MLIMBWENDE Pendo Laizer, juzi aliibuka Miss University baada ya kuwabwaga wenzake 11 katika kinyang'anyiro kilichorindima viwanja vya World Cinema, Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Shindano hilo lililoanza majira ya saa 5:30 usiku, ambako mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Kanali mstaafu, Fabian Masawe, lilimalizika salama huku Pendo aliyekuwa amevalia namba tisa akiibuka kinara wa Kituo cha Vyuo Vikuu.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa onyesho hilo, mratibu wa shindano hilo, Rukia Mtingwa, alisema kuwa, shindano lilikuwa na ushindani kutokana na warembo wote kuwa na mvuto kitendo kilichowapa kazi majaji kumchagua mshindi.
“Hali imekwenda vizuri kama ulivyoona wewe mwenyewe, isipokuwa majaji walikuwa na kazi ngumu, kutokana na warembo kuwa katika hali nzuri, na napenda kusema kuwa, warembo ambao hawakubahatika si kwamba si warembo, isipokuwa nafasi zilizotakiwa zilikuwa mbili, hivyo wasikate tamaa,” alisema Mtingwa.
Kwa ushindi huo, Laizer alijinyakulia zawadi ya kompyuta aina ya ‘Lap Top’ mpya yenye thamani sh milioni 1. 2 pamoja na tiketi ya ndege itakayompeleka popote ndani ya nchi na sh 200,000 fedha taslimu.
Mshindi wa pili, aliibuka Joal Aboubakar ambaye alijinyakulia ‘Decoder’ na tiketi ya ndege ya kwenda popote ndani ya nchi na fedha taslimu sh 250,000 wakati nafasi ya tatu ilikwenda kwa Suwema Eton, aliyezawadiwa simu ya mkononi aina ya Nokia 3300 na tiketi ya ndege kusafiri kwenda popote ndani ya nchi sambamba na sh 100,000.
Nafasi ya nne ilikwenda kwa Veronica Lukindo, aliyefuatiwa na Mery Mzena, katika shindano hilo ambalo lilipambwa na burudani kutoka kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya, Profesa Jay na Chid Benzi.