MICHUANO ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, imepangwa kuanza Julai 12 mwaka huu jijini Dar es Salaam ikishindanisha jumla ya timu 12.
Michuano hiyo inafanyika nchini kwa mara ya pili mfululizo, ambako mwaka jana, APR ya Rwanda, ndiyo ilifanikiwa kutwaa ubingwa huku timu za Tanzania, ambazo ni Yanga, Simba na Mlandege ya Zanzibar, zikiangukia pua.
Kama ilivyokuwa mwaka jana, mwaka huu pia Tanzania itawakilishwa na timu tatu ambazo ni Yanga, Simba na Miembeni katika kuwania ubingwa wa michuano hiyo.
Ni habari njema kwa wapenzi na mashabiki wa soka nchini kupata fursa nyingine ya kushuhudia kipute cha michuano hiyo, wakiziona timu zao na nyingine zitakazoshiriki.
Kwetu tunaona ni nafasi nyingine kwa makocha wa Simba na Yanga kujaribu kulibakisha kombe nyumbani, pia kuona uwezo wa wachezaji wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Agosti 23.
Aidha, tukiwa sehemu ya wadau wa michezo na maendeleo kwa ujumla, tunatoa wito kwa Yanga, Simba na Miembeni kujipanga vema ili kuwa shindani katika michuano hiyo badala ya kuwa wasindikizaji.
Itakuwa ni aibu kwa timu za Tanzania kushindwa kubakisha taji kwa mara ya pili, licha ya kuwa nyumbani kama ilivyotokea mwaka jana, ambako wapenzi na mashabiki wakabaki kuzishuhudia timu ngeni zikicheza fainali.
Hii si aibu tu kwa Tanzania, pia ni hasara kwa waandaaji wa michuano hiyo iliyo chini ya udhamini wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame ambaye amekuwa akitoa dola 60,000 kila mwaka kwa ajili ya zawadi kwa washindi.
Wito wetu kwa timu za Simba, Yanga na Miembeni, ni kufanya maandalizi ya uhakika ili kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwani hiyo itakuwa ni heshima na hadhi kisoka.
Ni wazi, safari hii Shirikisho la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), wamejitahidi pia kutafuta wadhamini wenza wa michuano hiyo ambao ni Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), hali ambayo tunaamini itaboresha mashindano hayo.
Tunayasema haya kwa kuzingatia kuwa, kuendesha mashindano si kitu cha mchezo, ni gharama kubwa, hivyo bila wadhamini, hukwaza ufanisi wake.
Hivyo, kutokana michuano hii kuwa chini ya wadhamini wa uhakika, tunataraji kuona mashindano bora zaidi tofauti na miaka iliyopita, hivyo timu za Tanzania, nazo zinapaswa kupigana vilivyo ili kufaidi matunda ya uwenyeji.
Katika michuano hiyo, Yanga iliyo katika kundi C pamoja na timu za Awassa ya Ethiopia, Miembeni ya Zanzibar na APR ya Rwanda, inapaswa kujiandaa vema ili kufanya vizuri tofauti na mwaka jana ambako ilichemka.
Ni wito kwa dawati la ufundi la Yanga, chini ya Mserbia Dusan Kondic, kuandaa kikosi cha ushindani kitakachopigana vilivyo kubakisha kombe katika ardhi ya Tanzania.
Aidha, tunatoa wito kama huo pia kwa Simba iliyo chini ya kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kujipanga imara ili kuwa shindani katika michuano hiyo hata kutwaa ubingwa ili kuiepusha Tanzania na aibu ya kushindwa kutwaa taji hilo.
Ni matarajio kwamba, Simba iliyo katika kundi A, itapambana vilivyo kwani mbali ya lengo la kutwaa ubingwa, pia kama ilivyo kwa Yanga, Simba pia ni kujiimarisha kwa Ligi Kuu ya Bara, iliyopangwa kuanza Agosti 23.
Tukirejea kwa upande wa waandaaji (CECAFA) na wenyeji (TFF), kupitia kamati husika, vema pande hizo mbili zikahakikisha mashindano hayo yanaendeshwa kwa mujibu wa kanuni.
Tunataka kuona waamuzi wakitimiza wajibu wao ipasavyo kwani kama watafanya hivyo, wanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa mchezo huo yaani timu ikashinda au kufungwa kulingana na uwezo wake na siyo kubebwa au kuonewa.
Tunamaliza maoni haya tukiitakia kila la kheri michuano ya Kagame itakayoanza Jumamosi ya wiki hii huku tukizikumbusha timu za Simba, Yanga na Miembeni kupigana vilivyo kubakisha taji katika ardhi ya Tanzania huku waamuzi nao wakitimiza wajibu wao bila upendeleo ili soka yetu isonge mbele.