UJENZI wa daraja linalounganisha nchi za Tanzania na Msumbiji ambalo linaendelea kujengwa katika eneo la Mtambaswala, Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara, utakamilika Novemba 2009.
Awali kwa mujibu wa mkataba huo, Mkandarasi wa ujenzi wa daraja hilo la kihistoria, M/S China Geo-Engineering Corporation kutoka China, alitakiwa awe amekamilisha ujenzi huu, Novemba mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Miundombinu kwa vyombo vya habari jana, ilisema hatua hiyo ilibainishwa wakati wa kikao cha pamoja kilichofanyika Septemba 19, mji wa Negomane, Msumbiji, kilichowakutanisha mawaziri wenye dhamana ya ujenzi wa daraja hilo kutoka Tanzania na Msumbiji .
Mawaziri waliohudhuria kikao hicho ni Fellicio Pedro Zacarias ambaye ni Waziri wa Ujenzi na Nyumba wa Jamhuri ya Msumbiji wakati Tanzania iliwakilishwa na Naibu wa Waziri wa Miundombinu, Hezakiah Chibulunje.
Uzinduzi wa ujenzi wa Daraja la Umoja ulifanyika mwaka 2005 kwa marais Benjamin William Mkapa wa Tanzania na Rais Armando Emilio Guebuza wa Msumbiji, kuweka jiwe la msingi katika eneo hilo la mradi.
Daraja la Umoja ambalo litagharimu sh bilioni 30, lina urefu wa mita 720, likiwa na uwezo wa kupitisha magari manne na sehemu ya watembea kwa miguu kwa wakati mmoja.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwakilishi wa Mhandisi Mshauri kutoka Kampuni ya Norconsult, ilielezwa kuwa sababu kubwa ya kuchelewa kukamilika kwa mradi huu kwa mwaka mmoja zaidi, ni matatizo yaliyojitokeza katika usanifu wa daraja hilo.