KUNDI la taarab la Jahazi Modern, limekanusha uvumi ulioenea kwa kasi katika baadhi ya mitaa ya Jiji la Dar es Salaam, kuwa wana mpango wa kumnyakua Jokha Kassim wa Zanzibar Stars.
Mkurugenzi wa kundi hilo linalotumia mtindo wa ‘Nakshi Nakshi’, Mzee Yussuf ‘Mfalme’, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa, habari hizo hazina ukweli wowote na kuwataka mashabiki wao kutotilia maanani.
“Naomba wapenzi na mashabiki wetu wote walioathirika na uzushi huo kupuuza taarifa hizo na naeleza bayana kuwa, sisi kama Jahazi, katakata hatumwitaji Jokha,” alisema Yussuf aliye mpapasa kinanda mahiri kwa upande wa taarab hapa nchini.
Yusssuf alisema kuwa, anaamini waimbaji alionao ndani ya kundi lake wanatosha, hivyo hakuna sababu ya msingi ya kumuongeza mwimbaji huyo licha ya uwezo wake wa kufanya kazi.
Uvumi wa kwamba Jahazi wana mpango wa kumchukua Jokha umezuka baada ya kuonekana mara kwa mara katika maonyesho ya Jahazi, ambako huingia na kuanza kucheza kwa ushabiki sambamba na kutunza baadhi ya waimbaji.