HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
jumatano, 2 Aprili 2008
Pekua Tovuti
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari


CCM wasaliti



TULIPATA faraja kubwa wakati yalipoanza mazungumzo ya makatibu wakuu wa vyama vya CCM na CUF, Zanzibar, yenye lengo la kutafuta ufumbuzi wa mpasuko wa kisiasa visiwani humo.

Tulipata kuandika huko nyuma mara kadhaa kwamba, tukiwa sehemu ya Watanzania, wapenda demokrasia, tukaeleza bayana kuhusu msimamo wetu wa kuyaunga mkono mazungumzo hayo tuliyoyaona kuwa ni ya heri.

Hata hivyo wakati tukisema hayo, tulieza wazi wazi kuwapo kwa wasiwasi kuhusu dhamira ya kundi dogo la wahafidhina lenye lengo la makusudi kabisa la kuyavuruga mazungumzo hayo kwa sababu wanazozijua wao, wasiwasi ambao sasa umekuwa kweli.

Tulisema hivyo tukitambua kuwa kwa zaidi ya miaka 15, tangu Tanzania itangaze rasmi kuukubali mfumo wa ushindani wa vyama vingi, kumekuwa na mambo ambayo kimsingi yamekuwa yakizua maswali magumu kuhusu utayari wetu wa kuukubali mfumo huo na kuheshimu matokeo yake.

Ushahidi wa wazi kuhusu hilo ulikuwa ukijionyesha huko Zanzibar ambako chaguzi zote tatu za vyama vingi zimekuwa zikizingirwa na mambo ya ajabu ajabu ambayo kimsingi ndiyo yamezaa mazungumo haya ya sasa na mengine kabla yake.

Pamoja na ukweli huo basi, wasomi, wanasiasa na taasisi zinazoheshimika kwa pamoja wamekuwa wakitoa mapendekezo mbalimbali kuhusu namna ya kuendesha mambo visiwani humo, ambayo kwa bahati mbaya yamekuwa yakikwamishwa na viongozi walio madarakani na hususan wale wa upande wa Zanzibar.

Kwa mfano huko nyuma, kwa zaidi ya mara moja chama hicho tawala kilionekana kikifanya mchezo wa kuigiza wa kufanya kile ambacho machoni kilikuwa kikionyesha nia njema kabisa ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la Zanzibar.

Mwaka 2001 kwa mfano, baada ya hali ya kisiasa visiwani huko kuchafuka, CCM ililazimika kukutana na viongozi wa CUF na kukaa meza moja katika vikao ambavyo vilizaa muafaka wa Oktoba mwaka huo huo.

Hata hivyo, muafaka huo ambao pamoja na mambo mengine ulipendekeza kuangaliwa kwa uwezekano wa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa umeendelea kupuuzwa kwa matendo na kwa maneno na viongozi wa CCM, hususan wale wa upande wa Zanzibar kabla suala hilo halijazimwa kabisa majuzi huko Butiama katika uamuzi tunaoweza tukaueleza pasipo shaka kuwa ni wa aibu.

Jambo la ajabu ni kwamba, hata baada ya vikao halali vya chama hicho tawala na viongozi wake wakuu kutangaza kwamba, walikuwa wameamua kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la Zanzibar siku zilizopita, hili la sasa la kusema eti wanaurudisha muafaka kwa wananchi, linafedhehesha na kuturudisha nyuma sana.

Hata hivyo tukiwa sehemu ya Watanzania tuliofuatilia kwa karibu mchakato mzima wa suala hilo, tunaamini CCM imechukua hatua hiyo kwa sababu ya kuwahadaa Wazanzibari na jumuiya ya kimataifa huku ikijua fika kuwa imeamua kuukataa muafaka.

Kwa maelezo yoyote yale, Azimio la Butiama la kuzima muafaka kwa namna ya kisanii kama ilivyoelezwa na CUF, ni jambo ambalo Watanzania hatuna budi kuungana na kuinyoshea kidole CCM, ambayo sasa ni wazi imeamua kwa makusudi kuzima kiu ya miezi 14 ya Watanzania, na hususan Wazanzibari walio wengi. CCM imelisaliti taifa.


juu

Warning: mysql_connect() [function.mysql-connect]: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2) in /hermes/bosweb/web098/b983/glo.freemanm2/include/comment.php on line 9
I cannot connect to the database because: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2)