logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
ijumaa, 15 Februari 2008
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1


Kama kumuenzi St. Valentine ndiko huku, bora tuache tu!
 
Khadija Kalili


HAPPY Valentine’s Day wapendwa popote pale mlipo.

Imekuwa ni jambo la kawaida kila ifikapo Februari 14 ambako kila mtu huhangaika kwa kumtafutia mwenza wake zawadi ambayo hakika kila atakapoitazama itampa raha fulani.

Habari haiishii hapo, kuna baadhi ya watu ambao huhaha wiki moja kabla ya maadhimisho hayo kwa kuiandaa siku hiyo tofauti na siku nyingine za kawaida.

Kwa upande wa burudani, nako mambo huandaliwa kivingine, kama ni ukumbi basi utakuta umepambwa na maua mekundu, muziki laini yaani ule wa taratibu, huku wenza wakiwa katika hali ya utulivu wa pekee.

Hapo sasa binafsi huwa nashindwa kufahamu hivi watu hawa kwa nini wasionyeshane upendo na huba zenye tashtiti kama inavyokuwa katika sikukuu hii ya Mtakatifu Valentino, Valentines Day.

Nilichogundua mimi ni kwamba, watu wengi ambao wameikurupukia sikukuu hii hawaelewi maana halisi wala chimbuko lake.

Historia inasema kwamba awali kulikuwa na jamaa aliyefahamika kwa jina la Valentine, ambaye alipingana na sheria zilizokuwepo za Kanisa la Katoliki lililowapiga marufuku vijana kufunga ndoa kwa madai kwamba ndiyo walikuwa wapiganaji katika vita hivyo ikatungwa sheria ya kuwazuia viongozi wa dini kuwafungisha ndoa.

Wapo vijana waliokwenda vitani, lakini wapo ambao hawakupenda sheria hiyo, hivyo Valentine kutokana na huruma yake, aliamua kujivika jukumu la kuwafungisha ndoa kwa siri vijana ambao walikuwa wakihitaji, kitendo kilichowafanya vijana wengi kumpenda.

Hivyo basi, alipogundulika kama anakwenda kinyume cha sheria ya kanisa, alikamatwa akafungwa gerezani, ambako hata hivyo vijana wengi walikuwa wakimiminika kwenda kumtembelea wakiwa na maua mekundu ‘Red Rose’ kama ishara ya mapenzi.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, Valentine alifariki Februari 14, ambayo sisi tunaona kwamba ni bonge la pati hivyo kwa kumpa heshima ndipo Waroma wakamtangaza kuwa mtakatifu na siku hiyo kujizolea umaarufu duniani kote.

Katika hali nyingine, wapo baadhi ya watu wanaosema kwamba siku ya Valentine ilikuwa ya kupata wachumba, ambako wanaume waliandika majina ya wasichana katika vikaratasi kisha walivirusha katika maji, zaidi walitumia mito na bahari kisha wasichana walivikimbilia na kuviokota kisha kuvifungua na jina utakalolikuta ndiyo atakuwa mume wako na hakuna aliyebisha.

Sasa basi, hadi hapo utaona kwamba kila mtu anazungumza lake, ndiyo maana wapo baadhi ya watu wanaiharibu siku hii, haipendezi.

Tuzungumze katika lugha ya wenzetu kidogo ‘Love is something which is supposed to be continued every day’, yaani mapenzi ni jambo ambalo linatakiwa liendelezwe kila siku na si kuonyeshana mapenzi kwa siku moja tu ya kumbukumbu ya Mtakatifu Valentine.

Kwa kuwakumbushia tu, unaweza kumwonyesha mwenza wako kuwa unampenda kwa njia nyingi si lazima kuzungumza, unaweza kumwonyesha kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kujenga uaminifu na kumtoa shaka kwa kila jambo ambalo yeye amekuwa hana imani juu yako.

Hivyo basi, katika kumuenzi siku hii muhimu na adimu nawakumbusha wote ambao ni wadanganyifu, wabadilike kwa kuwa endapo mwenza wako atakugundua kuwa unamdanganya mambo fulani, ni sumu katika mapenzi na utakuwa umeharibu mtu wangu.

Hivyo basi, ni wajibu kwa kila mtu kufahamu kwamba kila siku ni siku ya Valentine, ndiyo maana hata yeye wakati wa uhai wake alijitahidi kutimiza wajibu kwa kuwaaunganisha katika maisha ya ndoa pale walipohitaji awasaidie.

Kuvaa nguo nyekundu na kushika maua, kununua kadi hivi sasa imekuwa ni kama mtindo ulioingia mjini na kugeuzwa kuwa mradi wa msimu huku tukisahau kwamba maana halisi tunaipotosha.

Hivi ni wangapi waliosherehekea Valentine kwamba wana uhakika wa asilimia kubwa zaidi kama kweli wenza wao ni wa kweli au wanadanganyana?

Inashangaza pia pale unapoona mtu anampelekea kadi, ua na zawadi mume wa mtu, hivi hapo kweli uhusiano huo ni wa kweli ama ni kwenda na fasheni? Tuache kudanganyana, kama hatuwezi kumuenzi huyo Valentine, bora tuache.

Ikumbukwe kwamba bila mapenzi hakuna jambo lolote lile litakaloendelea duniani, nasema hilo kwa kuona kwamba watu ambao hawana amani kamwe hawawezi kuwa pamoja na kujumuika kama wengine ambao husherehekea sikukuu hii kwa dhati.

Mapenzi huleta amani, huleta watoto na kukuza familia na bila ya mapenzi hakuna maisha, hivyo tusiipotoshe siku hii na kuigeuza kuwa ya kihuni kama baadhi ya watu wanavyofanya.

Kama hakuna mapenzi kamwe hakutakuwa na maelewano ya upendo miongoni mwetu na kama watu wako katika maisha ya ndoa au uchumba na hakuna mapenzi basi ifahamike kwamba uhusiano huo hautadumu kwa sababu hakuna mtu anayemwamini mwenza wake.

Katika hatua nyingine na kwa kukumbushana litakuwa jambo jema endapo watu tutatumia siku hii kuyatazama kwa kina mapenzi kuyachambua ikiwa ni pamoja na kumsoma zaidi mpenzi wako na siyo kumpa ua kwa sababu eti umemwona rafiki yako kanunua ua na kadi, basi wewe unakurupuka na kumpa huyo unayedhani ni mwenza wa kweli.

Wapo baadhi ya watu katika jamii yetu huitumia siku hii kumaliza tofauti zao jambo ambalo ni la busara tofauti na wale ambao hulazimishana na kusababisha kufanya mambo yasiyo na maana, hasa ikizingatiwa kwamba hivi sasa ulimwengu mzima umegubikwa na kiza kinene cha ugonjwa hatari wa ukimwi.

Vilevile kwa wale wanandoa ni wakati muafaka wa kukaa pamoja kwa upendo na siyo kila mtu kumsaka mwenza mpya, hiyo haipendezi na hapo hayatakuwa mapenzi ya kweli na dhati ila utakuwa unakidhi matamanio ya roho na mwili wako tu.

Ikumbukwe kwamba enzi za uhai wa Mtakatifu Valentine vijana aliokuwa akiwafungisha ndoa kwa siri walimtembelea gerezani huku wakimweleza kwamba wanafurahia maisha ya ndoa, lakini tofauti na ilivyo sasa ndoa nyingi zimejaa migogoro hali ambayo utamkuta mtu katika ukumbi wa burudani akiwa na mwenza ambaye siyo yule aliyeapa kuwa naye kwa shida na raha kwa uzima na ugonjwa hadi kifo kitakapowatenganisha.

Tofauti na ilivyo sasa, hakuna wanandoa ambao utakaa nao na kusikia kwamba wanafurahia maisha ya ndoa, wengi wao utawasikia wakilalamika na kujutia uamuzi wa kujitia kitanzi hicho, hivi tatizo hasa ni nini na nani msaliti? Tunapaswa tujiulize.

Inashangaza kuona kwamba kijana alimchumbia mke mwenyewe akaoa kwa ridhaa yake, lakini mara anamgeuka mke wake na kuwa mwiba wenye makali zaidi ya mchongoma kwa kumfedhehesha mke wake kwa vitendo dhairi vya kiasherati, huku akibadili wanawake kama nguo kadhalika na kwa wanawake nao wapo wanaowadhalilisha waume zao, lakini hawavumi.

Kwa upande wangu, mimi naona kwamba haya madhila yote yanasababishwa na mmomonyoko wa madaili katika jamii.

Tukumbushane hapo zamani enzi za mababu zetu walichaguliwa wake wa kuoa kufuatana na mila na tamaduni, huku wakizingatia zaidi ukoo ambao mwoaji alitakiwa aoe.

Wengi walichumbia na kuoa katika ukoo ambao wazazi wa pande zote walifahamiana vilivyo, hali ambayo ilikuwa ni marufuku mtu kuingia kabila lingine ili kulinda mila na desturi za kabila husika hivyo ilikuwa nadra wenza kugombana, pia waliweza kukaa mitala kwakuwa wote walikuwa ni wamoja jambo ambalo hivi sasa ni vigumu kuwakuta wakewenza wakimudu kukaa pamoja japo kwa sekunde.

Tofauti na hivi sasa, wapenzi wengi hukutana katika kumbi za burudani, hivyo inakuwa vigumu kumtambua mtu tabia ya familia yake jambo ambalo unaweza kuvamia ukoo wenye tabia zisizofaa na mwisho wa siku ukijikuta ukiweka mikono kichwani.

Hivyo basi, lazima tukubaliane kwamba wengi waliosherehekea Valentine’s Day hawakusherehekea kwa imani ya kweli kutoka moyoni, wengi wao wameiba waume za watu na wake za watu huku wakifanya vitendo vya kiasherati, jamani hivyo sivyo na huko siyo kumuenzi kwa usahihi Mtakatifu Valentine.

Napenda kuwakumbusha wapenzi wote kukumbuka kukaa pamoja na familia zao kwa upendo na amani, ikiwa na kama bado hujajaaliwa basi kuwa muangalifu katika kuchagua yule ambaye unapenda awe mwenza wako ili kujenga familia iliyo bora.

Katika kusherehekea sikukuu ya Valentine bendi ya muziki wa dansi ya Diamond Musica International ‘Moto x3 ‘ ilizikonga nyoyo za mashabiki katika ukumbi wa Landmark Ubungo, Kundi la mirindimo ya pwani Jahazi Modern Taarab waliwarusha mashabiki vidole juu katika Ukumbi wa Mango Garden Kinondoni, Banana Zorro aliwapa raha wakazi wa Dodoma katika Ukumbi wa Royal Village, FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’ walitoa zawadi ya Valentine’s Day katika ukumbi wa Pricess Sinza na bendi ya Acudo Impact waliporomosha burudani katika Ukumbi wa Vitican City.

Nawatakia mapenzi mazuri.

Kwa maoni au ushauri piga simu 0755 707046.


h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2008 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa Mkwepu na Makunganya, jengo la Bilicanas, gorofa ya kwanza, SLP 15261, Dar es salaam, Tanzania
simu +255-22-2126233  •  faksi +255-22-2126234  •  Selula  0713 296570
ban