WAKATI Simba ya Dar es Salaam jana ilianza kupoza machungu yake ya vipigo viwili mfululizo katika Ligi Kuu ya Vodacom, Kocha wake Mkuu, Mbulgaria, Krasimir Sminelov Benziski, amesema anataka kurudi kwao.
Hatua ya kocha huyo inafuatia kuwapo kwa msigano baina yake na wachezaji wa timu hiyo, hatua inayodaiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kufanya vibaya katika michezo yake ya hivi karibuni kwa timu hiyo.
Akizungumzia azima yake hiyo mara baada ya kumalizika kwa mechi ya ligi hiyo jana kati ya Simba na Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Benziski alisema sababu inayomfanya kutaka kurudi kwao ni baada ya timu yake kupoteza mechi tatu mfululizo.
Simba ambayo jana ilitoka sare ya mabao 2-2 na maafande hao wa Dodoma, mchezo ambao Benziski aliuona ni mgumu kwani uliielemea sana timu yake, hivyo kusema anahitaji kwenda kwao kupumzika.
Katika mchezo huo Polisi ilianza kuandika bao lake la kwanza dakika ya 59 kupitia kwa Boniventura Mateza baada ya kupokea pasi safi ya John Kanakamfumu, kabla ya Simba kusawazisha dakika moja baadaye kupitia kwa Mnigeria, Obina Orji.
Bantu Admin aliiandikia Polisi Dodoma bao la pili katika dakika ya 62, huku Simba nayo ilisawazisha katika dakika ya 87, kupitia kwa Haruna Moshi aliyepokea pasi ya Adam Kingwande.
Kocha wa Polisi Dodoma, Sekilojo Chambua akizungumzia mechi hiyo alisema kwamba, wachezaji wake walichanganyikiwa, hasa safu ya ulinzi, hivyo kusababisha mashambulizi ya pasi ndefu.
Naye Moses Ng’wati kutoka Mbeya, anaripoti kwamba, Mechi ya Ligi Daraja la kwanza kati ya Kijiweni na Mbeya dhidi ya Polisi Iringa, imeitoa kifua Mbele kijiweni kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.