BAADHI ya wakazi wa Dar es Salaam wanaotumia usafiri wa daladala nchini, wamedai kuchoshwa na usumbufu wanaoupata magari hayo yanapokatisha safari zake kinyume na zilivyopangiwa, jambo linalosababisha kutumia fedha nyingi kwa nauli.
Wakizungumza jana na Tanzania Daima Jumapili kwa nyakati tofauti, abiria hao walisema tabia hiyo imekuwa ikiwasababishia usumbufu na kuharibu bajeti ya matumizi yao ya kila siku.
Mmoja wa abiria aliyejitambulisha kwa jina la Juma Omary alisema tabia hiyo imeshamiri kwa magari yanayofanya safari zake kati ya Buguruni na Tabata.
“Hawa makonda huwa wanatushangaza sana wakati wakipakia abiria, wanadai gari linaishia njiani halafu gari likifika hapo wanapotaka hushusha abiri na kupandisha wengine, tunalazimika kutumia fedha nyingi kwa nauli wakati maisha ni magumu,” alisema.
Naye Gidion Philipo, alisema sababu ya daladala kuishia njiani husababisha wao walipe nauli mara mbili hata kama sio kwa gari hilo hilo walilopanda mwanzo.
“Unajua mtu unatokea labda Buguruni kwenda kivukoni, unapopanda gari la Kivukoni unaambiwa linaishia Kariakoo hapo inabidi ulipe 300 na ukifika Kariakoo inabidi uchukue usafiri mwingine utakaokufikisha kivukoni nao unalipa 300 sasa unakuwa umetumia sh 600, inaumiza sana,” alisema.
Wote waliomba mamlaka husika kuchukue hatua ili kukomesha tabia hiyo.