WADAU mbalimbali wa soka wamekuwa wakitegeana katika zoezi la uchukuaji fomu kwa ajili ya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwa Chama cha Soka cha Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA).
Akizungumza jijini Dar es Salaam, mratibu wa zoezi hilo ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya uchaguzi, Haduriki Kabunju alisema kwamba, zoezi hilo limezoroka kutokana na wadau kutegeana kila mmoja akisubiria fulani kwanza achukue ndipo na yeye ajitose kuwania nafasi.
Kabunju alipinga madai ya kuwa kiwango kikubwa kilichowekwa kwa ajili ya fomu za kuwania nafasi hizo ndicho kinachokweza watu kujitosa kuchukua fomu hizo na kusema kwamba kipo kawaida tu.
Wakati zoezi hilo litafikia tamati, Oktoba Mosi, mpaka sasa ni wadau wawili tu ndio wamejitokeza kuchukua fomu kuwania nafasi za ujumbe ambako wagombea hao ni pamoja na mwanasoka wa zamani, Abeid Mziba na Issa Mangungu.
Mkutano Mkuu wa Uchaguzi unatarajia kufanyika Oktoba 12, ambapo Oktoba nane na tisa zitakuwa siku za usaili kwa wagombea, ambako nafasi zinazowaniwa ni pamoja na ile ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu.
Nafasi nyingine ni katibu msaidizi, mhazini, mhazini msaidizi, wajumbe watatu wa Kamati ya Utendaji na mjumbe mwakilishi wa klabu za mkoa.