ijumaa, 15 Februari 2008

Soka la Bongo Filamu iliyoibua vipaji vya wanasoka nje ya soka

na Khadija Kalili


‘SOKA la Bongo’ ni filamu mpya ambayo imeonyesha umahiri wa wacheza soka wa Tanzania katika medani ya uigizaji.

Bila shaka, ujio wa filamu hii utawafumbua macho watu wengi hasa wapenzi wa michezo na burudani, kwamba hata wacheza soka nao wanaweza kuigiza kama watapewa nafasi.

Katika filamu hii, wanasoka wameonyesha namna wanavyoweza kufanya kazi nyingine nje ya uwanja wa soka na kudhirisha kuwa kama wakiwezeshwa wanaweza kufanya mambo makubwa zaidi.

Pia ni jambo la kufurahisha kuona kwamba, waandaaji ambao ni Tamba Arts Group kwa kushirikiana na Sultan Tamba, wameweza kuwakutanisha mahasimu wawili Juma Kaseja ‘Tanzania One’ wa klabu ya Simba na Athumani Idd ‘Chuji’ wa Yanga, ambao wameweza kucheza filamu hii kwa ufanisi mkubwa bila kujali tofauti zao.

Katika filamu hii, wanasoka wote wameonekana kwamba wana vipaji katika uigizaji, lakini vimekosa mvumbuzi na kuendelezwa.

Hivyo basi, wakati umefika wa kuwa wabunifu zaidi na kuacha kutunga filamu ambazo zimekosa ubunifu na kung’ang’ania kuiga kazi za wengine.

Hebu angalia ubunifu huu wa wachezaji, ambao watu hufurika katika viwanja mbalimbali wanapokuwa wakicheza kwenda kuwashangilia kwamba wanaweza kuigiza na kukupa hamasa wewe mtazamaji.

Katika filamu hii utaweza kumwona Selemani Matola ambaye ameigiza kama mwanasoka ambaye ni mlevi na aliyebobea katika mapenzi na wanawake, huku wakati mwingine akifumaniwa, jambo ambalo linaonyesha athari mbaya kwa mtoto mdogo ambaye alimshuhudia akifanya mambo hayo na kuiga tabia hiyo chafu.

Pia yupo golikipa mahiri wa timu ya soka ya Yanga, Ivo Mapunda, ambaye anakumbana na matatizo ya kuzuiwa na mkewe kujiunga na wachezaji wenzake kambini kutokana na uelewa mdogo wa mkewe, akidhani kuwa, akienda huko atapata mwanamke mwingine na kujihusisha na vitendo vya kihuni.

Hapo ndipo kwenye neno, hivi nani asiyetambua kwamba wachezaji wote wa soka wanaonekana kwamba ni wahuni na wasiojali maisha yao na familia zao?

Si hayo tu, pia filamu hiyo imegusia masuala ya ushirikina, ambako ni tatizo kubwa katika soka la hapa nchini na hata Afrika kwa ujumla.

Imekuwa jambo la kawaida pale mchezaji anapopatwa na tatizo la kuumwa mguu au goti kujaa maji, lazima utasikia watu wakisema karogwa na fulani ili soka lake lisiendelee.

Mbali na wacheza soka, filamu hii pia imemuibua tena mwigizaji maarufu wa filamu na michezo ya kuigiza, Jacob Stephen ‘JB’, ambaye ni mmoja wa wachezaji, akicheza kama mshauri wa timu.

Katika mahojiano na Tanzania Daima, JB anasema kuwa, hajawahi kuwa mchezaji wa soka, lakini anashukuru kwa kuweza kuimudu vema nafasi aliyopewa kuicheza.

JB alisema mbali ya yeye kuonyesha kipaji, pia amefurahishwa kuona wanasoka wakicheza kwa ufanisi katika filamu hiyo, hivyo amewataka watu wanaofanya kazi mbalimbali kujiingiza katika fani hiyo ya kuigiza.

Akizungumza na Tanzania Daima hivi karibuni, mwandaaji wa filamu hiyo, ambayo itazinduliwa hivi karibuni, Dk. Abdallah Maneno Tamba, alisema kuwa ‘Soka la Bongo’ imebeba maudhui ya aina nyingi ambayo ni mambo yanayoendelea katika maisha ya kila siku ya Mtanzania.

Alisema kwamba ni faraja kubwa kwa mtu kupata nakala yake ili apate kile kilicho muhimu kwa maisha ya kila siku.

“Kwa vile tayari imekwishaingia sokoni ikiwa katika VHS, huu ndiyo wakati muafaka kwa mashabiki wa filamu nchini kushuhudia kila kitu,” alisema Tamba.

Alisema kwamba mara baada ya kuitoa katika VHS, baadaye filamu hiyo itatolewa katika CD na DVD.