jumapili, 30 Machi 2008

Tujihadhari na vitendo vya kitapeli makanisani kwa mgongo wa uchawi

TAHARIRI


TUNA mashaka na taarifa za kutatanisha zinazowahusu watoto wawili waliojulikana kwa jina moja moja la Yusufu na Ramadhani, kuwa wanafanya vitendo vya kitapeli, kwa kutumia mgongo wa uchawi.

Watoto hawa wanaelezwa kuwa katika matukio tofauti wamekuwa wakijifanya kuwa wamedondoka kutoka angani walikokuwa wakiwanga, kutokana na maombi ya waumini wa makanisa mbalimbali walikokwishawahi kufanya hivyo.

Shaka yetu inaanzia kwenye historia ya matukio ya watoto hawa kudondoka katika maeneo ya kanisa na umri wao. Wanakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka saba hadi kumi.

Kwa mara ya kwanza, taarifa za watoto hao kudondoka kutoka angani ziliripotiwa kutokea Januari 6, mwaka huu katika eneo la Tangi Bovu jijini Dar es Salaam.

Watoto hao wanadaiwa kufanya tukio kama hilo kwa mara ya pili katika kanisa moja huko Manzese, mwezi Februari, mwaka huu ambako polisi walifika wakawachukua na kuwapeleka katika kituo cha kulelea watoto yatima, Kurasini.

Katika hali ambayo inatutia shaka, watoto hao waliripotiwa kufanya tukio la aina hiyo hiyo hivi karibuni katika kanisa linaloongozwa na Mchungaji Gertrude Rwakatare, wakati waumini wa kanisa hilo wakiwa katika maombi.

Taarifa za kipolisi zinaeleza kuwa watoto hawa walihojiwa na polisi na baadaye walifanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Mwananyamala na kugundulika kuwa hawasumbuliwi na maradhi ya aina yoyote na kwamba afya zao ni njema.

Mara zote watoto hawa wanapodondoka kutoka angani huwa wanaombewa na waumini pamoja na wachungaji wa makanisa husika, hivyo tunaamini kwamba kwa nguvu ya maombi hayo watoto hawa hawana nguvu za giza zinazowatawala katika miili au akili zao.

Na tunaamini kwamba, ingawa baadhi ya watoto jijini Dar es Salaam ni watukutu na wana uwezo wa kujihusisha na matukio ambayo si rahisi kuamini kuwa yamefanywa na watoto, tuna wasiwasi kama haya yanayofanywa sasa na watoto Yusufu na Ramadhani hayana msukumo wa mtu au kikundi cha watu fulani.

Tuna imani hii kwa sababu tayari tumekwishapata uhakika kwamba rekodi za watoto hawa hazina hata chembe ya kujihusisha na mambo ya kishirikana, bali wanatumiwa kufanya matukio hayo kwa makusudi fulani ambayo mpaka sasa yanabaki hayajafahamika.

Matukio mengi ya watu wanaotuhumiwa kujihusisha na masuala ya kishirikina na kudondoka kutoka angani kila wanapopita katika anga za baadhi ya makanisa, yanatulazimisha tuamini kuwa huenda sasa uchawi umeanza kutumiwa kama njia ya kujipatia chochote.

Na iwapo imani yetu hii itakuwa sahihi, basi ni wazi kwamba lipo kundi la watu au watu ambao wameamua kuwatumia watoto hao ili kupata chochote kwa kufanya matukio ya kutisha ambayo huwasukuma watu kuwaombea na kuwapatia misaada ya aina mbalimbali.

Pamoja na imani yetu, tunapenda kuyashauri baadhi ya makanisa ambayo yamekutana na hali hii, kuwa makini na matukio ya aina hii kwa sababu yanaweza kuharibu kabisa sifa yake kwa jamii inayoweza kuwa na imani mbaya nayo.