alhamis, 27 Machi 2008

Prof. Tibaijuka kukimbiza Mwenge wa Olimpiki Dar

na Dina Zubeiry


MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN Habitat), Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka, ni miongoni mwa watu sita mashuhuri barani Afrika walioteuliwa kukimbiza Mwenge wa Olimpiki utakaokimbizwa jijini Dar es Salaam, Aprili 13, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Hoteli ya Holiday Inn jijini Dar es Salaam jana, Meneja Masoko Mwandamizi wa Coca Cola, Caroline Mbaga alisema, lengo la kuwateua watu hao ni kutokana na mchango wao katika kuisadia jamii, kwa namna moja ama nyingine, hasa suala la utunzaji mazingira.

Mbaga alisema, wateule hao, pia matendo yao yanaonyesha kujitoa kwa dhana nzima ya michezo ya Olimpiki na kwa maendeleo ya jamii yenye utulivu.

Mbali na Prof. Tibaijuka ambaye ni Mtanzania, wengine ni Prof. Wangari Muta Maathai wa Kenya, ambaye ni mshindi wa tuzo ya Nobel na Kepchoge Keino pia kutoka Kenya, ambaye ni mwanariadha aliyeshinda medali mbili za dhahabu mwaka 1968 na 1972, pia mshindi wa medali mbili za shaba 1968 na 1972 katika michezo ya Olimpiki.

Pia yumo Pierre Kakule Vwirasihikya kutoka Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), ambaye ni mwanamazingira, Dorcus Inzikuru wa Uganda ambaye ni mwanariadha na Nathan Kalumbu raia wa Zimbabwe ambaye ni Rais wa Coca Cola Afrika Mashariki na Kati.

Coca Cola pia itaratibu mbio za kilometa 5 na zile za Nusu Marathon zitakazofanyika Aprili 6, ambako mshindi wa kwanza hadi wa kumi watazawadiwa zawadi za fedha taslimu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Meja mstaafu Filbert Bayi, alisema mwenge huo utakimbizwa kwa kupokezana na wakimbizaji 80, ambako kila mtu atakimbiza kilometa 5, huku kati yao pia wakiwamo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano, Muhammed Seif Khatib na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Nkaya Bendera.

Dar es Salaam ni jiji pekee lililoteuliwa kukimbizwa mwenge huo katika bara la Afrika, ambako mbio hizo ni maalumu kwa ajili kukaribisha tamasha la michezo ya Olimpiki mwaka huu huko Beijing, China ambayo inatarajiwa kuanza Agosti 8.