WAFANYAKAZI wa Benki ya National Microfinance (NMB), leo wanatarajia kuanza mgomo nchi nzima kwa lengo la kuishinikiza serikali kuwalipa mafao yao pamoja na kupatiwa asilimia tano ya hisa ambazo zilitengwa kwa ajili ya wafanyakazi wakati serikali ilipoamua kuuza hisa zake.
Mgomo huo umetokana na notisi ya saa 48 iliyotolewa na Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO), Septemba 19, ikielezea kusudio la wafanyakazi hao kuanza mgomo leo.
Notisi hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa TUICO, Boniface Nkakatisi, kwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ben Christiaanse, ilisema wafanyakazi hao wamefikia hatua hiyo baada ya majadiliano ya muda mrefu kati yao, serikali na uongozi wa benki hiyo, kushindikana.
“Serikali kwa sababu inazozijua, imekataa kusaini makubalino hayo na hiyo maana yake ni kwamba makubaliano kati ya pande hizo mbili, yameshindikana na kuacha malalamiko ya msingi ya wafanyakazi yakibaki palepale,” ilisomeka sehemu ya notisi hiyo.
Kwa mujibu wa notisi hiyo, wafanyakazi hao wanakusudia kuanza mgomo huo leo na utaendelea hadi hapo madai yao ya msingi yatakapotekelezwa.
Wakati wafanyakazi hao wakijiandaa kuanza mgomo huo wa kwanza kwa benki hiyo leo, kwa upande wake uongozi wa NMB, umetoa taarifa nzito kwa wafanyakazi wake wote nchini, ikiwatahadhalisha watakaoshiriki katika mgomo huo.
Taarifa hiyo iliyosambazwa katika matawi yote nchini na kusainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Christiaanse na Tanzania Daima kupata nakala yake, ilisema mgomo huo ni batili na kuwaonya watakaoshiriki kwamba watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Mkurugenzi huyo alitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kukatwa mshahara kwa siku zote ambazo wafanyakazi watashiriki kugoma pamoja na kukabiliwa na hatari ya kuvunja mikataba yao ya kazi.
Mkurugenzi huyo alisema mgomo huo unaihusu serikali kutosaini makubaliano ya kuongezewa masilahi ya wafanyakazi hao pamoja na mgawo wa asilimia tano ya hisa za benki hiyo kama walivyoahidiwa, lakini hauwahusu wateja, hivyo isingependa kuona wakihangaika kwa kukosa huduma.
“Mgomo huo hauhuhusu uongozi wa NMB na wateja wake, hivyo hatutaki kuona wateja wakiathirika kwa namna yoyote.
“Uongozi unataka kuwaambia wafanyakazi kuwa mgomo huo ni batili, hasa ukizingatia kuwa suala hili liko mahakamani, hivyo hakuna mgomo unaoruhusiwa hadi hapo suala litakapomalizika kisheria, kinyume cha hapo ni batili,” ilisema taarifa hiyo kwa wafanyakazi wa NMB wote nchini.
Christiaanse alisema katika taarifa hiyo kuwa suala la mgomo ni haki ya mfanyakazi kama linavyoonekana kwenye sheria ya ajira, lakini ufanyike baada ya kushindikana kwa majadiliano na taratibu zingine za kisheria, lakini suala la wafanyakazi wa benki hiyo, bado liko mahakamani na kusisitiza kuwa mgomo wao leo ni batili.
Kutokana na hali hiyo, mkurugenzi huyo aliwataka wafanyakazi wote kutoshiriki katika mgomo huo na badala yake waendelee kuchapa kazi ya kutoa huduma kwa wateja kama kawaida, kwani malalamiko yao yanashughulikiwa.
“Uongozi wa NMB, unafuatilia kwa karibu sana suala la madai ya wafanyakazi hao na unasikitika kuona kwamba uamuzi wa mgomo huo unachukuliwa kabla ya kupata msimamo wa mwisho wa serikali,” alisema.
Kwa upande wa wateja, mkurugenzi huyo aliwahakikishia wateja wa benki hiyo kuwa wakati wa mgomo huo, uongozi wao utajitahidi kadiri inavyowezekana kuhakikisha huduma zote muhimu za kibenki zinaendelea kutolewa kwa wateja kama kawaida.
Hata hivyo habari zaidi ambazo Tanzania Daima imezipata, zilisema kuwa leo kutakuwa na ulinzi mkali katika matawi yote ya benki hiyo nchini.
Kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa NMB, Shay-Rose Bhanji, alisema uongozi wa benki utahakikisha kunakuwapo ulinzi wa kutosha katika matawi yote nchini kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa mali za wateja na benki yenyewe.
“Kwa sasa ni vigumu kusema kama tutafunga matawi au la kutokana na hali itakavyokuwa hii leo, lakini kama tukiona ulinzi wa tawi lolote uko shakani, tunaweza kufunga, ila nawahakikishia wateja kuwa huduma za NMB leo zitakuwapo kama kawaida,” alisema.
Wafanyakazi wa NMB, wamekuwa katika mvutano wa muda mrefu na uongozi wa benki hiyo, wakidai kupewa marupurupu yao pamoja na kupata gawio la asilimia tano ya hisa za Serikali kama walivyolipwa wenzao wa (NBC).
Wiki iliyopita, TUICO ilitoa baraka kwa wafanyakazi wa NMB kugoma baada ya kupigwa danadana kwa muda mrefu.
Uamuzi huo ulipitishwa na Kamati ya Utendaji ya TUICO, Kanda ya Dar es ambayo ilibainisha kuwa wafanyakazi hao, wana haki kuandamana, wakishinikiza kupewa masilahi yao kutokana na makubaliano ya mwekezaji wa NMB.
Mwenyekiti wa TUICO, Hassan Athuman, alisema wafanyakazi wa NMB, toka awali walishakubaliana kulipwa mafao yao na asilimia tano ya hisa toka mwaka 1995.
Mwenyekiti wa Kamati ya Majadiliano ya NMB, Joseph Massana, alisema jana kuwa uvumilivu waliokuwa nao umekwisha, hivyo kitachofuata kitajulikana leo.
Alisema mgomo wa wafanyakazi wa NMB ni sehemu ya masilahi yao ambayo wanatakiwa kupata na si kuwazungusha, hali ambayo ni tofauti na mkataba wao.
Hata hivyo aliitaka serikali kuheshimu hatua zitakazochukuliwa na wafanyakazi hao, kwani wana madai ya msingi.
NMB ilipobinafsishwa, serikali ilikuwa na asilimia 51 ya hisa na hivi karibuni iliuza hisa zake 21 kwa wananchi na kubakia na asilimia 30 ya hisa zake.