HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
jumapili, 30 Machi 2008
Pekua Tovuti
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari


Hip Hop (12)
 
Innocent Nganyagwa


SAFARI yetu ya kuchimbua chanzo cha hip-hop inazidi kuchanja mbuga.

Leo tuko katika kituo cha kumi na mbili, kina kinazidi kuzama.

Tunaanza na muhtasari wa wiki iliyopita wa kituo cha kumi na moja, kisha tutaendelea na ngwe ya leo.

Kimsingi tuliona nyimbo za kwanza kabisa zilizotumika kushushia mistari kwenye rap zilipigwa na bendi, hiyo ilileta heshima kwa wanamuziki waliopiga nyimbo hizo.

Mchango wao umesaidia sana kuundwa kwa msingi wa hip-hop kutokana na kutumiwa kwa nyimbo hizo na wale Mc’s.

Hapo tukazama kwa kina na kuona mfululizo wa nyimbo ambazo tulijitahidi kufafanua jinsi zilivyokuwa kimuundo.

Traki hizo, nilizozitaja, ni pamoja na ‘Give It Up Or Turn it Loose’-Jungle Groove Remix- ya James Brown ‘The Godfather of Soul’ huo ulikuwa kama wimbo wa taifa wa hip-hop ulioshabikiwa sana na wadau.

Nyingine ni ‘Get Into Something’ ya ‘The Isley Brothers’ ngoma iliyotengenezwa ki-B-Boy, ‘Melting Pot’ ya Booker T. & The M.G.'s, jazz la ki-hip-hop ‘Listen To Me’ ya Baby Huey wimbo uliopendwa zaidi na ‘ma-underground’ wa ki-B-Boys wa Dj Kool Herc.

‘Scorpio’ wa Dennis Coffey & The Detroit Guitar Band ndio uliotesa sana mwaka 1971, ni funky lenye ‘ma-break’ ya kiaina, Mc Young na LL Cool J walitumia ‘instrumental’ yake kuimbia traki zao za ‘Bust A Move’ na ‘Jingling Baby’

Ikashushwa traki iliyojizolea umarufu mkubwa ya Jimmy Castor Bunch yenye kianzio cha maneno “What we're gonna do right here is go back, way back” maneno haya utakuwa umewahi kuyasikia kwenye wimbo wa mtindo wa kwaito, yamerudiwa na kundi la TKZee kutoka bondeni, Afrika Kusini. Ngoma hiyo ya mkali Bunch iliitwa ‘It's Just Begun’, ‘Apache’ wa Michael Viner na Bongo Band kutoka Jamaica, hip-hop ya ki-calypso, wimbo ambao haukukosekana katika collection ya Kool Herc na kurudiwa tena baadaye na Sugarhill Gang, ni ngoma nyingine iliyokuwa kali kupindukia.

Wacko Jacko, Michael Jackson, alitoa mchango wake kupitia ‘Hum Along And Dance’ wimbo wao katika kundi la The Jackson Five, B-Boy na mashabiki wa Jacksons Five walipagawishwa vilivyo na traki hiyo.

Nyimbo zilikuwa nyingi sana kama vile ‘Love The Life You Live’ wa Black Heat waliou-sample kwa Kool & The Gang, ‘Theme From S.W.A.T’ wa Rhythm Heritage na ‘Dance To The Drummer's Beat’ wa Herman Kelly & Life, wimbo ulioibuka mwishoni mwa miaka ya 70.

Huu ulikuwa na nafasi kubwa ya ‘instrumental’ kwa Dj au Mc kuonyesha ujuzi wake wa kushusha mistari.

Nyimbo zote hizo, zilipigwa na bendi.

Tulifunga safari ya kituo kilichopita kwa swali, lini na nani aliibuka na wimbo wa kwanza kabisa uliotengenezwa ki-rap hasa na si ki-bendi?

Tukaahidi kuanzia hapo, wiki hii, basi tusonge!

Wimbo wa King Tim III ‘Personality Jock’ wa Fatback ndio unaosemekana kuwa wa awali kabisa wa ki-rap.

King Tim III, alikuwa ni rapa kutoka Harlem aliyeibuka baada ya kujipenyeza kwenye kundi la funk la Fatback.

Alianza kwa ku-rap na bendi hiyo inapotumbuiza na kusisimua mashabiki kwa kuwaimbisha, aliwakonga watu vilivyo.

Lakini unaweza kuuliza, mbona zile nyimbo nyingine nazo si zilipigwa na bendi?

Tofauti ni kuwa, huyu hakuchukua wimbo wa bendi uliokwishapigwa tayari na kupangapanga namna ya ku-flow, bali aliundiwa mapigo na bendi hiyo kwenye kuwakilisha jukwaani.

Ni muhimu kueleza hapa kuwa nyingi kati ya nyimbo hizi, zile za awali na zilizofuata zilitikisa sana kupitia disko na kupenya jamii yote ya Wamarekani, si Bronx tu.

Ni nyimbo zilizoakisi uasi, zenye vionjo vya mirindimo ya asili ya Kiafrika na Kijamaica, utakumbuka kuwa Kool Herc alitokea huko.

Nyimbo hizo ziliwawezesha madensa wa ki-B-Boys kujirusha kwa staili walizotaka na kustaajabisha watu ambao mara nyingi waliwazunguka na kuwakodolea macho.

Kumbuka B-Boys, ndio waliojengea utamaduni wa hip-hop mtaani kama tulivyoeleza wiki iliyopita, katika kusakata kwao magoma walishindana wenyewe kwa wenyewe na kutafuta nani mkali baina yao. Baadhi ya makundi ya B-Boy yaliyoshindana kwenye vitongoji vya Bronx na Harlem ni Herculoids (vijana wa Dj Kool Herc), The Nigga Twins, Clark Kent, DST, DJ Coke La Rock na wengineo.

Mashindano ya B-Boy yalikuwa zaidi mitaani, hayakufaulu kuvuka na kuingia kwenye madisko ya klabu.

Mpaka kufikia hapo rap ikawa imeshapata maendeleo ya kutosha kwa kusonga mbele, lakini unakumbuka yale mambo ya ‘zigilizaga’ tuliyoyasema awali kwenye sehemu za mwanzoni za uchambuzi huu?

Kama ndio, soma kwa makini sehemu ifuatayo hapa chini.

Dj Hollywood, ndiye alikuwa rapa wa kwanza aliyeanza kutumia mtindo wa ‘rhythmic disco rap’.

Huu ni mtindo uliozingatia vina na mizani, lakini ulipindisha ‘zigilizaga’ kwa mbali na kuwa kama kuimba.

Huyu si yule JT Hollywood, Mc wa Dj Pete Jones, ni mwingine ambaye badala ya kuweka mizizi yake Bronx tu, alitembelea vitongoji vingi vya New York.

Aliutumia vyema umaarufu wake ulioanzia kwenye Klabu ya 371 ya huko Bronx kusambaza mizizi yake maeneo mengine.

Sifa yake ya ziada ni uwezo wa kutumbukiza ladha kwenye rap zake za ki-melody, tofauti na ma-Dj na Mc’s waliomtangulia.

Wale wa awali, walisikika zaidi kama watangazaji wa redio wanaochangamsha wasikilizaji, wakati walipochangamsha umati uliokuwa kwenye dancing floor.

Hollywood alichanganya ghani, midundo na miito ya ziada ya kusisimua kwa mashabiki.

Alichomekezea maneno kama vile ‘Everybody scream!’ na ‘Throw ya’ hands in the air!’ ambayo baadae yalikuwa ya kawaida katika kusisimua umati.

Mpaka kufikia miaka ya mwishoni mwa sabini, yeye ndiye alikuwa Dj namba wani wa New York, kila alikopiga disko alijizolea mashabiki wengi sana.

Ni wakati huo huo pia Klabu ya 371 ndio ilikuwa maarufu kuliko zote katika jiji hilo. Wakati hayo yakitukia, uhasimu baina ya DJ Pete Jones na DJ Kool Herc uliendelea.

Tatizo la Herc na Jones ni kwamba, hawakupata hata kuthaminiana michango yao kwa muziki huo, hata mashabiki wao walikuwa tofauti.

B-Boys walitokea ghetto wakati wale wa ma-disko ya klabu walitokea kwenye maisha ya kati na ya kitajiri.

Lakini, pande zote hizo mbili ziliendeleza hip-hop licha ya upinzani baina yao, kila upande ukitimiza wajibu wake.

Sifa nyingine ya ziada ya Dj Hollywood ni mvuto wa sauti na uwezo wake.

Kwenye mashine aliongozwa na Dj Junebug. Timu hiyo ya watu wawili unaweza kuilinganisha na ile ya Dj Pete Jones na Grand Master Flash kwa jinsi ilivyofanya kazi vyema.

Dj Junebug, aliuawa mwanzoni mwa miaka ya 80.

Okay msomaji, ngwe yetu ya leo inatia nanga hapo. Tumeshazunguka sana Bronx katika kuona msingi wa hip-hop ulivyojengeka, tukirudi tena wiki ijayo tutaanza taratibu kuelekea maeneo mengine ndani ya Marekani. Pamoja!

Mwandishi wa makala hii ni mwanamuziki mkongwe wa miondoko ya reggae hapa nchini. Kwa maoni na ushauri anapatikana kwa simu namba: +255 752 227 594, barua pepe: rasinnoganyagwa@yahoo.com


juu

Warning: mysql_connect() [function.mysql-connect]: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2) in /hermes/bosweb/web098/b983/glo.freemanm2/include/comment.php on line 9
I cannot connect to the database because: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2)