logo spc.r_ad0
sp.b_ad0
blu.strip
spc.bt_blu.strip
HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
sp.b_menu
ban
sp.b_ban
jumamosi, 16 Februari 2008
Pekua Tovuti
sp.t_sech.box sp.tafuta_w_tuma sp.t_tuma sp.r_tuma
sp.b_box sp.b_tuma
sp.b_F1
h.sep1
sp.r_men
sp.t
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari
sp.b_tuma
sp.l_men
h.sep1


Waislamu, tatizo si Bush
 
Salehe Mohamed


‘BANIANI mbaya kiatu chake dawa na mtumikie kafiri upate mradi wako ni misemo ya Kiswahili ambayo kwa namna moja au nyingine inamhamasisha mtu kufanya kazi bila kuangalia kasoro za majiri wake.

Kwa maneno rahisi ni afadhali ukafanya kazi kwa mtu usiyempenda au kuelewana naye ilimradi maisha yako yanakwenda vizuri, kuliko kukaa nyumbani au vijiweni bila ya kuwa na kazi.

Misemo hii imerithiwa tangu enzi na enzi na ina mantiki makubwa kwa watu wenye nia ya kufanya kazi kwa bidii na wenye kiu na maendeleo ya familia zao na taifa lao kwa ujumla.

Linapofika suala la kazi au kutaka msaada wa maendeleo, mtu hapaswi kuweka mbele tofauti zake na anayempatia msaada, kwani akifanya hivyo kuna kila dalili za kukosa msaada husika na atakayepata hasara zaidi ni yule aliyekuwa akitarajia kupata msaada.

Marekani ni miongoni mwa mataifa machache makubwa yenye kujiweza kiuchumi na inaaminika kuwa ni taifa linalopenda kuingilia mambo ya mataifa mengine, bila ridhaa ya taifa husika au umoja wa mataifa.

Miongoni mwa mambo ambayo hadi hivi sasa yanalaumiwa na jumuiya mbalimbali ni kitendo cha kujiingiza katika vita ya Iraq bila baraka za Umoja wa Mataifa.

Kutokana na vitendo vyake hivyo hasa kwa mataifa ya Kiislamu, baadhi ya Waislamu wanatafsiri kuwa taifa hilo halitaki kuona Uislamu unaendelea.

Matokeo ya sera za nje za Marekani yamechangia zaidi raia wa nchi hiyo kutokuwa na amani wapokuwa katika mataifa mengine, kiasi cha kushambuliwa mara kwa mara na kupoteza maisha yao.

Maadui wa Marekani hivi sasa wapo kila kona na kila kukicha kuna taarifa za kukamatwa kwa kundi fulani kwa kufanya uhalifu dhidi ya raia wa Marekani, kiufupi hali si shwari kwa raia wa Marekani.

Kesho Rais wa Marekani George Bush anatarajia kuanza ziara ya siku nne hapa nchini ziara iliyoelezewa kuwa ni kwa ajili ya kusaidia Tanzania kifedha, ili kufikia malengo ya melinia, kupambana na ukimwi na malaria.

Ziara hiyo imeanza kupata wakati mgumu baada ya jumuiya mbalimbali za Kiislamu kujitokeza na kudai zitafanya maandamano kuipinga, kwa madai Rais Bush amekuwa kinara wa kuua Waislamu katika nchi zenye mrengo wa dini hiyo.

Kumekuwa na mivutano ya kutofautiana katika jumuiya hizo ilimradi kila mtu anasimamia upande wake na kutoa hisia zake bila kutathmini kwa umakini ni kwa kiwango gani Tanzania itanufaika na ziara hiyo.

Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Issa bin Shaaban Simba, alisema Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) kama msemaji mkuu wa Waislamu wanaunga mkono ziara hiyo, kwani itakuwa na manufaa zaidi kwa Watanzania na ni ya kiserikali, hivyo si vema watu wakichanganya na dini.

Kimsingi maneno ya Mufti Simba yana mantiki ndani yake, kwani huu si muda wa kuanza kuangalia matatizo yanayosababishwa na Marekani katika nchi nyingine, bali kuangalia matatizo ya Tanzania.

Ukweli siku zote unauma, lakini ni lazima usemwe ili kama kuna mkosaji aweze kujisahihisha kwa lengo la kuleta ufanisi ndani na nje ya dini hiyo au sekta husika.

Waislamu hapa nchini wana matatizo mengi tu ambayo wao hawajaweza kukaa na kuyatafutia ufumbuzi kwa lengo la kuendeleza dini yao na maendeleo kwa ujumla.

Migogoro ya kugombea madaraka kila kukicha haishi. Mara leo msikiti huu mara kesho msikiti ule ilimradi watu wanaoanzisha migogoro hiyo wapate kile wanachohitaji.

Migogoro hiyo kwa kiasi kikubwa imewarudisha nyuma sana kimaendeleo Waislamu hasa katika suala zima la elimu dunia ambayo ndiyo ufunguo wa maisha.

Hivi sasa unapoamua kutafuta shule na vyuo vya Kiislamu hapa nchini ni vichache sana kulinganisha na madhehebu mengine ambayo kila kukicha shule au vyuo vyao vinasikika kwa kutoa matokeo mazuri katika mitihani.

Hata shule za Kiislamu zilizopo hazina walimu wazuri, kwani hata maslahi yao ni duni hivyo walimu wazuri huamua kuzikimbia na kwenda kufundisha kule kwenye maslahi manono.

Tatizo la Waislamu hapa si Bush, bali ni wao wenyewe kushindwa kujipanga vema, ili kufikia malengo waliyojiwekea ili kuleta tija na ufanisi katika familia zao na taifa kwa ujumla.

Ni aibu leo hii kumpeleka mgeni katika makao makuu ya Bakwata na kuanza kumtambulisha kuwa hizo ndizo ofisi za baraza hilo, ambalo ndiyo chombo kikuu cha kusimamia mambo ya Kiislamu.

Shule, msikiti na majengo mengine ya Bakwata hayapendezi hata kidogo machoni mwa watu, lakini hilo wahusika hawalioni. Wao wanafikiria kubeba mabango siku ya ujio wa Bush.

La watoto yatima kukosa ada za kuwasomesha kwa sababu ya kukosekana mfuko maalumu wa kuwasidia, halionekani bali hili la Bush ambaye anakuja kutembea hapa kwa siku nne ndilo linaonekana na rahisi kulitekeleza.

Hao wanaopinga ziara hiyo kwa nguvu hiyo hiyo wangeanzisha harambee angalau kila mtu atoe sh 500 kwa ajili ya ujenzi wa shule za Kiislamu au kuwasaidia yatima, ingekuwa bora zaidi kuliko walichokifikiria.

Ni kitegauchumi gani ambacho watu hao wamekianzisha na leo hii unaweza kusema hiki kilitokana na nguvu za jumuiya fulani ya Kiislamu ambayo iliguswa na matatizo ya wananchi.

Kitabu cha Qur’an hakitaki mtu mwongo, mnafiki au watu kugombania madaraka misikitini, kisa kutaka maslahi binafsi au sifa ya kukalia uongozi.

Leo hii hapa Tanzania ugonjwa wa malaria ndiyo unaoongoza kwa kusababisha vifo vingi vya watoto wachanga na watu wazima kila kukicha na serikali imekuwa ikijitadi kupambana na ugonjwa huo kwa kadri iwezavyo, lakini tatizo kubwa ni uwezo mdogo wa kifedha.

Ugonjwa wa ukimwi kila siku unazidi kumaliza watu na hauangalii huu ni Mwislamu au Mkristo. Ukimwi leo hii msaada kwa ajili ya kupambana nao unakuja watu wanaanza kuuwekea vikwazo.

Katika nchi hii kuna watu wanapata mlo mmoja kwa siku kwa sababu ya ugumu wa maisha, msaada unakuja watu wanatanguliza siasa za nje zisizo na maslahi kwa taifa na watu wake.

Maji, nishati ni tatizo kubwa sana hapa Tanzania kwani ni asilimia kubwa ya Watanzania hawapati huduma hizo sababu kubwa ikiwa ni uwezo mdogo wa serikali katika kutoa huduma hizo.

Miongoni mwa maeneo ambayo Rais Bush anatarajia kuja kuidhinisha fedha ni maji na nishati, hivyo ni vema Watanzania wakawa watulivu katika ziara hii ili wanufaike.

Kimsingi yapo mambo mengi ambayo wahusika kama watafuatilia kwa makini, wanaweza wakawa na jibu sahihi na sababu kamili za kufanya au kutokufanya maandamano ya kupinga ujio wa Bush.

Mambo ya kutumiwa na watu kufanya mambo yalishapitwa na wakati na kamwe hayawezi kuikwamua nchi katika lindi la umaskini ambao unazidi kuongezeka siku hadi siku.

Rais Bush na taifa lake la Marekani wana madhambi mengi wanayoyafanya, na Tanzania ikiwa kama nchi inayojali ubinadamu, lazima ikemee hali hiyo kwa umakini na uangalifu wa hali ya juu ili isije kujiingiza katika matatizo yatakayoiathiri yenyewe.

Ni fedheha kwa taifa changa kama la Tanzania linalotafuta nafasi ya kuonekana na kusaidia kimataifa kuanza kuwa na sifa mbaya ya kuwazomea au kuwapokea kwa maandamano viongozi wa kimataifa.

Matatizo ya Tanzania au Waislamu hayakusababishwa na Bush au nchi yake, bali yalisababishwa na Watanzania wenyewe, hivyo ni vema yakatatuliwa na wenyewe bila kuwashirikisha watu wengine.

Mwisho, ni busara kwa Waislamu wakakaa pamoja na kuangalia walipojikwaa, ili waweze kurekebisha hali waliyonayo bila ya kufanya shinikizo kwa watu wasiohusika na hali waliyonayo.


h.sep
juu sp.b
Habari Mpya  |  Kitaifa  |  Dar  |  Mikoani  |  Tahariri  |  Makala  |  Michezo  |  Matangazo  |  Webmaster
Copyright 2008 © FreeMedia Ltd.
Free media limited
mtaa wa Mkwepu na Makunganya, jengo la Bilicanas, gorofa ya kwanza, SLP 15261, Dar es salaam, Tanzania
simu +255-22-2126233  •  faksi +255-22-2126234  •  Selula  0713 296570