ASKARI wastaafu wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) wametishia kuifungulia serikali yao mashitaka, baada ya Wizara ya Fedha na Uchumi kukataa kupitisha viwango vipya vya mafao vilivyopendekezwa na Tume ya Uajiri ya vikosi hivyo.
Wakizungumza na Tanzania Daima Jumapili visiwani hapa juzi, askari wastaafu hao walisema wamefikia hatua hiyo kwa kile walichoeleza kuwa wizara imekwamisha malipo hayo mapya waliyotarajia kuanza kulipwa Januari, mwaka huu.
Walisema Tume ya Utumishi ya vikosi hivyo ilianzishwa kwa mujibu wa sheria namba 7 ya mwaka 2007, iliyopitishwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Baada ya sheria hiyo kupitishwa na Baraza la Wawakilishi, Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya SMZ, aliisaini na kuwa sheria halali, hivyo haipaswi kupingwa.
Walivitaja vikosi vya SMZ vilivyoathirika na uamuzi huo kuwa ni Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM), Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Kikosi cha Vyuo vya Mafunzo (Magereza), Zimamoto na Uokozi na Valantia.
Walidai kuwa awali viwango vya mafao viligawanyika katika makundi matatu - askari wastaafu walipaswa kulipwa kati ya sh mil 50, 40 na 20 kulingana na cheo alichokuwa nacho mdai hadi wakati anastaafu.
“Tume ya Utumishi ilirekebisha viwango vya mafao kwa asilimia zaidi ya 50. Marekebisho hayo tulitarajia yangetusaidia pale tunapoanza maisha mapya, lakini tumelipwa kwa viwango vya zamani,” alisema askari mmoja aliyeomba jina lake lisitajwe gazetini.
Mstaafu alisema hivi sasa wanawasiliana na wanasheria ili waweze kufungua kesi mahakamani, kwa vile viwango vya mafao walivyolipwa ni vidogo na havilingani na hali ya sasa ya maisha.
Walieleza kushangazwa kwao na Wizara ya Fedha kuzuia viwango vipya wakati vimekwishapitishwa na Wizara ya Nchi Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, pamoja na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali.
Walidai kuwa viwango vya zamani walivyolipwa vimewavurugia mipango yao ikiwamo uendelezaji wa ujenzi wa nyumba zao za kuishi.
“Binafsi nilitarajia nitalipwa milioni 25 kwa mujibu wa mapendekezo ya viwagao vipya, lakini nimeambulia shilingi milioni saba…unadhani nitaishi vipi na kuna familia inayonitegemea?” alidai mmoja wa wastaafu hao.
Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Hassan Haji Wambi, alilithibitishia gazeti hili kukwama kwa malipo ya viwango hivyo vipya, licha ya kukiri kuwa baada ya sheria namba 7 ya mwaka 2007 kupitishwa na Baraza la Wawakilishi, waziri alitunga kanuni na utekelezaji wake ulianza kusimamiwa na tume hiyo.
Hata hivyo, alieleza kuwa baada ya mapendekezo ya viwango vipya vya mafao ya wastaafu hao kuwasilishwa Wizara ya Fedha na Uchumi, ilibainika sheria hiyo inakwenda kinyume na Sheria ya Fedha ya mwaka 2005, inayoeleza kuwa malipo yoyote lazima yafanyike kwa kushauriana na wizara hiyo, kabla ya utekelezaji wake ili kuepuka kuathiri bajeti ya serikali, jambo ambalo halikufanyika.
“Jambo la msingi ni kuwa na subira, nyongeza zao zitazingatiwa baada ya kufikiwa muafaka katika kikao cha pamoja,” alisema Wambi.
Akizungumzia suala hilo jana, Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, alisema mafao mapya ya wastaafu wa vikosi yamekwama baada ya kutayarishwa kinyume na taratibu za sheria za fedha.