MACHO ya Watanzania na masikio yao yote wanataka kusikia na kujionea utekelezaji wa mambo makubwa ya kitaifa, hasa yale yanayolenga kukisafisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kikao chake cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Ni wazi kuwa uamuzi wa chama hicho kujikita katika mji maarufu hapa Tanzania alikolazwa kiongozi wa kwanza wa nchi hii, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kutakuwa kumeacha maswali mengi kwa watu, wengi wakijiuliza hayo ya Butiama kulikoni?
Hakuna Mtanzania asiyefahamu tangu CCM ilipozaliwa mwaka 1977 makao makuu ya chama hicho hadi leo yapo Dodoma na ndiko kwenye kila aina ya miundombinu bora inayokifanya chama hicho kionekane kuwa na nguvu na makao yanayoheshimika.
Ndicho chama pekee kilichoshika nchi hii tangu ilipopata uhuru na ndicho kilichoweza kukubali na kupokea matakwa ya Watanzania wachache wa kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa bila kujali kundi la watu wengi waliokuwa wakipinga kuwepo kwa mfumo huo.
Watanzania wanajua na pengine wengi waliogopa kutoa maoni yao wakati huo wakidhani kuwa uamuzi huo utarekodiwa na kuwa kumbukumbu zitakazoweza kuwabana baadaye, lakini hivi sasa wanashuhudia kwa macho yao jinsi mfumo huo unavyoweza kufichua mambo mazito ya ufisadi na hujuma kali dhidi ya uchumi wa nchi.
Yote hayo wanayajua na wanajua fika kazi kubwa iliyofanywa na Baba wa Taifa ya kuijenga nchi yenye amani na utulivu, mtu ambaye hakuwa muongo, mnafiki wala mdhulumaji na hakuweza hata siku moja kutumia madaraka yake kwa ajili ya manufaa ya familia ya Nyerere hadi alipokufa akiwa masikini pamoja na familia yake.
Huyo ni Nyerere aliyeweza kuisimika CCM yenye kuamini fikra sahihi za viongozi wake na ni wazi hakuweza kuweka uficho kwa viongozi ambao aliona kuwa hawafai, aliwaumbua na hakutaka hata kidogo wachukue madaraka ya nchi, viongozi walioonekana kwake wana tamaa ya madaraka na uchu wa kujilimbikizia mali.
Nyerere wa Butiama hakupenda kumpa mtu sifa za uongo, hakupenda kumvisha mtu kilemba cha ukoka ili amridhishe kwa matakwa yake na hakupenda kumsifia mtu bila kutekeleza yale aliyodhani kuwa yanaweza kufanywa kama alivyotaka na kuagiza.
Huyo ndiye Nyerere aliyelazwa Butiama, ambaye leo makada wa CCM wameamua kuyakimbia makao makuu ya chama hicho, Dodoma kwenye Ukumbi wa Kizota ili kwenda kuzungumza yale ambayo wanadhani yanaweza kuwa mustakabali wa CCM na serikali yake kwa ajili ya manufaa na ukombozi wa kiuchumi kwa Watanzania.
Wakiwa huko, sidhani kama watatumia fursa hiyo kumcheza shere Nyerere wa Butiama kwa kutumia fursa hiyo kuwadanganya wananchi, kuvikana vilemba vya ukoka na kusifiana kwa mambo ambayo wameshindwa kuyatekeleza ukiwemo ufisadi uliopita mipaka.
Lakini kikubwa zaidi ambacho CCM ya Butiama inapaswa kufanya ni kuuweka wazi u-CCM wa Bara na ule wa Zanzibar ambao kwa utata mkubwa unahusu muafaka kati ya vyama viwili, yaani Chama cha Wananchi (CUF) na CCM yenyewe ili Watanzania waamini kuwa uwepo wa kikao hicho cha NEC (Taifa) CCM si kikao cha kucheza shere.
Hilo lazima niliseme nikiamini kabisa jitihada alizozifanya Mwenyekiti wa CCM (Taifa), Rais Jakaya Kikwete nchini Kenya ya kuvipatanisha vyama viwili vya ODM cha Raila Odinga na PNU cha Rais Mwai Kibaki, ndiko kulikoweza kuleta nafuu kubwa kwa Wakenya licha ya kupoteza uhai wa mamia ya wananchi wa nchi hiyo kutokana na vurugu za kisiasa.
Rais Kikwete alifanya kazi kubwa na ni wazi amejiandikia historia katika ukanda wa nchi za Kiafrika na dunia baada ya kufanikiwa kuleta amani na utulivu kwenye nchi hiyo na kufikia uamuzi wa kuundwa kwa serikali ya mseto ambayo leo hii huko Zanzibar, CUF wameafiki mfumo huo kuwa ndio utakaoweza kuondoa mvutano wa kisiasa visiwani humo.
Halmashauri Kuu ya CCM, ina kila sababu ya kutoa baraka zote ili kuhakikisha muafaka wake na CUF unafikiwa na serikali ya mseto inaundwa ili kuwafanya Wazanzibar kutulia na kukitumikia kisiwa hicho kwa nguvu zao zote bila kuwepo kwa uhasama wa kisiasa na mvutano usiokwisha.
Kwa msimamo huo na pengine ni fursa pekee kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Visiwani) Amani Karume kuridhia bila kinyongo uamuzi wa kwanza na wa kishujaa wa kuifanya serikali yake kuwa ya mseto, uamuzi ambao ni wazi kuwa kwa upande mwingine utawapoka tonge mdomoni wale waliokuwa na madaraka kwenye Serikali ya Karume.
Hatua hiyo haina ujanja na haiwezi kuepukika kama CCM itafikia uamuzi huo kwa ajili ya mustakabali wa kisiasa huko Zanzibar na mustakabali wa CCM kwa upande huo, vinginevyo sifa na hekima alizotuachia Baba wa Taifa ambaye ndiye anayeshuhudia vichwa vya makada hao vikigongana kwa hilo, sitegemei kuwepo kwa shere.
Hilo pengine ni kubwa kuliko maandalizi yanayofanywa na CCM kama sehemu ya mkakati mkubwa wa kulinda dola yake ifikapo mwaka 2010 kwa kuwa hali hivi sasa inatakiwa itengemezwe mapema kabla ya uchaguzi huo, ifikie mahali ikiamini kabisa yale yaliyotokea Kenya ni matunda ya kupuuza mambo muhimu na kuyafanya madogo.
Huko Butiama walipoketi makada hao bila kujali gharama kusitoe fursa ya kuendelea kuwaumiza vichwa Watanzania wakiamini kabisa kuwa fedha zinazotolewa kwa ajili ya kuviendeleza vyama vyenye wabunge ni fedha za walipa kodi na ni fedha zinazotokana na jasho la wananchi.
Nauona muafaka wa Zanzibar kama eneo kuu na muhimu zaidi kuliko jambo lolote, mengine yatakuja kwa wakati wake, lakini umefika wakati ambao tunapaswa kukiri wazi kuwa mbinu zote za kuchelewesha maafikiano zinatakiwa zikomee Butiama mbele ya kaburi la Mwalimu Nyerere.
Huko ndiko ambako hata kama hamtakubali, ndio sehemu pekee ya toba, ndio sehemu ya kusema ukweli, ndio sehemu ya kuonyana na kukemea vitendo viovu na ndio sehemu pekee ya kuuzika ufisadi wote ulioifikisha nchi hii hapa ilipo. Hakuna haja ya kusifiana kwa kufurahishana huku maisha ya Watanzania yakizidi kuwa magumu.
Butiama ya Nyerere inapaswa kuheshimiwa kama sehemu muhimu ya hija kwa watu wenye dhambi, watu waliojipatia madaraka kwa hila, watu waliojichotea mamilioni ya fedha za walalahoi kwa kuanzisha makampuni hewa na mikataba mibovu ni Butiama ya Nyerere ambayo haitaki hata tone la uchafu.
Nasema hivi kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kitakijengea sifa chama hicho tu kama wale waliohusishwa na ufisadi hata kama ni makada wa chama hicho watatimuliwa vinginevyo kitendo cha kuendelea kuwakumbatia mafisadi hao matunda yake yapo kwenye mikono ya wananchi siku watakapotakiwa kutumia haki yao ya kupiga kura.
Rais Kikwete naamini kabisa uamuzi wa kuketi Butiama kwenye kaburi la Nyerere kutakwenda sambamba na hekima na busara nzito kama zile ulizozitumia nchini Kenya na kuliondoa taifa hili kwenye aibu za ufisadi, wimbo ambao haufurahishi kusikika masikioni mwa wapenda haki na demokrasia ya kweli.
Kazi kubwa uliifanya ya kuunda upya Baraza la Mawaziri, ipo haja kubwa kuwageukia viongozi wa serikali na CCM kwa ngazi zote ili kuweka timu yenye kujali maslahi ya Watanzania, vinginevyo Butiama ya Nyerere itatugeuka na kilio chake kamwe hakitakoma hadi tutakaposimika umoja wa kweli wa kitaifa.
cnyenyembe@yahoo.com
0754 301864
0787 862586