“UKITAKA biashara zako ziende vizuri basi jiunge na CCM, chagueni mafiga matatu ili muweze kupata maendeleo, mkichagua upinzani hatutaleta maendeleo.”
Hizo ni baadhi ya kauli zilizowahi kunukuliwa kutoka kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho ndiyo chama kinachoshikilia dola hivi sasa Tanzania bara na visiwani. Kauli hizi kwa kiasi kikubwa zinawahamasisha au kuwalazamisha wananchi wajiunge na CCM si kwa hiari yao, bali kwa lazima kutokana na shida zinazowakabili.
Jambo hili ni la kusikitisha sana kwani mfumo wa vyama vingi ulianzishwa kwa ajili ya kukuza demokrasia ya kweli ndiyo maana Mwalimu Nyerere alitoa ushawishi kwa watu kuubali mfumo wa vyama vingi licha ya kuonekana kutokubalika na watu wengi.
Nyerere aliona mbali na ajilijua kuwa vyama vingi ni changamoto kubwa katika maendeleo ya taifa na hata Spika wa Bunge Samuel Sitta, katika mkutano wa 12 wa Bunge uliomalizika hivi karibuni alikiri kuwa upinzani umeleta maendeleo na ufanisi kwa watendaji wa Serikali licha ya kuwa na uwakilishi mdogo bungeni.
Kauli kama hizo zikitolewa wakati wa kampeni za uchaguzi angalau tunaweza kusema ni njia ya kutaka kujipatia kura zaidi, lakini kwa bahati mbaya hata baada ya uchaguzi CCM huamua kuzifanyia kazi kauli hizo. Wakati dunia ikihangaika kila kukicha kukuza demokrasia, hapa Tanzania baadhi ya viongozi wa CCM wamekuwa wakitumia madaraka yao kutopeleka maendeleo sehemu zinazoongwa na vyama vya upinzani.
Aliyekuwa Waziri Mkuu katika serikali ya awamu ya tatu, Fredrick Sumaye, aliwahi kukaririwa kuwa kama mfanyabiashara anayetaka mambo yake ‘yaende vema’, basi ni vema akajiunga na CCM.
Lakini kibaya zaidi ni kauli ya hivi karibuni ya Katibu wa CCM mkoa wa Tanga, Idd Ame, alisema wataishinikza Serikali kutopeleka maendeleo katika kata zinazochukuliwa na upinzani na kuwaonya wananchi wasiwachague viongozi kutoka upinzani. Aliongeza kuwa wananchi walifanya makosa kuwachagua wapinzani katika chaguzi zilizopita ndiyo maana maendeleo katika maeneo yao yamekuwa ya kususua.
Ubaguzi wa aina hii ni hatari kwa maendeleo ya taifa kama CCM wanataka kuendelea na mfumo wa chama kimoja, ni vema wakatafuta nchi yao ili waweze kulitimiza jambo hilo ambalo kwa hakika ni kero kubwa miongoni mwa jamii. Leo hii majimbo, mitaa na kata yanayoongozwa na upinzani yamekuwa yakipata wakati mgumu katika maendeleo kwa kile kinachodhaniwa kuwa kuyaendeleza ni sawa na kukipa sifa chama cha upinzani.
Dhana hii ni dhaifu na haipaswi kupewa nafasi na inawanyima wananchi maendeleo ambayo ni haki yao ya msingi bila kuangalia mwananchi ana itikadi gani ya siasa. Kila kukicha, wanasiasa wa kambi ya wapinzani wamekuwa wakipiga kelele kutopelekewa huduma muhimu katika sehemu wanaazoziongoza na wamekuwa wakiilaumu CCM kwa kutumia fimbo la dola kuwanyima maendeleo wananchi kwa kuchagua kambi ya upinzani.
Ni aibu kwa Tanzania hii ambayo inasifika katika uso wa kimataifa kwenye kushughulikia migogoro na kukuza demokrasia, yenyewe inashiriki kikamilifu katika kukwaza ukuaji wa demokrasia. Marekani ni miongoni mwa mataifa machache duniani ambayo inaaminika angalau imekomaa kidemokrasia na mara kwa mara imekuwa ikishuhudia kupokezana vijiti vya uongozi baina ya vyama viwili vikubwa vya Republican na Democratic.
Pamoja na vyama hivi kuwa na sera tofauti lakini havijasisika vikidai iwapo wananchi wa nchi hiyo watakichagua chama kingine basi chama tawala kwa wakati huo hakitapeleka maendeleo kwenye majimbo yaliyoteua upinzani. Kila kukicha tumekuwa tukishuhudia maendeleo katika majimbo ya nchi hiyo na Waafrika wakizidi kuzikimbia nchi zao kuelekea huko kwa lengo la kupata maisha mazuri.
Hivyo hivyo, kwa Uingereza nao wamekuwa na siasa zinazotia moyo kwani siasa za ubaguzi zinazoanza kuchipua hapa nchini walishaachana nazo na wanachokiangalia zaidi ni maendeleo ya nchi yao bila kujali sehemu gani inaongozwa na nani.
Leo hii ukienda Zanzibar, hasa katika kisiwa cha Pemba, ambako ndiyo ngome kuu ya Chama cha Wananchi (CUF), utshuhudia kasi ya maendeleo yake imekuwa ni ya taratibu mno kulinganisha na upande wa pili unaoongozwa na CCM. Ukiuliza sababu ya kufanya hivyo utapata jibu kuwa eti kuyaendeleza maeneo hayo ni sawa na kuwapa sifa CUF.
Jambo hili ni hatari kulikubali na kuliacha liendelee kwani ni ukweli usiopingika kuwa Rais Jakaya Kikwete alipata kura hata kwa wale waliokuwa vyama pinzani na wengine wasio na chama chochote. Wapo watu wasiokipenda chama chochote cha siasa lakini wanahitaji maendeleo, kwani wanalipa kodi kupitia huduma mbalimbali wanazozipata hivyo si sahihi kutopeleka maendeleo sehemu fulani kwa misingi ya itikadi za siasa.
Wapo wafanyabiashara ambao sipendi kuwataja, ambao biashara zao zimepata msukosuko mkubwa kutokana na kuvisadia vyama pinzani au kwa wao wenyewe kuwamo kwa vyama hivyo. Bidhaa zao zilipoletwa hapa nchini ziliharibiwa kwa madai ya kuwa chini ya kiwango, wengine walifuatwa na maofisa wa Mamlaka ya Mapato kwa madai ya kutolipa kodi ipasavyo. Mambo yote hayo yanafanyika ili kuwakatisha tamaa wasiendelee na harakati za kuunga mkono vyama vya upinzani.
Ni vema siasa za namna hii zikaachwa kwani itafikia wakati eneo fulani litajikuta lina maendeleo zaidi kuliko jingine na kuwafanya wananchi wa eneo lisilokuwa na maendeleo kujenga chuki dhidi ya viongozi na inawezekana wakasababisha vurugu. CCM wanapotumia dola kudhoofisha maendeleo katika majimbo ya upinzani, ili wananchi wajiunge nacho wasidhani wananchi wote wanaweza kuingia katika mtego huo wengine waking’amua inaweza kuwa hatari zaidi.
Mfano hai ulionekana bungeni mwaka jana pale wabunge ambao wengine walikuwa wakitoka CCM walipomkalia kooni aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha, Miundombinu na baadae Viwanda Biashara na Masoko, Basil Mramba, kwa kujenga zaidi eneo analotoka na kusahau sehemu nyingine.
Umefika wakati wa kuangalia maslahi ya wananchi kwanza badala ya kufuata siasa za kibaguzi ambazo hazina faida yoyote kwa taifa zaidi ya kutengeneza chuki kwa misingi ya siasa.