HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
alhamis, 27 Machi 2008
Pekua Tovuti
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari


Serikali itazame vyombo binafsi vya habari



JANA, Rais Jakaya Kikwete, alizindua Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC). Shirika hilo limeunganisha vilivyokuwa vituo vya utangazaji vya Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na Televisheni ya Taifa (TvT).

Bila shaka uamuzi huo wa kuviunganisha vituo hivyo umelenga kuboresha huduma na kuongeza ufanisi katika upatikanaji wa habari nchini.

Tunaamini serikali imechukua uamuzi huo kwa kutambua ukweli kwamba ndicho chombo pekee chenye wajibu wa kikatiba wa kuwapatia habari Watanzania kwa kodi zao zinazotumika katika uendeshaji wa vyombo hivyo.

Tunaipongeza serikali kwa hatua iliyofikia ya kuviunganisha vyombo vyake kwa nia ya kuboresha huduma zaidi. Ikumbukwe kuwa habari ni muhimu kwa maendeleo ya binadamu, hakuna jamii inayoweza kuendelea bila kupashwa habari.

Ni imani yetu kuwa baada ya kuzinduliwa kwa shirika hilo, changamoto iliyopo ni kuhakikisha kuwa Watanzania wanafaidika na huduma za shirika hilo popote pale walipo.

Tunasema hivyo kwa sababu hapo awali kulikuwa na malalamiko kutoka sehemu mbalimbali kuwa matangazo ya iliyokuwa RTD na TvT, hayakuwafikia walengwa wengi na baadhi yao waliyapata kwa kiwango kisichokubalika.

Changamoto nyingine inayoikabili serikali ni kuwawezesha wamiliki wa vyombo binafsi vya habari kupanua huduma za kuwahabarisha Watanzania, kwa kuwawekea nafuu ya kodi mbalimbali na kuwapatia matangazo ili wamudu gharama za uzalishaji, kuwalipa wafanyakazi wao na kutoa habari kwa ufanisi.

Chombo hicho kitumike kwa usahihi katika kuburudisha, kufundisha na kuadilisha jamii pasipo upendeleo wowote, tunasema hivyo kwa kuwa mara nyingine inaweza kuonekana kama chombo cha serikali kinatumika kuficha maovu serikalini.

Kama ilivyo kwa vyombo binafsi vya habari, kuzungumzia ufisadi wowote bila woga, tunalitaka shirika hilo kufanya hivyo pale kiongozi anapokosea, bila kuficha, kwa kuwa ni kiongozi.

Tunasema hivyo kutokana na ubaguzi uliokuwapo, kuhusu itikadi za kisiasa kwa idara nyingi serikalini na mashirika mbalimbali kutoa habari za upendeleo na kuvinyima habari vyombo vingine vinavyoeleza bayana maovu ya viongozi.

Pamoja na kuwapo kwa shirika hilo, tunaiomba serikali iangalie upande mwingine wa shilingi, kwa vyombo vya habari binafsi, kwa kutoa habari zote zihusuzo jamii, siasa au biashara kwa manufaa ya taifa.

Hata kwa upande wa safari za viongozi mbalimbali serikalini, wachukuliwe pia waandishi wa habari kutoka vyombo binafsi kwa ajili ya masilahi ya taifa.

Hili ni muhimu, kwa kuwa mara nyingi tunashuhudia wizara mbalimbali zikichukua waandishi kutoka vyombo vya serikali na magazeti ya chama.

Kama wizara na idara za serikali zitabadilika na kugeukia vyombo binafsi na kutoa ushirikiano stahiki, tunaamini kuwa Watanzania watanufaika na habari zinazotolewa kupitia vyombo binafsi.


juu

Warning: mysql_connect() [function.mysql-connect]: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2) in /hermes/bosweb/web098/b983/glo.freemanm2/include/comment.php on line 9
I cannot connect to the database because: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2)