HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
jumapili, 21 septemba 2008
Pekua Tovuti
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari


Mbeki adondoshwa


na Mwandishi Wetu na mashirika


MGOGORO baina yake na hasimu wake kisiasa unaonekana kuanza kumweka mahali pabaya Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki. Kwa muda sasa, Mbeki amekuwa katika shutuma nzito, akidaiwa kushinikiza hatua za kisheria zinazochukuliwa dhidi ya hasimu wake mkuu, Jacob Zuma.

Chama chake cha ANC kinaonekana kuanza kumtosa baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kilichomalizika jana, kumtaka aachie madaraka ya urais mara moja.

Hivi sasa Zuma ni bosi wa Mbeki ndani ya chama, kwani katika uchaguzi uliofanyika mwaka jana, Zuma alimshinda Mbeki na kunyakua uongozi wa chama hicho.

Uamuzi wa NEC ya ANC unakuja siku chache tu baada ya jaji mmoja nchini humo kuitupilia mbali kesi ya ulaji rushwa iliyokuwa inamkabili Zuma, akidai kuwa mashitaka hayo yalikuwa na harufu ya kisiasa.

Katibu Mkuu wa ANC, Gwede Mantashe, aliwaambia waandishi wa habari kuwa Mbeki anafahamu kuhusiana na maamuzi hayo ya chama lakini hajaweka wazi iwapo atayatekeleza.

Zuma anatarajiwa kumrithi Mbeki kwenye nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika mwakani nchini humo.

Jana hiyo hiyo, taarifa zilieleza kuwa, kimsingi, Mbeki alikubaliana na uamuzi wa chama chake wa kumtaka ajiuzulu nafasi yake ya uongozi wa nchi.

Msemaji wa kiongozi huyo, Mukoni Ratshitanga, alisema kuwa Mbeki ataondoka madarakani baada ya matakwa ya kikatiba kufuatwa na kukamilishwa.

Taratibu za kikatiba anazozizungumzia Mbeki ni pamoja na suala hilo kufikishwa bungeni na kutolewa maamuzi. Halmashauri Kuu ya ANC ambayo imemtaka kujiuzulu, kimsingi haina mamlaka ya kumwondoa katika nafasi yake isipokuwa Bunge, ambalo ndilo linalomuidhinisha rais.

Bunge linatarajiwa kukutana siku chache zijazo kwa ajili ya kukamilisha taratibu ili kumwezesha Mbeki kuondoka madarakani rasmi.

Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, Spika wa Bunge atachaguliwa kuwa kiongozi wa muda wa nchi.

Inaelekea Mbeki alitarajia uamuzi huu kwani alipopewa taarifa kuwa chama chake kinamtaka ajiuzulu, hakuonyesha kushituka.

Mantashe alisema kuwa uamuzi wa kumtaka Mbeki aachie ngazi ulifikiwa kwa ajili ya kulinda utulivu, amani na maendeleo ya Afrika Kusini.

Aliwaambia waandishi wa habari kuwa hii si adhabu kwa Mbeki kama ambavyo baadhi ya watu wanaweza kutafsiri. Alisema hata akiondoka madarakani, Mbeki ataachiwa baadhi ya majukumu yake kama vile kuendelea kuwa msuluhishi wa mgogoro wa Zimbabwe.

Wakati huo huo, mawaziri wanaotokana na WNC wametakiwa kutojiuzulu nafasi zao ili kuhakikisha uimara wa serikali.

Hata hivyo, uamuzi huo utabadili kabisa hali ya kisiasa nchini humo.

Mbeki, ambaye alirithi nafasi ya kiongozi wa chama mwaka 1997 kutoka kwa Nelson Mandela, anaonekana kama mtu aliyejitolea maisha yake kwa ajili ya ANC.

Kwa mara ya kwanza alishika nafasi ya urais mwaka 1999 na muhula wake wa kwanza ulipokamilika mwaka 2004, alichaguliwa tena kuendelea na nafasi hiyo.

Atakumbukwa kwa kufanikisha maendeleo makubwa ya kiuchumi nchini humo tangu kuanguka kwa siasa za ubaguzi wa rangi, ingawa bado watu wengi, hasa weusi, wana hasira kutokana na mgawanyo usio sawa wa utajiri.

Hadi sasa, sehemu kubwa ya utajiri nchini humo unashikiliwa na weupe wachache.


juu

Warning: mysql_connect() [function.mysql-connect]: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2) in /hermes/bosweb/web098/b983/glo.freemanm2/include/comment.php on line 9
I cannot connect to the database because: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2)