UONGOZI wa klabu ya soka ya Malindi ya visiwani hapa, imeupongeza uongozi wa mabingwa wa soka Zanzibar, Miembeni, kuwezesha mashabiki kuingia bure katika mechi yake dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini itakayopigwa leo usiku katika Uwanja wa Amaan.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Malindi, Jaffar Hussein Babu, kitendo hicho kilichofanywa na Mkurugenzi wa Miembeni, Amani Makungu kuinunua mechi hiyo kimevunja rekodi.
Babu alisema kwa mazingira hayo, Malindi leo itaungana na Wazanzibar wote kuishangilia Miembeni, na kwamba wameandaa mabasi maalumu kwa ajili ya kuwapeleka mashabiki uwanjani kushuhudia mechi hiyo itakayoanza saa 2:00 usiku.
“Kitendo cha Makungu kununua mechi kimevunja rekodi, kwani mwaka 1995 Malindi ilipocheza na Etoile du Sahel ya Tunisia, tuliingiza sh mil 19.6 kiasi ambacho kingeweza kuvunwa na Miembeni kesho (leo), lakini sasa mashabiki wataingia bure, ni jambo la kujivunia,” alisema Babu.
Alisema, licha ya upinzani wa jadi na Miembeni, lakini inapofika suala la mechi za kimataifa, hawana budi kuwa pamoja kwa sababu za utaifa kwani, uzalendo unapaswa kuwekwa mbele kwanza, upinzani wa jadi baadaye.
Akizungumzia mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha wa Miembeni, Mahamoud Suleiman Jabri, alisema kambi waliyoweka ya siku kumi huko Nungwi, vijana wake wako fiti kuiangamiza Mamelodi katika mechi ya leo kabla ya kupigwa kwa mechi ya marudiano wiki mbili baadaye.
Naye Mkurugenzi wa Miembeni, Amani Makungu alisema, timu yake lazima iibuke na ushindi, kwa sababu imejiandaa vema, huku ikitarajia kupata sapoti kubwa kutoka kwa wapenzi na mashabiki watakaoingia uwanjani bila kulipa kiingilio.
Wakati Miembeni ikishuka dimbani leo, wawakilishi wengine wa Zanzibar katika Kombe la Shirikisho, Chipukizi ya Pemba, nayo itashuka kwenye dimba la Gombani kisiwani humo kuwakaribisha Green Buffaloes ya Zambia.
Aidha, katika mechi ya Miembeni na Mamelodi, mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Haroun Ali Suleiman na katika mechi baina ya Chipukizi na Buffaloes, ni Naibu Waziri Kiongozi na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Ali Juma Shamuhuna.