JAMII imetakiwa kubadilika na kuachana na matumizi ya kemikali katika kukabiliana na maradhi mbalimbali na badala yake watumie vyakula na mimea mingine kukabiliana na maradhi ambayo yanaonekana kushindikana hospitali.
Akizungumza na waandishi wa habari katika zahanati ya tiba maradhi yasababishwayo na tabia za ulaji, uvaaji na vitu vingine vya namna hiyo, daktari wa kituo hicho kilichopo katika soko la Makumbusho, Allice Magasa, alisema walioshindikana hospitali waende katika kituo hicho.
Alisema matumizi ya dawa zenye kemikali yameathiri kwa kiasi kikubwa maisha ya kawaida ya walio wengi na kuwasababishia matatizo mengine ambayo kati yao yamewasababishia vifo au maradhi yanayotajwa kuwa hayaponi.
“Hakuna ugonjwa usiopona, yote ni madhara ya kemikali tunazokutana nazo katika vyakula, dawa za kinga mbalimbali na hata zile za maradhi ambayo yanaonekana kuwa ni ya kawaida kama malaria,” alisema.
Dk. Allice alisema watu wanatakiwa kubadilika na kujua wanakula nini, kina faida gani kwao na wanajikinga vipi na maradhi mbalimbali kwa kutumia mitindo ya maisha badala ya kukimbilia katika dawa ambazo zinawaletea madhara.
“Watu wanapona kwa kutumia aina mbalimbali za mimea na vyakula tunavyokula kila siku, hilo nina ushahidi nalo na tafiti mbalimbali zinabainisha,” alisema na kuongeza kila siku wanapokea wagonjwa kati ya 15 hadi 20.
Alisema jamii inapaswa kuamka na kutumia tiba za mimea kujitibu maradhi mbalimbali kwa gharama nafuu badala ya kutumia mamilioni katika kemikali. Alisema amepata elimu hiyo Chuo Kikuu cha Tiba za Mimea, Zanzibar.
Kituo hicho ambacho kimeanzishwa nchini miaka miwili iliyopita kina tawi lake eneo la Tabata na mipango inafanywa kupanua zaidi huduma za kituo hicho ambacho kwa siku za karibuni kimeonekana kimbilio la walio wengi.