HII ni ngwe nyingine watu wangu, bado tunasonga na mistari yetu ya kiugumu. Mida kitambo hivi, ngwe mbili zilizopita, tulikuwa tumejikita kule kitaa cha jirani nchini Kenya.
Hapo watu wangu ni Afrika ya Mashariki, ambako hata Wabongo tuko eneo hilo, lakini hatutajikita hapa Bongo kwa sasa.
Kwanza nataka tusonge bondeni, lakini kabla hatujajikita huko kwa Mzee Madiba, tutapitia nchi mbili tatu hivi. Kule Kenya tulicheki mambo kibao ya maprodyuza wakali akina Dunga, waliojikita hata hapa Bongo.
Ma-dj kama Mosse ‘The Darkchild’ aliyewaibua washusha mistari, pia tuliona mobu za kuprodyuzi mikito ya kushushia mistari.
Hizo ni kama vile Ogopa Dj’s, Homeboyz, Mandugu Digital, Calif Records, Samawati Studios na Blu Zebra. Watu wangu, kule Kenya jamaa ni wabunifu wa beat kivyaovyao, ni mambo ya ‘genge’ ‘kapuka’ na ‘Boomba’ halafu wanajua sana ‘ku-sample’ kiaina, kiasi huwezi kustukia kuwa mikito yao ni sample.
Mistari ya Kenya iko hadi levo za kimataifa, manake kuna wagumu wao wachache wamejikita vitaa vya Uzunguni wanakotengeneza mistari ya kikwao.
Kwa mfano kuna jamaa wanajiita Social Misfit Entertainment, hiyo ni lebo ya kuprodyuzi mikito, kusimamia na kurekodi mistari iliyoanzishwa na Wakenya huko Uingereza mwaka 1998.
Kule Kenya, tulicheki hata jinsi redio zao zinavyorusha mistari hewani kimtindo, yaani kuna vipindi vya mistari mitupu. Halafu ma-Mc wao wanalipuka pamba za nguvu sana, kuanzia jukwaani, kwenye video na hata vitaani.
Tuliona mobu za watengeneza pamba ambazo nyingine zimejikita hadi Mamtoni, hizo ni kama vile Jamhuri Wear, Mau-Mau University Clothing Co, Fundi Frank, Stitch Styles na Ruff Wear. Kisha tuliona mambo yao ya tuzo kibao kama vile ‘Kisima Music Awards’ ‘CHAT’ na ‘The Groove Awards’. Lakini mbaya watu wangu ni kuwa, jamaa pamoja na kukomaa na mistari lakini bado kuna miyeyusho michache. Ma-Mc hawakamati pesa kama wanavyokomaa, kwahiyo huamua kudondosha singo moja moja badala ya albamu nzima.
Wanategemea sana kupata kipato kutokana na ‘ku-perfome’ jukwaani, ila wana misimamo mikali sana. Kama unawafahamu ma-Mc wa Arusha, hapa Bongo, kwa misimamo, basi kule Kenya ni kama hivyo.
Manake pale A-Town ni karibu kabisa na kule, sasa mambo ya ugumu wa Kikenya kidogo yamejikita Arusha.
Usicheze na wagumu wa A-town, wana misimamo mikali sana kama ya ma-Mc wa Kikenya.
Kwa kifupi hayo ni baadhi ya mambo tuliyoyaona ngwe ya mwisho tuliyokuwa kule kitaa cha jirani, Kenya, japokuwa ni kama tumeyaminya.
Manake najua watu wangu mnaipata sana mistari ya kitaa hicho, kwa kuwa kiko karibu na sisi, kwa hiyo hata mambo yao ya juzi kati tunayapata.
Si mnaipata ile mikito ya ma-Mc wao wa hivi karibuni, kama yule mzee wa kubanjuka, DNA?
Kimtindo jamaa wako fiti kimistari, japo wana lugha za dizaini ya kivyao kabisa, ukifika hata kule Arusha, unapata fleva za Kikenya, manake Sheng imejipenyeza.
Sasa baada ya hapo tuanze kusonga kuelekea Bondeni, lakini kwanza niwape ngwe ya mwisho ya ramani yetu.
Tangu tujikite hapa barani Afrika, kwenye ‘intro’ huwa nawakumbusha ramani yetu ya mistari, sasa kwa kipande kilichobakia ramani yetu inasomeka hivi: Tutajikita Angola kidogo, kisha tutasonga Botswana halafu tutatua Afrika Kusini.
Hapo tutakesha kiasi, tukitoka hapo tutakuja Zimbabwe kisha Msumbiji, halafu tutajikita Madagascar.
Baada ya Madagascar tutakuja hapa nyumbani Bongo, hapo ndipo tutakita breki za ngwe za mwishoni kabisa. Watu wangu ishikeni ramani hiyo kichwani, manake ndiyo tunayotiririka nayo kumalizia safari yetu ndefu ya mistari. Tujikite Angola kidogo, hapo mistari imechangamka kwa sana.
Kuna ma-Mc wakali ambao wengine hupenda kujikita kitaa cha jirani kule Sauz, manake pale watu wangu sio mbali kutokea hapo Angola.
Mobu za ma-Mc wa kule ni kama vile SSP na Army Squad, ambazo mara nyingi sana hujikita kule Bondeni na kujichanganya na ma-Mc wa kule kwa kupeana nao mistari.
Ni mambo ya ‘Featuring’ za kiugumu, ila hapo Angola hatukeshi, sasa twende kule Botswana, tuone nao mistari yao imekaaje.
Kwanza kule mipini haijajikita sana kwa nyenzo, yaani watu wakitaka kutengeneza traki za kikweli kweli, inabidi wajikite ama Sauz au Mamtoni kabisa.
Lakini kuanzia mwaka 1999, ma-Mc wa kule walianza kukubalika kutokana na lebo ya Phat Boy kupromoti sana mistari yao.
Mistari ikanoga na ma-Mc wakaanza kudondosha albamu zao, hao ni kama vile Mr Doe, Zuess, Ignition, S.C.A.R, Awesomore a.k.a Gaddamit, Nitro, Konkrete, HT, Flex, Dice, 3rd Mind, Kast, Nomadic na Draztik.
Watu wangu, jamaa wanajua sana kujitengenezea majina kama unavyoyacheki.
Ngoja nikupe maana ya baadhi ya majina hayo: ‘Ignition’ hiyo maana yake ni sawa na kusema kuanzisha, yaani pale unapotaka gari litembee unaliwasha kwa kufanya ignition.
Konkrete ni sawa na kuandika ‘Concrete’ si unajua majina ya wagumu yanavyoandikwa ki-graffith?
Hiyo maana yake ni kakamavu au ugumu, Dice ni dadu.
Hicho ni kile kidude fulani hivi, ambacho wacheza kamari ya bao hukizungusha kwenye kopo na kukifunika.
Kisha kikifunuliwa ile alama ya mchoro iliyoko juu ndio imeshinda, sasa kama uliweka fedha zako kwenye alama kama ile kwenye lile bao umekula.
Kama umeweka kwenye alama nyingine na sio ile iliyojipindua juu kwenye dadu, basi umeliwa, sijui kwanini jamaa aliamua kujiita hivyo.
Labda inawezekana anapoteza sana kimistari na hafunikiki, yule 3rd Mind jina lake maana yake ni akili ya tatu, sijui jamaa ana akili ngapi.
Lakini kule Botswana kuna tatizo kidogo la albamu za mistari, manake mida fulani zamani wagumu walidondosha sana albamu.
Kila mmoja alikomaa kutoka, lakini soko limekuwa dogo, yaani wanabanana na mipini mingine.
Lakini sio kama mistari imedorora kabisa watu wangu, manake ma-Mc bado wamekomaa bila kujali matatizo.
Ma-Mc kama Scar, Kast na 3rd Mind wamedondosha albamu kali, S.C.A.R alishusha kitu ‘Happy Hour’ na Kast akashusha kitu ‘Dazzit’.
Mwaka jana S.C.A.R alishinda tuzo za Channel O zinazoitwa ‘Spirit of Africa Award’ kama ‘Best Hip-Hop Artist’ yaani mkali wa mistari ya hip-hop.
Basi kwa leo tukitie breki hapa watu wangu, tukiwa tumeshamalizana na mambo ya Botswana. Ngwe ijayo tutachoma moja kwa moja kule Bondeni, ambako tutaanza kuangalia mistari ya huko imekaaje. Pamoja!
Mwandishi wa makala hii ni mwanamuziki mkongwe wa miondoko ya reggae hapa nchini. Kwa maoni na ushauri anapatikana kwa simu namba: +255 752 227 594, barua pepe: rasinnonganyagwa@yahoo.com