na TAHARIRI
RAIS wa Marekani, George Bush na mkewe Laura Bush pamoja na ujumbe wake, leo wanatarajiwa kuwasili kwa ziara ya siku nne nchini. Hii ni mara ya kwanza kwa rais huyo kuwasili nchini.
Ziara ya kiongozi huyo ni heshima kubwa kwa nchi yetu, kwani hiyo itakuwa ni mara ya pili kutembelewa na kiongozi wa taifa hilo kubwa duniani kwa ziara ya kitaifa. Mwaka 2000, Rais Bill Clinton alifanya ziara ya kikazi nchini.
Pamoja na kutembelea Tanzania, Bush pia atatembelea nchi nyinginie, ili kuangalia maendeleo ya wananchi wa nchi hizo pamoja na kuhamasisha mapambano dhidi ya ukimwi na malaria.
Ingawa ziara ya kiongozi huyo imezusha minong’ono miongoni mwa wanajamii kuhusu imani za kidini, lakini lengo la ziara hiyo si kuhamasisha masuala ya dini, bali ni kwa maendeleo ya nchi yetu.
Ni ukweli usiopingika kuwa, nchi yetu inakabiliwa na matatizo mbalimbali na kwa kiasi kikubwa, tunahitaji misaada kutoka maeneo mbalimbali kwa lengo la kuboresha hali zetu kiuchumi.
Akiwa nchini, Rais Bush atafanya ziara katika maeneo mbalimbali na kukagua shughuli za kimaendeleo zilizotekelezwa kwa msaada wa Mpango wa MCC.
Sambamba na kutembelea maeneo hayo, Rais Bush atasaini mkataba wa dola milioni 698 kwa ajili ya shughuli za maendeleo nchini, hasa katika sekta za afya na miundombinu.
Hiyo ni faraja kwa nchi yetu, ikiwa fedha hizo zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, kwani zitaweza kuleta mafanikio katika sekta hizo ambazo ni muhimu kwa maisha ya binadamu.
Kutokana na hali hiyo, ziara ya kiongozi huyo inapaswa kuungwa mkono na wananchi wote, hivyo shime wananchi tujitokeze kumlaki mgeni wetu na kumwonyesha ukarimu wakati wote atakapokuwapo nchini, ili naye atakaporejea kwao atukumbuke kwa ukarimu tuliompatia.
Pamoja na yote hayo, tunaamini ziara ya kiongozi huyo itakuwa na manufaa kwa nchi yetu na kwa kiasi kikubwa itasaidia kupunguza matatizo katika sekta hizo ambazo zimekuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi.
Pia tunaamini ziara hiyo kwa kiasi kikubwa itaongeza sekta ya utalii nchini, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa.
Rais Bush anakuja na kundi kubwa la waandishi wa habari wasiopungua 100 ambao hata kama baadhi yao wataandika mambo mabaya yaliyoyakuta nchini, bado watakuwepo wachache watakaoandika habari za utajiri wa maliasili ambao tumejaaliwa, hivyo kwa namna moja ama nyingine, watakuwa wakitangaza utalii uliopo nchini.
Baada ya ziara ya Bush, tunaamini itavutia Wamarekani wengi kuja kutembelea Tanzania, huku wananchi wa Kenya wakilaani vurugu za kisiasa zinazoendelea kwao kwa kukosa heshima ya kutembelewa na kiongozi huyo.
Wakenya watalaani kutokana na kutambua kwamba, Tanzania kwa kiasi kikubwa itanufaika na ziara ya Bush. Hivyo ziara hiyo, ni nafasi ya wazi ya kuitangaza nchi yetu kwa mataifa mengine kwa lengo la kuvutia watalii.