MBUNGE wa Kishapu, mkoani Shinyanga, Fred Mpendazoe (CCM), amefuta ziara ya kulitembelea jimbo lake, baada ya kupata taarifa za kuwapo njama za kutaka kuvuruga mikutano yake kwa kumzomea na kufanya vurugu.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Mpendazoe alisema mipango hiyo imeandaliwa na baadhi ya watu waliokerwa na michango yake wakati wa bunge la bajeti na wameamua kufanya hivyo ili kulipiza kisasi.
Alisema watu hao, hivi sasa wameanza kumfuata jimboni ili kumvurugia mikutano na kumchafulia jina kwa wapiga kura wake.
Mbunge huyo alisema taarifa alizozipata kutoka kwa baadhi ya wapiga kura wake, zinasema kuwa baadhi ya watu waliopandikizwa kuuliza maswali katika mikutano yake kuhusu utekelezaji wa ahadi alizozitoa wakati wa kampeni pamoja na kuibua kero ambazo bado zinawakabili wananchi.
Kutokana na hali hiyo, mbunge huyo alisema amelazimika kufuta ratiba ya ziara zake ili kuepuka madhara ambayo yangeweza kutokea kwa wananchi watakaohudhuria mikutano yake.