MWANARIADHA maarufu wa Kenya, Paul Kibii Tergat, aliwasili nchini jana akiambatana na meneja wake Samson Chebo kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vijana wa Tanzania watakaokimbia mbio za nusu marathoni zilizo chini ya udhamini wa Kampuni ya Coca Cola.
Tergat, miongoni mwa wakimbiaji mahiri wa Kenya, alitamba vilivyo hata kuweka rekodi ya dunia mwaka 2003 na 2007, akitumia dakika 2:04:55, sambamba na kushinda mataji mbalimbali ya kimataifa.
Akizungumza baada ya kuwasili nchini jana, Tergat alisema, amefurahishwa kuja Tanzania kwa shughuli za kimichezo.
“Nimefurahi sana kuja Tanzania nchi yenye watu wakarimu kutoa mafunzo. Nilipoambiwa nije Tanzania kutoa mafunzo, sikusita kwani ni kitu ambacho nilikuwa nakitamani,” alisema.
Rekodi yake ya hivi karibu katika riadha, ni ushindi wake Novemba 2005, alipovunja rekodi ya mjini New York, Marekani iliyowekwa mwaka 2003.
Aidha, Tergat ameweka rekodi ya dunia katika mbio ndefu alipokimbia kwa dakika 2:04:55 katika mashindano yaliyofanyika Berlin, Ujerumani.
Mafanikio mengine kwa mwanariadha huyo ni ushindi wake mfululizo wa mara tano wa mbio zilizokuwa zimeandaliwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa kuanzia mwaka 1995 hadi 1999.
Januari mwaka 2004, Tergat aliteuliwa na Shirika la Chakula la Kimataifa (FAO), kuwa balozi wake wa vita dhidi ya njaa na mwaka 2005 alianzisha taasisi yake ikiwa na madhumuni ya kuwasaidia wanamichezo wenye shida barani Afrika.
Mbio hizo za nusu marathoni za kilomita 21, zitakuwa wazi kwa watu wote, ambapo pia zitakuwapo mbio za kilomita tano ambazo zitakuwa maalum kwa wasio na uwezo wa kumudu urefu wa kilomita 21.
Ofisa Habari wa Kampuni ya Vodacom, Leticia Kaijage alisema jana kuwa, mbio za kilomita 21, zitaanzia viwanja vya Biafra, hadi Uwanja wa Taifa.
Alisema zitamalizika viwanja vya Biafra huku mbio za kilomita tano zitaanzia Biafra kupitia kwa Manyanya mpaka daraja la Salender, ambako zitaendelea kupitia barabara ya Ali Hassan Mwinyi hadi Morocco na kurudi tena viwanja vya Biafra.