MBUNGE wa Tandahimba, Juma Njwayo (CCM), jana aliliambia Bunge kuwa, wakazi wa Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara wanalazimika kusafiri masafa marefu kwenda Newala kufuata huduma za mtandao, EMS na fax kutokana na wilaya hiyo kutokuwa na ofisi za Shirika la Posta.
Alitoa taarifa hizo jana wakati akiuliza swali la nyongeza na kubainisha kuwa, huo umekuwa ni usumbufu mkubwa kwa wakazi wa wilaya hiyo, na kuiomba serikali kuangalia namna ya kulimaliza tatizo hilo.
Aliitaka serikali kuwaeleza wananchi wa wilaya hiyo ni lini Shirika la Posta litajenga ofisi yake ya kudumu wilayani humo, kwani hivi sasa inatumia kontena kama ofisi.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Dk. Maua Daftari, alisema ni kweli kuwa mji wa Tandahimba, ambao ni makao makuu ya Wilaya ya Tandahimba, hauna jengo rasmi kwa ajili ya huduma za Posta na badala yake kontena hutumika kwa madhumuni hayo.
Alisema hali kama hiyo ipo pia katika wilaya nyingine nchini, hasa zile mpya, kutokana na hali mbaya ya kifedha inayolikabili Shirika la Posta.
Hata hivyo, alisema baada ya serikali kufanya maamuzi yanayolenga kuliweka Shirika la Posta katika hali nzuri kifedha, shirika hilo litaanza kutekeleza mikakati yake ya kibishara ikiwa ni pamoja na kujenga majengo katika makao makuu ya wilaya.
Kutokana na mkakati huo, alisema Wilaya ya Tandahimba itajumuishwa na hadi hivi sasa tayari shirika hilo limeshakodi nyumba wilayani Tandahimba itakayotumika kama ofisi ya Posta baada ya matengenezo.