HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
jumapili, 30 Machi 2008
Pekua Tovuti
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari


Salamu kwenu makomredi wa chama chetu!
 
Juvenalis Ngowi


KABLA ya kutoa salamu zangu kwa makomredi watukufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa yote kwa kutujalia tena kuiona siku ya leo.

Hakika nitakuwa mtovu wa nidhamu na mwizi wa fadhila kama sitafanya dua yangu hii kabla ya wazo langu jepesi kabisa. Kisha baada ya dua yangu, niwasalimu makomredi kwa kuwaambia wakeshe maana hawajui muda tutakaposambaratika. Kigumu Chama Cha Mapinduzi!

Ninaandika waraka huu kwenu vigogo wa chama tawala mkiwa mmeanza kikao huko nyumbani kwa Mwalimu ingawa nafahamu wakati wa kuusoma mtakuwa mnamalizia au mmeshamaliza kikao chenu karibu na kaburi la Mwalimu.

Watu wamehoji, mnafuata kaburi la nini? Mwataka tuanze kudhania kwamba chama chetu kigumu kinachodumu kimeanza kupata mawenge? Mnaenda kutubu kwa Mwalimu? Mnaenda kumkejeli Mwalimu? Ni kipi hasa kilichowafanya mkumbuke alipolala Mwalimu wakati huu? Kigumu chama chetu!

Mnapokaa karibu na kaburi la Mwalimu mjikumbushe yale aliyowafunza. Mnakumbuka alikuwa muasisi wa chama chetu enyi makomredi wenzangu? Mnakumbuka alama za chama chetu ni jembe na nyundo?

Basi mnapokaa kando kando ya kaburi la Mwalimu, mkumbuke maana ya alama hizo kuwa ni wakulima na wafanyakazi. Mwalimu hakuanzisha chama cha wafanyabiashara. Nilishaandika zaidi ya mara mbili kwamba mkitaka chama chetu kiwawakilishe pia wafanyabishara, shuruti muongeze alama ya sarafu au noti kwenye nembo ya bendera yetu ya chama. Kwamba kuwepo alama ya jembe, nyundo na sarafu.

Bado mnadhani hiki ni chama cha kuwasimamia wakulima na wafanyakazi? Jitazameni wenyewe halafu mtuambie kati yenu ni yupi anatoka katika moja ya matabaka hayo mawili. Kila mmoja ajitafiti kwenye nafsi yake atuambie kama kweli bila wafanyabiashara angekuwa mahali alipo.

Chama chetu kimeporwa na kuhodhiwa na wenye fedha. Bahati mbaya hakuna anayejua uhalali wa fedha hizo. Nani anajua kama hazitoki kwenye dawa za kulevya? Nani anaweza kututhibitishia hazina uhusiano na ubadhirifu wa Benki Kuu?

Kuna tetesi mtaani kwamba magari ya chama chetu katika mikoa ya Arusha na Mwanza yalikuwa yakijazwa mafuta bure kwenye vituo vya mmoja wa watuhumiwa wa ufisadi wa Benki Kuu. Kama hili ni kweli, inabidi kutubu mbele ya kaburi la Mwalimu mlilolifuata vinginevyo chama chetu kitabaki kaburini.

Enyi makomredi, siku nyingi kabla mwenyekiti wenu hajatoa angalizo la kutenganisha biashara na siasa, niliwahi kuandika kuhusu hatari inayokikumba chama chetu kwa kukumbatia wafanyabiashara. Mmoja wa wasomaji aliyejitapa kwamba amesomea Ulaya elimu ya siasa, alinikejeli na kuniambia kwamba hata Freeman Mbowe ni mfanyabiashara.

Nilimpuuza kwa kuwa sikumtaja Mbowe kama mfano katika makala ile. Nikajua huyo kama amesoma siasa, basi amezikariri vinginevyo asingetoa hoja ambayo ilikuwa nje ya mstari, nilionya kwamba CCM iko kwenye janga kwa kuwakimbia wakulima na wafanyakazi.

Sasa mwenyekiti keshatamka kwamba hakuna budi kutenganisha siasa na biashara. Bwana yule sijui kama atamtafuta mwenyekiti na kumwambia kwamba Mwenyekiti wa Chadema ni mfanyabiashara! Sijui.

Lakini ukweli ni mmoja, CCM imekimbia asili yake na inabidi iamue moja kati ya mawili. Ipotee au igeuke nyuma na kurudi kwenye asili yake. Hakuna njia mbadala.

Makomredi watukufu, mnapokaa karibu na mwili wa Mwalimu uliolala Butiama, mkumbuke jambo moja muhimu. Chama chetu hakiko madarakani kwa ajili ya sera zake bora wala kwa ajili ya kukubalika na wengi.

Kiko madarakani kwa sababu mbili. Ufahamu wa wananchi wengi bado ni finyu na wamehadaika na majigambo yetu. Pili hakukuwa na chama mbadala cha kuchukua nafasi yetu wakati wa kupiga kura. Lakini sababu hizi mbili zitapitwa na wakati hivi punde.

Wananchi wameanza kupata pambazuko la akili. Walizomea mawaziri kwenye ziara zao. Wamepiga kelele dhidi ya ufisadi na mafisadi. Wameamka na wamegundua kwamba senti chache zinazotembea kabla ya kupiga kura si suluhisho la matatizo yao.

Historia imetufundisha kwamba watu katika ujumla wao hawawezi kudanganyika wakati wote. Muda wa kugawa fulana, kanga, kofia na kugawa senti chache kwa wapiga kura unapita kwa haraka. Muda wa kuwarubuni wananchi unatokomea kwa kasi.

Asiyeamini asubiri aone. Kuhusu vyama mbadala pia mjue kwamba ilikuwa ni suala la muda. Wapinzani wetu wanakomaa. Wamekoroma hadi tukafahamu kuhusu ujambazi ndani ya Benki Kuu. Wamenguruma hadi wafuasi wetu wakafanya maasi matakatifu wakalazimisha bwana mkubwa ajiuzulu.

Dalili ya mvua ni mawingu. Mawingu tumeyaona. Hivyo mvua itanyesha. Tutaficha wapi nyuso zetu kama hatutatubu mbele ya kaburi la Mwalimu mlilolifuata wenyewe? Kigumu chama chetu!

Lakini yote haya yametokea kwa sababu ya kushabikia utatu haramu. Utatu usio mtakatifu wa biashara, siasa na madaraka. Wanachama wetu hawawi makomredi wa kweli kwa kuwa wanavaa mavazi ya kijani. Hawawi waadilifu kwa kuimba mapambio ya chama.

Wapo waliovaa magwanda ya chama, lakini tunahisi wana mkono katika ujambazi wa Benki Kuu. Wapo wanaoimba kwa bidii zidumu fikra sahihi zisizokosea za Mwenyekiti wa CCM, lakini tuna shaka ya haki kwamba wameshiriki kutuuza katika miradi tata ya umeme.

Wapo tuliodhani damu yao ni kijani kama bendera ya chama, lakini walikiuka maadili ya uongozi kwa kufungua vioski kwenye ofisi ya umma. Wapo tuliodhani chama chetu ni zaidi ya wazazi wao, lakini wakasaini mikataba yenye utata katika mazingira tata.

Tuna wakati mgumu enyi makomredi wetu mliokimbilia mbele ya Mwalimu. Msipokana kwa maneno na matendo maovu yote yaliyotokea, laana ya Mwalimu haitawaacha. Mtakuwa mmeifuata wenyewe huko.

Historia ina mafunzo mengi ambayo si lazima yatufurahishe enyi makomredi wapendwa. Dola ya Rumi ilidondoka. Aliyejipa urais wa maisha wa Malawi, marehemu Kamuzu Banda alifariki akiwa ameshatolewa ofisini.

KANU kilikuwa chama tawala kwa jirani zetu Kenya. Mbwembwe na namna yake ya kuhodhi madaraka vilikuwa kama au zaidi ya mbwembwe za CCM. Mwenyekiti wake wakati huo, Daniel arap Moi alifikia mahali pa kuitwa profesa wa siasa. Lakini pamoja na yote hayo, chama hicho kiliangushwa chali kwenye uchaguzi. Hakuna chenye mwanzo kisichokuwa na mwisho.

Chama chetu kitukufu na chenye historia iliyotukuka kina mwanzo, hivyo pia kina mwisho. Ole wa chama chetu kama kitafikia mwisho huku makomredi wetu wakiwa wamegubikwa na kashfa za kupora mali ya umma.

Hata kama si wao, labda rafiki zao. Tusipojitakasa tusubiri kutakaswa kwa moto. Hapo hakutakuwepo cha kinga wala msamaha. Tuwatose wanaotaka kututosa ili tujinusuru. Kigumu chama chetu. Wasalaam.

kevinmakyao@hotmail.com
0784 265072


juu

Warning: mysql_connect() [function.mysql-connect]: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2) in /hermes/bosweb/web098/b983/glo.freemanm2/include/comment.php on line 9
I cannot connect to the database because: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2)