunahusika kuwatakia Wamarekani kila la heri, kwa kumchagua kiongozi atakayefungua ukurasa mpya wa mahusiano ya Marekani na dunia kwa ujumla.
Hii ni baada ya rais anayeondoka madarakani, Bush, kujenga idadi kubwa ya maadui kati ya Marekani na nchi nyingi duniani.
Hata vikundi vinavyojitokeza hivi sasa vinavyojihusisha na ugaidi vitapungua kutokana na sera rafiki, zitakazoanzishwa na uongozi utakaowekwa madarakani na kura zitakazopigwa leo.
Vile vile tunaamini sera ya nje kuwa hata misaada itakayotolewa kwa nchi zinazoendelea haitalenga kulinda maslahi ya Marekani duniani pekee bali ni kwa ustawi wa maendeleo ya dunia.
Hakuna asiyefahamu kwamba maslahi ya kudumu ya Marekani yanatetewa na chama chochote kati ya hivi vilivyosimamisha wagombea, ndiyo maana tumebainisha hapo juu kwamba, kwa yeyote yule atakayepatikana, hatima ya dunia ipo mikononi mwake.
Kama ilivyokuwa kwa Bush, ambaye analaumiwa na sera yake iliyosababisha dunia kukosa amani, basi ndivyo hivyo, rais ajaye arejeshe amani iliyopotea.
Mungu wape Wamarekani muono wa kuweza kumpata rais atakayeweza kuirejesha dunia katika amani.