HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
jumatatu, 22 septemba 2008
Pekua Tovuti
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari


TAMWA yatangaza bingo kwa wanafunzi


na Mwandishi Wetu


CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kimeanzisha shindano la kuandika insha kuhusu utumikishaji na unyanyasaji watoto kingono kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na wale walio na umri chini ya miaka 18.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho, Ananilea Nkya, inaeleza lengo la shindano hilo ni kukuza uelewa wa watoto juu ya unyanyasaji huo na kuwawezesha kuwataja bila woga watu wanaowadhalilisha watoto kingono.

Pia lengo jingine ni kukusanya maoni ya wanafunzi hao juu ya nini kifanyika katika kukabiliana na vitendo hivyo katika jamii.

Taarifa hiyo inaeleza washiriki watatakiwa kujibu kwa ubunifu kwa kutoa maelezo ya nini kifanyike, ili watoto waepukane na kulindwa dhidi ya vitendo vya unyanyasaji na utumikishwaji kingono.

Maelezo ya washiriki yanapaswa yajikite katika kuibua mawazo ambayo yanatekelezeka kwa kufafanua jukumu la viongozi na kila mwanajamii, wakiwemo watoto wenyewe, wazazi, walimu, viongozi wa mtaa/kijiji kata, wilaya, mkoa na serikali kuu katika kupambana na hatimaye kukomesha ukatili huo dhidi ya watoto.

Inaelezwa insha hizo zinaweza kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza na kila mshiriki atatakiwa kuandika jina kamili, jinsi, umri na shule anayosoma na kutuma insha iliyochapishwa isiyozidi maneno 1,000 au iliyoandikwa kwa kalamu, isiyozidi kurasa mbili.

Mshindi wa kwanza katika shindano hilo atajipatia fedha taslimu sh 300,000, mshindi wa pili sh 200,000 na mshindi wa tatu sh 100,000. Washindi wengine 10 watajinyakulia sh 50,000 kila mmoja.

Taraifa hiyo inaeleza insha 10 bora zitachapishwa kwenye kitabu kinachoandaliwa kwa ushirikiano na vyama vya wanahabari vya Kenya (AMWIK), Ethiopia (EMWA), Uganda (UMWA) na Tanzania (TAMWA).

Baadaye kitabu hicho kitasambazwa kwenye shule mbalimbali, ili kuwaelimisha watoto juu ya vitendo vya unyanyasaji na utumikishaji kingono na kuwawezesha kushiriki katika kampeni mbalimbali za kupinga vitendo hivyo.

Mwisho wa kupokea insha hizo Oktoba 17 mwaka huu na washindi watatangazwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini, wiki mbili baada ya kufungwa kwa shindano hilo.


juu

Warning: mysql_connect() [function.mysql-connect]: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2) in /hermes/bosweb/web098/b983/glo.freemanm2/include/comment.php on line 9
I cannot connect to the database because: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2)