na Asha Bani
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimedai kubaini udanganyifu kwenye maboresho ya daftari la wapiga kura, zoezi ambalo limemalizika mwishoni mwa wiki katika Mkoa wa Ruvuma.
Hayo yamebainishwa juzi na Ofisa wa Sera wa CUF, Hussein Mmasi, alipozungumza na Tanzania Daima ofisini kwake Buguruni, Dar es Salaam.
Alisema udanganyifu huo umebainika baada ya chama hicho kupata malalamiko mbalimbali kutoka kwa baadhi ya wananchi katika vituo mbalimbali ambavyo vilitumika kuandikisha kura wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2005.
Mmasi alivitaja vituo hivyo ikiwa ni pamoja na kuainisha baadhi ya udanganyifu ambao wananchi waliuwekea wasiwasi kuwa ni pamoja na kituo cha Tarafani, Majengo na Muungano.
Alisema katika vituo hivyo kulitokea mtafaruku baada ya mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Omari katika kituo cha Muungano alikuwa akipita na kukusanya shahada za watu na kuanza kunakili namba, kitendo ambacho hakikutakiwa.
“Baada ya wananchi kubaini hivyo baadhi walimkamata na kumpeleka katika kituo kidogo cha polisi ambapo alidai baada ya muda mfupi aliachiwa,” alisema.
Alisema mbali na hilo katika kituo kilichopo Shule ya Mtina, mwandikishaji alikuwa anatumia daftari kama za wanafunzi kuhakiki na kuwa wamekamata baadhi ya vitambulisho ambavyo vilikuwa na tofauti na vile vya awali.
“Vitambulisho hivyo vilikuwa na tofauti kubwa kutokana na kuwa havina anwani, kata ya mtu alikotoka, kijiji wala mkoa,” alisema Mmasi.
Alisema tayari amezungumza na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Rajabu Kiravu, ambaye alimuahidi kufuatilia suala hilo.
Akizungumza na Tanzania Daima kuhusu hilo, Kiravu alikiri kupata malalamiko hayo, lakini alipoyafanyia kazi alibaini kuwa hayakuwa na ukweli.