UPO msemo wa Kiswahili kuwa uzee ni jalala.
Katika mazingira yetu, tunaamini kuwa serikali ndiye mzee wa Watanzania wote na kwa maana hiyo, ni jalala lao.
Hapo ndipo wanapostahili kupeleka shida, manung’uniko, malalamiko na pongezi zao zote kuhusiana na maisha yao.
Kwa miaka mingi Watanzania wamekuwa wakifanya hivyo, lakini kutokana na hali hiyo, tunadhani kuwa kasi ya watu kwenda jalalani kutupa yanayowakera, si tu imeongezeka, lakini pia kuna mwitikio chanya mdogo sana.
Hili linafanya matumaini ya watu hawa juu ya mzee wao, kutoweka haraka. Iwapo haitachungwa, hali hii inaweza kusababisha matatizo, si tu kwa serikali yenyewe, bali katika jamii nzima.
Kwa ujumla wake, wananchi wamekuwa wakilalamikia kupanda kwa gharama za maisha.
Hali hiyo inazidi kuleta machungu sana kwa sababu ya kupanda kwa gharama za maisha, kunakochangia kukua kwa mfumko wa bei, ambako hakuwiani na kupanda kwa vipato vya watu.
Malalamiko ya wananchi juu ya hali hii, yamekosa majibu kutoka serikalini.
Sana sana kunazidi kuwafanya wananchi wazidi kupatwa na jakamoyo kuhusiana na mustakabali wa maisha yao ya sasa na ya baadaye.
Kauli ya hivi majuzi ya Rais Jakaya Kikwete akiwataka Watanzania wavumilie shida, inaweza kuwa ndicho kilele cha kuwakatisha tamaa.
Juzi juzi zimeongezwa nauli kwa usafiri wa aina zote, wa mijini na masafa marefu. Sababu ya ongezeko hilo ni lilelile linalosababisha ukali wa maisha-kupanda kwa bei za mafuta.
Nauli zilipandishwa baada ya kilio cha wanaoendesha biashara ya kusafirisha watu mijini na mikoani wakiomba nauli ziongezeke ili waweze kumudu kubakia katika kutoa huduma hiyo.
Hawa hawana dhambi yoyote. Kazi wanayoifanya ni ya msingi na kwakweli bila huduma yao, shughuli nyingi sana zitakwama.
Lakini wananchi wanaotumia huduma hizo, nao wakalalamika kuwa gharama mpya ni mzigo mkubwa sana kwao. Malalamiko haya yalitokana na sababu kuwa ongezeko la gharama za maisha halikufanywa sambamba na ongezeko la vipato vya wananchi, ili waweze kumudu maisha katika mabadiliko hayo.
Maana yake ni kuwa kwa kukubali ongezeko la nauli, serikali imezidi kuwafanya wananchi wake kuwa maskini zaidi kwa sababu wanachokipata bado ni kile kile lakini matumizi yameongezeka.
Katika hali kama hii, tunashindwa kuelewa iwapo jitihada za kumkomboa Mtanzania katika umaskini uliotopea zitafanikiwa kwa kasi tuliyoitarajia.
Tunapatwa na wasiwasi huo kwa sababu hata ongezeko la mishahara ambayo serikali imeshaanza kuwakopa wafanyakazi, inaelezwa kuwa iliongezwa kwa shinikizo, lakini serikali yenyewe haikuwa tayari kuleta nyongeza hiyo. Hayo yametamkwa na mmoja wa mawaziri.
Katika mazingira kama haya, mwananchi anaweza kuwa amechanganyikiwa, asijue la kufanya. Ndiyo maana kwa wale wenye nafasi ya kuwakamua wanyonge wenzao hongo, wanafanya hivyo ili kuziba pengo lililosababishwa na ongezeko la nauli.
Mtu ambaye ataweza kuiba muda wa kufanya kazi ili ajikite kwenye shughuli zake bibafsi, atafanya hivyo pia. Matokeo yake, tija itazidi kupungua na umaskini utazidi kutamalaki.
Kwa upande wao, wanafunzi wao waliamua kuandamana kutoa kilio chao kuhusiana na nyongeza ya nauli. Hivi sasa wanatakiwa kulipa sh 100 badala ya sh 50 za awali (kwa wale wa Dar es Salaam). Wanafunzi hawa, kwa kuelewa kuwa hali za wazazi wao ni mbaya kiuchumi, wameeleza bayana kuwa ongezeko la nauli kwao litawasababishia madhara makubwa katika masomo yao.
Wazazi wengi hawataweza kumudu gharama hizi. Hii inaweza kuwa sababu nyingine ya kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoacha shule.
Lakini kila mara tumekuwa tukisisitiza kuwa elimu ndiyo ufunguo wa maisha. Tunamaanisha nini kwa msemo huu wakati tunawakatili wanafunzi kuipata elimu? Hivi tunatarajia nini hapo baadaye wakati hivi sasa tunawanyima wanafunzi ufunguo huu?
Sisi tunaamini kuwa serikali inapaswa kuhakikisha kuwa wanafunzi hawapaswi kuhangaika katika harakati zao za kusaka elimu, kwa sababu wanajiandaa kuwa wakombozi wa taifa hili hapo baadaye.