JUMLA ya wanafunzi 3,079 katika shule za msingi na sekondari nchini wameshindwa kumaliza masomo yao baada ya kutiwa mimba kati ya mwaka 2006 na 2007.
Takwimu hizo zilitolewa na Mkurugenzi Msaidizi, Ofisi ya Ofisa Elimu Kiongozi (Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi), Mary Machuve, wakati wa mjadala wa kupata maoni ya wadau wa elimu kanda ya kaskazini magharibi.
Machuve aliitaja mikoa inayoongoza kwa wanafunzi kutiwa mimba kuwa ni Tabora, Lindi, Mtwara, Singida, Morogoro na Ruvuma.
Alisema katika shule za msingi wanafunzi waliokatizwa masomo yao kwa sababu ya mimba ni 1,509 na wale wa sekondari ni 1,570.
Alisema kati ya mwaka 2002 na mwaka 2006, wanafunzi wa shule za msingi waliopata mimba walikuwa 14,036 na wa sekondari waliokuwa 4,113, jambo linaloonyesha kuwa tatizo hilo bado ni kubwa linalohitaji ufumbuzi wa haraka.
Macheve alisema kutokana na tatizo hilo, wizara husika imefanya utafiti katika nchi za Malawi, Zambia na Zimbabwe na kuona kinachofanywa na nchi hizo ili kuepuka mimba za wanafunzi na kukatishwa masomo.
Aidha, alisema msichana kufukuzwa shule baada ya kutiwa mimba si suluhisho la matatizo hayo kwa kuwa baadhi yao hupata mimba kwa kukusudia na wengine hubakwa.