MATUKIO ya aibu yanaendelea kutokea ndani ya Jumuiya za Chama Cha Mapindizi, yaani Umoja wa Vijana (UVCCM) na Umoja wa Wanawake (UWT) katika mchakato wa kuwapata viongozi wake yanashangaza.
Safari hii napenda nilikunje jamvi la vijana na kulikunjua jamvi la Kina mama wa CCM, ambao nao wameibua maswali mengi kiasi cha kunifanya nijiulize kwa kina umuhimu wa jumuiya hiyo.
Inanibidi nirejee kwa karibu zaidi tukio lililotokea ndani ya kikao cha Kamati ya Siasa ya mkoa wa Dar es Salaam, ambako wagombea wawili wa nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa UWT, wanaelezwa kurushiana maneno makali hata kufikia hatua ya kutaka kuwa akina ‘Tyson’.
Hii ni aibu na ni aibu kubwa iliyofanywa na viongozi wenye heshima na dhamana kubwa katika nchi. Viongozi hawa ni sehemu ya kioo cha mwanamke wa kesho anayesoma shule za msingi anayejiandaa kuwa kiongozi siku zijazo kuchukua nafasi za kina mama hawa.
Ugomvi wa Waziri wa nchi ofisi ya Rais, Utawala Bora, Sophia Simba, na Mwenyekiti wa UWT Dar es Salaam, Janeth Kahama, umeitia doa kubwa jumuiya hiyo ambayo sasa nimebaini wazi kuwa haina sura ya utaifa bali ina sura ya kimaslahi zaidi kwa chama chao.
Maswali zaidi yanaibuka. Kama kweli viongozi hao wanaotegemewa kuliongoza kundi la wanawake wa CCM wanaanza kugombana leo, nini matokeo yake na mustakabali wa jumuiya hiyo?
Tukio hilo linaaibisha zaidi hasa linapomhusisha waziri mwenye dhamana ya Utawala Bora. Hivi anatoa picha gani na anataka kuwaambia watanzania kuwa anawezaje kuwasimamia katika misingi ya haki, sheria na utawala bora, kama anakuwa katika mazingira yanayokosa subira ndani ya vikao?
Hivi heshima kubwa anayoipata waziri mwenye dhamana hiyo ni kidogo kiasi gani kung’ang’ania kutaka kuvaana mwilini na kutupiana maneno machafu kwa ajili ya kugombea cheo cha UWT? Au Uenyekiti wa UWT ni zaidi ya uwaziri?
Ni hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alisema wazi kuwa umefika wakati wa kuwashitukia wanasiasa kwa kuwa hawajengi nchi ipasavyo na wengi wao hawasaidii vizuri ukuaji wa uchumi kwa kuwa ni wababaishaji.
Ukweli ndio huo. Nafasi ya wanasiasa inazika kabisa nguvu za wataalamu waliobobea, ambao ndio wanaofanya kazi kubwa ya kupanga mipango ya serikali na mbinu zote za kukuza uchumi wa nchi, lakini hawathaminiwi.
Wanasiasa hawa wanaogombana leo kwenye kila kona ya nchi wana mchango gani ambao unaweza kuhesabika kuwa ndio unaoonyesha ukuaji wa uchumi na utatuzi wa maisha duni ya wananchi wa Tanzania?
Wanasiasa ndio wanaoongoza kwa rushwa wakati wa kampeni za uchaguzi, ndio wanaotumia mali za umma kama magari na vitu vingine kufanyia kampeni na ndio walioliingiza taifa kwenye kashfa za ajabu za ufisadi.
Yapo mambo mengi ambayo watanzania wanapaswa kujiuliza nikirejea umuhimu na faida ya Msajili wa Vyama vya Siasa hapa nchini kuweka wazi msimamo wa chombo hicho kushinikiza maamuzi ya kisheria yanayoruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi katika chaguzi zijazo.
Bila hivyo, hali itazidi kuwa mbaya kwa kuwa fitina, majungu, kunyoosheana vidole hasa kwa watu wanaotoka katika chama kimoja kikubwa, chenye nguvu kama CCM. Lakini hali hii inawafikisha pabaya zaidi watanzania.
Hofu niliyo nayo ni kuwa endapo msajili akiyadharau maoni haya, utafika wakati ambao demokrasia itakumbatiwa zaidi na watu wenye fedha na kuwaacha masikini wenye uwezo wa kuongoza wakiwashuhudia vigogo wanavyogombania madaraka.
Ndiyo maana nauliza hivi hii UWT inawasaidia kweli wanawake wa kesho na kazi kubwa inayofanywa na jumuiya hiyo kwa manufaa ya wanawake wengine wasiokuwa wana CCM ni ipi?
Jumuiya hiyo inawaandaaje wanawake wa leo waliopo shuleni, ili waje wawe wanawake bora wa kesho na viongozi watakaoheshimika ambao wanapaswa kuiga tabia njema za wale walioko leo madarakani?
Wanawake wa UWT nadhani kabisa kwa mtazamo wangu hawafanyi kazi ya uwakilishi wa wanawake wote, nikimaanisha kuwa jumuiya hiyo iliundwa wakati wa mfumo wa chama kimoja, hivyo walikuwa na haki ya kuiita ‘Jumuiya ya Wanawake Tanzania.’
Nadhani umefika wakati kama inavyoitwa jumuiya ya Vijana wa CCM (UVCCM) jumuiya hiyo ya wanawake wa CCM ilipaswa kuitwa kwa kifupi (UWCCM) yaani Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi. Huo ndio ukweli na utabaki kuwa ukweli, ili kama wanawake hao wanagombana ijulikane wazi kuwa huo ugomvi ni wanawake ndani ya CCM na kwa vyovyote vile hauwahusu wanawake wote.
Nataka kuwarudisha nyuma mama zangu hawa wa CCM. Kwa muda wamekuwa wakishuhudia mmomonyoko mkubwa wa maadili ya watoto wa kike. UWT inafanya nini?
Wanawake wa UWT ndio wanaotarajiwa kuwa na mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa wanakisaidia chama chao na serikali yao kupambana na ongezeko la mimba za wanafunzi katika shule za msingi na sekondari. UWT inafanya nini?
UWT ndio wanaotakiwa kuwa kioo bora cha malezi na tabia njema katika familia. Ndio wanaotakiwa kukemea mila na desturi mbaya za kumnyanyapaa mwanamke na ndio wanaotakiwa kuhakikisha kuwa wana mkomboa mwanamke kutoka kwenye lindi la umaskini. Wanafanya nini?
Ndio wanaotakiwa kusimama kidete kuhakikisha mavazi ya aibu kwa watoto wao yanatoweka na kuwapa nasaha wanafunzi ili waweze kuepukana na vishawishi vya kupata mimba wakiwa na umri mdogo. Sijui UWT hapo walipo wanafanya nini?
Sipati jibu na sioni kazi kubwa inayofanywa na UWT kwa ajili ya kuleta mapinduzi ya mwanawake wa jumuiya hiyo na wengine wanaotarajia mipango ya maendeleo inayotolewa na serikali ya CCM iliyopo madarakani. Sioni hapo UWT inachokifanya.
Sijaona kampeni za wazi zinazofanywa na UWT ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wa kike wanapiganiwa kufa na kupona na kuwahamasisha wananchi kwa nguvu zote wawajengee mabweni wanafunzi wa kike kwa nia ya kuwapunguzia vishawishi vya kupata mimba. Sijaona na sifahamu kazi kubwa inayofanywa na jumuiya hiyo, ili kukomesha vitendo vya unyanyasaji dhidi ya mtoto wa kike.
Nadhani maswali yapo mengi kuliko majibu na ni wazi kuwa ugomvi na aibu inayoonyeshwa na wagombea wa jumuiya hiyo hadi kufikia hatua ya kutaka kupigana, hakuwezi kujibu maswali hayo na ni wazi maslahi yanayopiganiwa hapo sio ya mwanawake.
Mwenyekiti anayeshikilia nafasi ya UWT Taifa, Anna Abdallah, ana kila sababu ya kukemea vitisho vinavyoendelea kujitokeza kwenye mchakato huo, hasa akizingatia kuwa mwanawake wa sasa anachohitaji ni maisha bora na maisha hayo hayawezi kuletwa na wanawake wenye ubinafsi.
Siku zote watu wamekuwa wakiimba kuwa ‘ukimuelimisha mwanamke mmoja umelielimisha taifa zima.’ Tukiwatazama hawa wanaogombana leo wajiulize wako wapi akina Asha-Rose Migiro, Anna Tibaijuka, Getrude Mongella na wengine kadhaa ambao ni kielelezo cha wanawake wanaoshimiwa na mataifa.
Wanawake ndio tegemeo na chachu ya uchumi wa nchi, UWT inatakiwa ipate viongozi bora watakaoweza kujibu maswali ya wanawake wenzao, wenye dhiki, shida na taabu nyingi wanaoishi mijini na vijijini, vinginevyo, maadili ya Taifa yataendelea kumomonyoka.
cnyenyembe@yahoo.com
0754 301864
0787 862586