WAWEZA kujiuliza; ni lini tutaweza kukaa na kuzungumzia maslahi yetu ya taifa? Ninashawishika kujiuliza swali hili, kwani kila nitazamapo wananchi na viongozi wanaonekana kujadili yale tu yanayohusu tofauti zao zaidi ya umoja wao ama Utanzania wao. Twajadili kimafungu; bungeni tuko kimafungu, twajadili dini zetu ambazo mwishowe zinadhihirisha utofauti wetu.
Hata shuleni tuko kimafungu; kuna wa Kiingereza na wa Kiswahili. Mwishowe mtu aweza kujiuliza ni nini kinachotuunganisha na kutufikirisha Kitanzania kwa ajili ya Tanzania?
Kwa sasa si elimu, si lugha, si dini, si vyama wala falsafa. Twajadili tukiwa vipande vipande. Hatimaye ni kuambulia maslahi binafsi ya kwa ajili ya mtu na wanawe, kabila, dini na hata kikundi katika jamii.
Hatufikiri kama wamoja, kama Watanzania bali ni kama mimi na sisi akina fulani. Ndiyo maana mtu akikosea, nyumbani kwao anapokelewa kwa mbwembwe akionekana kuwa shujaa. Hii yote inaashiria kwamba hatupo pamoja. Maana hatuna cha kutuleta pamoja. Lugha yetu mashuleni iko wapi, elimu yetu ya msingi hadi chuo kikuu iko wapi.
Misingi haituleti pamoja. Hatuna uwezo wa kuamua kwa pamoja mkosaji ni yupi na afanyiwe nini. Kwani alioko katika kosa kama si ndugu, ni wewe mwenyewe, achilia mbali mwanao na watoto wake. Ni kwa kuwa hatupo pamoja, kelele na misuguano inazidi katika jamii.
Kwa mfano, suala la Tanzania kujiunga na OIC. Wabunge watatofautiana. Wakristo wataona haina maana, Waislamu wataunga mkono. Kwenye elimu ya juu nako tumegawanyika. Waliopewa mikopo hawatagoma, waliokosa watagoma. Shule za msingi, watafundishwa Kiswahili, wengine watafundishwa Kiingereza. Tumia matokeo ya tofauti hizi kwa makundi tofauti yalipo hapa nchini.
Utaifa wetu unazidi kuporomoka. Mwishowe tutaonekana hapa Tanzania ni kama tumekuja kutalii. Wengine wanadai wagawiwe cha kwao waondoke. Hii nchi inakwenda wapi? Hatuwazi tutaishi vipi baada ya muda fulani wa maisha yetu.
Kwa hakika mtindo wa maisha yetu hivi sasa unatufanya tuwe tunaandaa vizazi mchanganyiko ambavyo baadaye havitakuwa kitu kimoja. Mwishowe kutakuwa na mchanyanyato fulani ambao hautakuwa katika chungu kimoja kutokana na kushabihiana na kukubaliana, bali ulio tofauti, kila mmoja akijaribu kujitafautia nafasi kwa kadri ya uwezo wake.
Ni kipindi ambacho katiba haitaunganisha tena Wakristo na Waislamu, bali itabariki utofauti wao kama walivyokwishajibainisha kutokana na waasisi na Wamisionari. Ni kipindi kinachoandaliwa cha jamii fulani kuendelea kutamalaki katika utawala hadi mwisho wa dahari. Hii ni ishara mbaya, na yote haya tunayapalilia muda huu huu wa ukuaji wa demokrasia.
Ni kiongozi gani atakayetuvuta na kutukaripia kwamba hatwendi vizuri na kamwe hatutafika tunakokwenda? Ni kwa sababu tumegawanyika katika vipande vipande, hakuna kinachotushikilia na kutuweka pamoja. Na viongozi nao ni miongoni mwa vipande hivi ambao mapengo yao hayalandani hata wakiunganishwa wawe wamoja.
Ndiyo maana hadi bungeni hatuwazi tena pamoja, hatuwazi tena Kitanzania. Tunawaza ni vipi dini zetu zitakavyopata fursa katika katiba, ili uhakika wa nguvu na mamlaka viendelee kudumishwa upande wetu. Tunaona kwamba kuitwa Mtanzania Mungu hatakuona, ni hadi uwe ama Mkristo au Mwislamu. Hii ni hatari. Kwa kuwaza hivi Tanzania haipo.
Kama tutaendelea kutang’ang’ania haki ya kundi moja, hivi kweli wa Kilimanjaro atawaza kuwa kuna Mtanzania wa Mtwara? Vile vile wa Mtwara atawaza kwamba kuna Mtanzania wa Ukerewe? La hasha. Ni vigumu.
Kitendo cha baadhi ya viongozi wetu na wananchi hawa waliogawanyika katika vipande vipande, kukinzana kuhusu hoja kuwa Tanzania ijiunge na OIC au la, ni dalili kwamba tunakokwenda hapatuhusu kama Watanzania, bali tunakwenda kama wewe ni Mwislamu wakati mimi ni Mkristo. Hata Bunge, sehemu pekee ya kujadili maslahi ya Watanzania, inatumika sasa kujadili maslahi ya makundi makundi katika jamii.
Nasema hivi kwa sababu kama taifa tulishajiwekea taratibu na kanuni kuhusiana na masuala haya ya kimataifa. Vipo vigezo ambavyo vinatawala masuala yahusuyo dini. Kwa nini leo tuanze kulumbana katikati ya vigezo na kanuni tulizojiwekea wenyewe? Kitu gani kinatutia upofu hadi tunashindwa kuziona tena kanuni na vigezio hivi?
Hatujadili kwamba kama Watanzania, tufanye nini ili rasilimali zetu zitufae maishani, rasilimalimali watu hawa waunganishwe vipi ili waweze kuvuna mema ya nchi ambayo Mungu ametujalia.
Tusisahau kuwa tofauti zetu ni mwanya mzuri sana kwa wageni kujizolea malighafi zetu. Kwani hata itafikia kwamba hatutokuwa na mwanya wa kukaa pamoja na kujadili yaliyo yetu sisi Watanzania, bali kama kikundi katika Watanzania. Mathalan hata katika viongozi wetu, tutaelekea kuwachagua kwa misingi ya dini zao, lugha zao na fikra zao ambazo hakika hazina hata chembe ya kuujali umma wa Watanzania. Uwezo wa mtu kuongoza na moyo wa uzalendo hautapewa tena nafasi.
Hata maswali yetu kwa wagombea yatabaki kuwa ‘utatusaidiaje sisi kama kikundi katika nchi inayoitwa Tanzania?’ Na baada ya kuingia madarakani ataulizwa, ‘yale uliyosema tutakupa kura kwa ajili yetu mbona hutekelezi?’
Ni mzaha lakini ukweli unaanza kujidhihirisha katika chembechembe ndogo sana, na kutokana na udogo wake si makosa kuyadharau, na kuonekana ni tone tu katika bahari iliyojaa wanadamu zaidi ya milioni 35.
Endapo Augustine Mrema atasimama na kutetea Tanzania iingie IOC kwa sababu tu aliahidi hivyo wakati wa kampeni za urais, nadhani hatuwawajibishi viongozi wetu kwa misingi ya Watanzania bali kwa kundi la Watanzania. Sasa na Wakristo watataka watambilike kama Wakristo, je, tunatakuwa na Tanzania watu ama Tanzania ramani?
Tuachane na hoja za kutuondolea weusi wetu, Utanzania wetu, umoja wetu uliojengwa kwa misingi ya upendo na utu. Tuache kabisa. Kabla ya kudai tuangalie ‘kuna nini, na mimi ni nani’ na maamuzi yatakayochukuliwa yatasaidia mazingira na jamii inayokuzunguka.
Endapo kabla ya kujenga hoja juu ya Tanzania, ukajihoji kuna nini Tanzania na jibu likawa Tanzania kuna weupe na weusi, Wakristo na Waislamu, Wapagani na Wabhuddha, Wamasai na Wanyakyusa, kaskazini na kusini, mashariki na magharibi n.k, ukigundua hilo, uhakika wa kujenga hoja ya kuwafaa Watanzania wote ni mkubwa. La sivyo, mgawanyiko wetu wa kinadharia utajidhihirisha katika matendo.
Ni wakati mahsusi sasa wa kujua kuwa muda tunaopoteza katika kujadili na kuomba upendeleo miongoni mwa tofauti zetu, ndivyo tunavyosahau kuweka falsafa, na vipaumbele vyetu bayana. Na tukikurupushwa na maazimio ya kimataifa tuamka na kusaini, na badala ya kuangalia mbinu ya kuweza kuyafikia na kuyatimiza, tunarudi katika tofauti zetu. Mwishowe tunajikuta hakuna lililotimizwa.
Misingi muhimu ya kutuunganisha inaonekana kudharaulika. Shuleni si pahala pa kumleta pamoja Mkristo na Mwislamu, maskini na tajiri, Mgogo na Msambaa, Mhindi na Mwafrika. Shule zinawaunganisha Wagogo peke yao, shule za Kikrito pekee, Kiislam pekee, vyuo vya matajiri na maskini navyo vipo.
Na hapa mtu anakabidhiwa ofisi ya umma isiyo ya Mchagga au Mhaya, maskini wala tajiri, hapa mtu atafikiri kitanzania kweli, kwa lipi? Walioliona hili mapema walishauri JKT irudi. Wazo lilisikika lakini ni nani atende kwa ajili ya Watanzania wote, ilhali tunawaza kwa misingi ya dini zetu na kabila zetu?
Wazee wetu yawapasa kusimama sana na kutueleza kuhusu hawa vijana wanaosema kuwa wanamuenzi Mwalimu Nyerere kwa jinsi wanavyosimamia jamii ya Watanzania ikimeguka kipande kipande kila uchao. Waondokane na kushadidia demokrasia ilhali hatujui itaisaidia vipi Tanzania.
Wasomi nao waamke usingizini, watoe mawazo yao kama Watanzania na si kama Waislamu ama Wakristo, Wamakonde wala Wasukuma. Bali ni kwa elimu yao waliyoipata ambayo si kwa ajili ya kutafutia mikate yao binafsi bali kwa ajili ya Tanzania yote.
Tukiacha fikra zetu kudumu kwamba mtu wa kabila fulani asipewe ofisi ya umma kwa kuwa atafanya hivi na vile, mtu asinyimwe uongozi eti kwamba hataweza kushawishi katiba ibalishwe ili kudi dogo ama kubwa lipate haki fulani.
Mtu aamininike kwamba kwa maadili yake ya Kitanzania anaweza kuwahamasisha, kuwaunganisha na kuwasimamia Watanzania wenzake waweze kufikia lengo walilojiwekea.
Ni katika fikra zetu ambapo itaweza kujulikana kuwa Tanzania itakuwa vipi baada ya miaka kadhaa ijayo. Kwa hali ilivyo sasa hatuna muda wa kujadili hatima yetu kama Wanzania. Misuguano yetu ya chinichini na tukijidanganya tumeshikama ni sawa na vita ya panzi ambayo kunguru/mgeni kwake ni mwanya wa kuvuna asichokipanda.