KUKIRI kwa Rais Jakaya Kikwete, mwaka mmoja baada ya kuingia madarakani, kwamba alitumia muda wa miaka kumi kufanya hila zilizomwingiza Ikulu, ni moja ya dalili za wazi kuwa, kundi lake lipo katika mwelekeo wa kushindwa.
Hii inaweza kuonekana kama kauli ya kujipa matumaini yasiyokuwapo, lakini alama za nyakati, iwapo zitasomwa bila makengeza, zinaonyesha mwisho usio mwema kwa kundi hilo.
Ni bahati mbaya sana kwamba kwa muda wa miaka kumi, watanzania walishindwa kujua uhalisi wa matukio mengi sana. Yapo yaliyotokea na watu wakashindwa kuyahusisha na harakati za kampeni za urais, mengi ya matukio ya wakati huo, na yale yaliyoandikwa, yalionekana kama sehemu ya jumla ya mchakato wa kisiasa.
Lakini nini kilimfanya Kikwete akiri muda mfupi tu baada ya kuingia madarakani kuwa, alitumia muda wa miaka kumi ‘kujiandaa’ kuingia Ikulu? Moja ya sababu kubwa ya kimantiki inayotokana na usemi wa mwanamuziki nguli wa Reggae, hayati Robert Nesta Marley, al maarufu kama BoB Marley kuwa ‘unaweza kuwadanganya watu wote kwa muda mfupi, au unaweza kuwadanganya watu wachache kwa muda wote, lakini kamwe hauwezi kuwadanganya watu wote kwa muda wote.’
Lakini inaweza kuwa zipo sababu nyingine za kimbinyo, zilizomlazimisha Rais Kikwete kukiri ukweli huu uliofichwa kwa muda wa muongo mmoja. Mlolongo wa matukio nchini unaonyesha kuwa kundi lililomwandaa rais Kikwete kuingia madarakani, halipendi, wala halikujipangia kumaliza kazi yake kwa kuhakikisha Kikwete anaingia madarakani.
Kwa hiyo, kufichua mbinu za medani zilizotumiwa na kundi hili, kama alivyofanya Kikwete, ni dalili kuwa kulikuwa na aina fulani ya kibano kilichowalazimisha wakiri hivyo. Watu wanaweza wasikigundue kibano hiki hivi sasa. Haitashangaza.
Kwanza hii ina kuwa ni kwa sababu walikaa miaka kumi bila kugundua maandalizi yaliyokuwa yanafanywa kuingia ikulu. Pili, rais Kikwete alikiri hivi akiwa nje ya nchi. Inashangaza kuwa masuala ya kisiasa ambayo yanaweza kuonekana kuwa ni mambo ya ndani mno, yanaenda kutolewa ufafanuzi nje ya nchi. Kwa hiyo, inawezekana kuwa kibano hicho kilitoka nje ya nchi na rais ‘akalazimika’ kwenda kutoa kauli huko huko kilikotokea kibano ili aeleweke vizuri.
Kwa upande mwingine, tangu Rais akiri hivyo, yametokea mambo mengi ambayo kwanza yamedhihirisha kuwa lengo la kundi lake halikuwa linaishia 2015 tu. Kwamba wanalikuwa na dhamira, na matukio yanaonyesha kuwa bado wanayo, ya kuendelea kutoa kiongozi wa nchi hata baada ya Kikwete kumaliza muda wake kikatiba.
Rafiki yangu mmoja wa karibu aliwahi kunidokeza kuwa kwa mtu mjuzi wa mambo, akiangalia matukio kadhaa yalitokea katika kipindi cha miaka miwli na nusu iliyopita, ni dhahiri kuwa harakati za kundi hili, zinaonyesha kuwa ni mwendelezo wa safari yao kuelekea 2010 na zaidi ya hapo.
Lakini mikakati imebadilika. Kwanza ni kwa sababu Kikwete alishatoa siri ya mkakati wao wa miaka kumi. Hivyo ni dhahiri kuwa hawawezi kurudia tena kile ambacho walikifanya kwa sababu kinajulikana.
Sababu nyingine ni kuwa hapa katikati yametokea na yamesemwa mengi. Akina Dk.Wilibrod Slaa na Chadema yao wamesema na kufichua mambo mengi ambayo kwa kiasi kikubwa, ukichanganya na kukiri mwa Kikwete, kumewaamsha watanzania wengi.
Hali hii imesababisha wachezaji wakuu kuingia katika mikakati hiyo katika hii mpya dhidi ya walipua mabomu hawa. Ni mikakati ile ile kwa sababu tumeshuhudia jinsi ambavyo akina Slaa na wenzake walivyoandamwa kwa kashfa za kupikwa kama ambavyo akina John Malecela, Salim Ahmed Salim, Frederick Sumaye na Profesa Mark Mwandosya kwa kuwataja wachache, waliibukiwa na kashfa katika kipindi cha miaka kumi kabla ya uchaguzi mkuu uliopita.
Lakini sasa wanalazimika kubadili mbinu za mchezo. Katika mazingira kama haya ya Watanzania kuamka na kuibuka kwa wapiga kelele kama akina Dk. Slaa, mabadiliko ya mbinu za mchezo ni lazima. Na mabadiliko hayatahusisha kubuni mbinu mpya tu, bali kubuni pia mbinu mbadala, ili kukabiliana na hali yoyote itakayojitokeza ghafla na bila kutarajiwa. Ni lazima kuwa na mbinu mbadala kwa sababu inaokena kuwa waliokuwa rahisi kuwahadaa kwa miaka kumi wameamshwa na sasa si rahisi kuwadanganya tena kwa kutumia mbinu zilezile.
Lakini huko tunakoelekea tutarajie nini? Dk. Harrison Mwakyembe alishasema kuwa Watanzania si mabwege. Iwapo mabwana wakubwa hawa hawakuisikia kauli hii ya Dk. Mwakyembe, au kama waliisikia wakaipuuza, wanatakuwa wameianza mapema safari kama ile ya wale watu waliojikusanya zamani na kuamua kujenga mnara mrefu utakaofika hadi aliko Mungu, ili wapande wamchungulie. Mnara huu ulijengwa katika mji uitwao Babeli nao ulipewa jina la Mnara wa Babeli.
Wajenzi wa mnara huo hawakufanikiwa hata kufika nusu ya kazi yao kwa sababu dhamira yao ilikuwa ni kama kumkufuru Mungu. Walisambaratika na kusambaa katika uso wa dunia kila kundi likiwa na hamsini zake, wakikosa ule umoja ambao walianza nao wakati wa ujenzi wa mnara.
Kwa kuwa Watanzania si mabwege tena, sidhani kama watakubali wajengewe mnara kuwazunguka ili baadaye waje kuchunguliwa. Kama watashindwa kuwasambaratisha, kwa woga wanaweza kuamua kuwakimbia watu wanaojenga mnara katikati yao. Hapo wajenga mnara watajikuta wapo peke yao. Au Watanzania wakiamua kuwa jasiri, wanaweza kukamata bakora na kuwasambaratisha wajenzi wa mnara haramu kama walivyosambaratishwa wale wajenzi wa Mnara wa Babeli.
Haya si mambo ya kufikirika hata kidogo kwa sababu Watanzania walishaamshwa na wanajua kwa kiasi kikubwa kile kinachofanyika. Si mabwege na katika werevu wao, sasa wameanza hata kusoma alama za yale yanayotokea katikati yao. Hata kama wao hawana uwezo huo, lakini wameibuka mawakili wengine ambao wapo tayari kuwafafanunulia nini maana ya mambo ya nyakati hizi yanayotumkia katikati yao.
Kimsingi, watu wameshafahamu kuwa katika medani ya siasa nchini hivi sasa, hakuna kinachotokea kwa bahati mbaya au kama matukio ya kawaida ya kisiasa kama ilivyokuwa miaka kumi kabla ya 2005.