HABARI MPYA KITAIFA DAR MIKOANI TAHARIRI MAKALA MICHEZO
jumatatu, 22 septemba 2008
Pekua Tovuti
Gazeti la Jana
Matangazo
Bei zetu
Wasiliana nasi
Tuma habari


Walalamikiwa kuchafua maji Mto Mara


na Chris Mang’era, Tarime


WAJUMBE wa Jumuiya za Watumia Maji katika Bonde la Mto Mara, wameulalamikia mgodi wa dhahabu wa North Mara uliopo wilayani Tarime, kuwa unachangia kuchafua rasilimali za maji na mazingira katika bonde hilo.

Wajumbe hao kutoka vijiji 14 vilivyo jirani na Bonde la Mto Mara, walitoa malalamiko hayo mwishoni wa wiki kwenye mafunzo yao kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto za uchafuzi wa maji na uharibifu wa mazingira katika Bonde hilo.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na kuwezeshwa na Mradi wa Usimamizi wa Bonde la Mto Mara na kuwezeshwa na Meneja wa mradi huo, William Kasanga na Ofisa wa mradi huo katika kitengo cha maji, Sariro Mwita.

Walilalamika kuwa kumekuwepo na uchafu unaotokana na shughuli za mgodi huo zikiwamo za kusaga na kuosha dhahabu ambao hutiririka na kuingia katika Mto Mara na hivyo, kuhatarisha watumiaji wa maji ya mto huo na viumbe hai ndani ya maji.

Meneja wa Mradi wa Usimamizi wa Bonde la Mto Mara, Kasanga, alipoulizwa alisema hana jibu la moja kwa moja kuhusu malalamiko hayo na kuwashauri wakazi wa vijiji husika kutumia Serikali za vijiji vyao kushughulikia kero hiyo.

Juhudi za mwandishi wa habari hizi kumpata Ofisa Mawasiliano wa mgodi huo, Emmanuel Nyasigo, hazikuzaa matunda baada ya kumpigia simu yake ya mkononi mara kadhaa ikiita bila kupokewa.

Baadhi ya mada zilizotolewa katika mafunzo hayo ni namna ya kuepuka vitendo vya uchafunzi wa maji na uharibifu wa mazingira katika Bonde la mto huo kama vile kukata miti, kuchoma moto misitu na kuendesha kilimo kisichozingatia uhifadhi wa mazingira.

Walielimishwa pia sheria na sera za usimamizi wa mazingira na ardhi vijijini ili wawe chachu ya uhamasishaji wa matumizi endelevu ya rasilimali za maji na mazingira katika bonde hilo.

Meneja wa mradi huo, Kasanga, alisema ofisi yake inaendelea kuwajengea uwezo wanavijiji husika katika dhana nzima ya kusimamia rasilimali za bonde hilo ili kunusuru tatizo la upungufu wa wingi na ubora wa maji ya Mto Mara.


juu

Warning: mysql_connect() [function.mysql-connect]: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2) in /hermes/bosweb/web098/b983/glo.freemanm2/include/comment.php on line 9
I cannot connect to the database because: Can't connect to local MySQL server through socket '/var/run/mysqld/mysqld.sock' (2)