KASHFA ya kughushi saini ya mtoto yatima, Onass Edward, imevaa sura mpya baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, kufungua jalada la uchunguzi sambamba na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Sahihi ya mtoto huyo na picha yake ndivyo vilivyotumika kuuza kiwanja cha urithi cha Paul Chauka, lakini mtoto huyo anaeleza kuwa sahihi iliyotumika si yake wala hamfahamu mhusika.
Jana, Tanzania Daima, ilishuhudia watuhumiwa wawili akiwemo dalali aliyeuza kiwanja hicho na mwingine aliyempiga picha mtoto huyo iliyotumika kuhalalisha uhamishaji wa miliki wa kiwanja, wakihojiwa na polisi.
Jalada la polisi katika kesi hiyo namba MOS/IR/4399/2007 lilifunguliwa mwaka jana lakini katika mazingira yasiyofahamika, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa za kuwahoji watu wanaotuhumiwa kwa kashfa hiyo.
Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya habari zimethibitisha kuwa, kuanza upya kwa upelelezi wa kesi hiyo kunatokana na malalamiko ya mmoja wa watoto wa marehemu aliyeshangazwa na ukimya wa polisi.
“RCO wetu ameamua kulivalia njuga suala hili la kashfa ya wazi na tunataka kufahamu nani aliweka sahihi katika nyaraka zile ‘and we will leave no stone unturned’ (kila mhusika ataguswa),” kilidokeza chanzo hicho.
Upelelezi wa kashfa hiyo sasa umeshika kasi kutokana na utendaji makini wa mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Kilimanjaro, Linus Sizumwa, anayefuatilia kwa karibu suala hilo tofauti na mtangulizi wake.
Aidha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Lucas Ng’hoboko, alipohojiwa na gazeti hili jana, alisema kuwa kosa lilotendwa ni kughushi hivyo kila anayetajwa atahojiwa kubaini ushiriki wake.
Mwaka jana, Chama cha Wanasheria mkoani Kilimanjaro (KLA), kilikaririwa na vyombo vya habari kikiitaka TAKUKURU kumkamata na kumsweka rumande Jaji Jonathan.
Jonathan ambaye sasa ni wakili wa kujitegemea, ni miongoni mwa majaji wa kwanza wa Tanzania baada ya uhuru, aliyewahi kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha na Dodoma.
Sakata la kukamatwa kwa jaji huyo mstaafu linatokana na kashfa iliyoanzia kwenye kiwanja ambacho mtoto yatima wa miaka 14 anadaiwa kusainishwa nyaraka kuwa ameuza kiwanja cha urithi kwa sh milioni 10.
Mtoto huyo, mwanafunzi wa kidato cha pili Sekondari ya Siha, amekana kusaini nyaraka hizo na kwamba saini si yake.
Kiwanja kilichouzwa kipo barabara ya Stesheni karibu na Hoteli ya Kilimanjaro na ni miongoni mwa mali za marehemu Paul Kyauka, zilizoorodheshwa katika kesi ya mirathi iliyopo Mahakama Kuu ikisubiri kusikilizwa.
Kisheria, mtoto mdogo haruhusiwi kumiliki ardhi wala kusaini hati zozote, lakini katika sakata hilo mtoto huyo anadaiwa aliwahi kufungua kesi ya mirathi ya babu yake na kuteuliwa kuwa msimamizi japo anakana kufungua kesi.
Kwa upande wake, wakili Jonathan alipohojiwa na waandishi wa habari, alikiri kuandaa nyaraka hizo na kusema asingeweza kufahamu kama kulikuwa na matatizo kwa kuwa alifuata taratibu zote za uwakili.