na Safina Tibanyendela
NYUMBA 33 zimeezuliwa mapaa kutokana na mvua iliyonyesha juzi katika Kata ya Kizinga Mbagala, Dar es Salaam.
Akizungumza na Tanzania Daima juzi, mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Ernest Nyambo, alisema mvua hiyo iliyoanza kunyesha saa 9 alasiri na kuendelea hadi saa 9.45 usiku, huku ikiandamana na upepo mkali iliezua mapaa ya nyumba hizo.
“Hatujaelewa kama ni kimbunga au ni nini…mvua ilikuwa ni kubwa mno na mara ukaja upepo mkali ulioezua mapaa ya nyumba na watu kulazimika kujihifadhi katika nyumba za jirani zao zilizosalimika,” alisema na kuongeza kuwa hakuna mtu aliyejeruhiwa.
Ofisa Mtendaji wa kata hiyo ameorodhesha majina ya watu wote walioathirika ili waweze kusaidiwa na kujua thamani yake.
Nyambo alisema pia kuwa mvua hiyo iliangusha ukuta wa kiwanda cha kutengeneza kanga cha Karibu Textile Mill uliojengwa hivi karibuni na kusababisha maji machafu kutoka kiwandani hapo kutiririkia katika makazi ya watu.
Hivyo, ameiomba serikali kuwasaidia ili waweze kuezeka nyumba zao, kwani wengi wao kipato chao ni duni.